Habari za Punde

Aliyekuwa Waziri wa Elimu na mafunzo ya amali akabidhi ofisi kwa Waziri wa Elimu mpya

Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe Riziki Pembe Juma akimkabidhi Waziri wa Elimu na mafunzo ya Amali, Mhe Simai Mohammed Said baadhi ya vitabu muhimu vya kiofisi baada ya kufanyika makabidhiano katika Wizara ya Elimu hapo Mazizini leo.
Waziri wa Elimu na mafunzo ya amali akifanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Mhe Riziki Pembe Juma wa baada ya makabidhiano katika Wizara ya Elimu hapo Mazizini leo.

Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri.


Na Mwandishi wetu


 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imefanya makabidhiano ya ofisi kwa aliekuwa Waziri wa Wizara hiyo Mhe Riziki Pembe Juma ambae kwa sasa ni Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi na kumkabidhi Mhe Simai Mohammed Said.

Hafla hiyo ya makabidhiano imefanyika katika ukumbi wa Wizara hiyo Mazizini Mjini Unguja.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo aliekuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma ameushukuru uongozi wa Wizara hiyo kwa malezi na ushirikiano mkubwa waliompa katika kipindi chote cha uongozi wake ndani ya Wizara hiyo na kuweza kuzalisha viongozi walioweza kupanda kutoka Naibu Waziri na kuwa Waziri kamili.
Aidha Mhe Riziki ameiahidi Wizara hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa hati miliki wa maeneo ya Skuli, na majengo yake ili kuleta maendeleo katika Elimu na Serikali kwa ujumla.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said Amesema ataendeleza juhudi za Mhe Riziki Pembe Juma na ataongeza juhudi ili kuhakikisha anatimiza maagizo yote ya sekta ya elimu yaliopo katika ilani ya chama cha Mapinduzi.
Hata hivyo Mhe Simai amewasisitiza watendaji wa Wizara kuendana na mabadiliko na kasi ya Mhe Rais kwa kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ili kuyafikia malengo ya maendeleo ya uchumi wa buluu.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar dkt Idrissa Muslim Hija ameipongeza Wizara yake kwa kuendelea kuzalisha viongozi makini na kumtaka Mhe Simai na Mhe Riziki kuendana na kasi ya mabadiliko ili kuendelea kuliletea Taifa maendeleo zaidi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Naibu Katibu Mkuu Taaluma wa Wizara hiyo Bi Madina Mjaka Mwinyi amesema umoja na ushirikiano katika kazi ndio mafanikio ya sekta ya elimu nchini hivyo amewaahidi viongozi wote hao kuendelea kuwapa ushirikiano ili kueleta maendeleo katika nchi.
Katika hafla hiyo Mhe Riziki amemkabidhi Mhe Simai zana za kutendea kazi ikiwemo sera ya elimu, ilani ya Chama cha Mapinduzi na ripoti ya taarifa ya makabidhiano ambayo imekusanya majukumu ya Idara zote za Wizara na changamoto zake ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.