Habari za Punde

WAKUTUBI WASISISTIZWA KUHAMASISHA WANAFUNZI KUZITUMIA MAKTABA

Na Sabiha Khamis  Maelezo    09/10/2020

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Zanzibar Suleiman Yahya Ame amewataka wakutubi nchini kuweka Mikakati ya kuhakikisha Wanafunzi wanazitumia maktaba katika masomo yao ili kuhakikisha wanafaulu na kuondosha O.

Ameyasema hayo katika sherehe ya maadhimisho ya wiki ya Maktaba za skuli, iliyoandaliwa na Skuli ya Sekondari ya Kwarara kwa kushirikiana na Jumuiya ya kukuza maktaba za skuli Zanzibar huko Kwarara Wilaya ya Magharibi “B”

Amesema ili Wanafunzi waweze kufaulu vizuri mitihani yao hakuna budi kutumia Maktaba na kufuata sheria za maktaba jambo ambalo litaweza kuleta ufaulu mzuri katika masomo.

Aidha ameipongeza Jumuiya ya kukuza Maktaba za Skuli Zanzibar kwa kushirikiana na walimu katika kuwahamasisha wanafunzi kutumia maktaba kwa maendeleo ya masomo yao.

Nae Rais wa Jumuiya kukuza Maktaba za Skuli Zanzibar ambae pia ni Mhadhir wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Dkt.Haji Ali Haji amewataka wakutubi kujiendeleza zaidi kielimu ili waweze kukabiliana na ushindani wa utumiaji wa maktaba katika sehemu mbalimbali.

“Wanafunzi wapatiwe elimu ya Maktaba ili kuupunguza division “0” katika masomo yao” alisema Rais wa Jumuiya kukuza Maktaba za Skuli Zanzibar.

Hata hivyo alieleza kuwa Jumuiya ipo tayari kutoa huduma popote na muda wowote watakapohitajika katika kutoa elimu ya kutumia Maktaba.

Kwa upande wake Mkutubi wa Maktaba ya Skuli ya kituo cha Waalimu (T.C) Bububu Khadija Khamis Hamdani amesema walimu wanawajibu wa kutunza Maktaba na vitendea kazi vilivyomo kwani ndio vinavyosaidia katika ufaulu wa wanafunzi.

Mbali na changamoto zinazowakabili amewaomba walimu kuwawekea vipindi vya maktaba katika ratiba ya vipindi vya skuli.

Maadhimisho hayo ya wiki ya Maktaba za Skuli Yameandaliwa na Skuli ya Sekondari ya Kwarara na Jumuiya ya kukuza Maktaba za Skuli zanzibar ambapo kauli mbiu ni “ONDOA ZIRO KWA KUTUMIA MAKTABA”


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.