Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais , Mhe Hemed aendelea na ziara kisiwani Pemba afika Hospitali ya Micheweni na kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Nyumba za Wananchi walioathirika na Maafa

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akipata maelezo kutoka kwa Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Dr. Mbwana Hamad Shoka alipofanya ziara fupi kuangalia huduma za Afya.
Mheshimiwa Hemed na ujumbe wa wake akikagua Chumba cha Upasuaji kwenye Hospitali ya Wilaya Micheweni na kupata maelezo ya kina jinsi ya utendaji unavyoendelea.
Daktari Dhamana wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Dr. Mbwana Hamad Shoka kushoto akimuelezea Mh. Hemed upungufu wa baadhi ya Vifaa na Watendaji unaoikabili Hospitali ya Micheweni
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akiutaka Uongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufanya utaratibu wa kuwaajiri Vijana waliosomea taaluma ya Sekta ya Afya kujaza  maeneo yenye upungufu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman akikagua Maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Nyumba za Wananchi walioathirika na Maafa hapo katika Kijiji cha Tumbe  Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Msimamizi wa Ujenzi wa Nyumba za Wananchi walioathirika na Maafa Mhandisi Ernest Mbaguka akimfahamisha Mhe. Hatua kubwa iliyofikiwa ya ujenzi wa Majengo ya Mradi huo ukiwa katika hatua za kukamilika.
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Tumbe mara baada ya kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Mradi wa Nyumba za Wananchi walioathirika na Maafa.

Mzee Juma Kombo Dadi aliyebeba Gango lenye Picha za Baraza la Kwanza na Afro Shirazi Party akiwa na Wananchi wenzake wakimsikiliza kwa Makini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman alipokuwa akiwasalimia.

Picha na – OMPR – ZNZ


Mkurugenzi wa Bohari Kuu Zanzibar ametakiwa kuharakisha upatikanaji wa Dawa katika Bohari Kuu ya Pemba ili kuepuka upungufu wa Dawa zinazohitajika kupatiwa Wananchi wanaofuata huduma za Afya katika Hospitali na Vituo vya Afya  Kisiwani Pemba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii baada ya kufanya ziara Maalum ya kuangalia upatikanaji wa huduma za Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mh. Hemed akishuhudia upungufu wa baadhi ya Dawa ndani ya Ghala ya Hospitali hiyo ambazo kwenye Ghala Kuu zipo alisema iwapo kuna tatizo katika mfumo wa Mtandao wa usambazaji Dawa baina ya Bohari Kuu na Hospitali Washirika lazima litafutiwe ufumbuzi wa haraka ili kuondosha usumbufu unaoweza kuwaathiri Wananchi.

Alisema haipendezi kuona hitilafu nyingi zilizojichomoza kwa kipindi kirefu na kuleta changamoto katika utendaji kazi katika maeneo mengi ya huduma baadhi ya Viongozi na Watendaji husingizia uwepo wa maambukizi ya Corona Nchini Virusi ambavyo vimeisumbua Jamii ndani ya Miezi sita wakati matatizo mengine yana zaidi ya Mwaka sasa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhimiza Uongozi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuandaa utaratibu wa kuwaajiri Vijana Wataalamu waliopata mafunzo mbali mbali ya fani ya Afya ili kujaza mapungufu yaliyomo ndani ya Hospitali na Vituo vya Afya Nchini.

Alisema yapo maeneo kadhaa ya huduma za Afya katika baadhi ya Hospitali yaliyokosa Watendaji akitolea mfano vitengo vya Maabara, upasuaji na hata  huduma za Mama na Mtoto wakati Vijana wenye Taalum hiyo wameachwa na kuzagaa Mitaani.

“ Wale waliosomeshwa  na tayari wamefanikiwa kuwa na Taaluma ya kutosha ni vyema wakatafutiwa utaratibu wa kuajiriwa badala ya kuachwa wakaendelea kuzurura mitaani na matokeo yake mara hujiingiza katika vitendo visivyokubalika”. Alisisitiza Mh. Hemed Suleiman.

Akizungumzia madeni na haki za Watendaji wa Afya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Uongozi wa Wizara ya Afya lazima ujipange vyema katika kuona masuala hayo muhimu yanapatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu ili shughuli ya huduma za Afya iendelee kuwafikia Wananchi.

Mheshimiwa Hemed alisema Viongozi wengi wamekuwa wakipokea malalamiko ya kila mara kutoka kwa Watendaji wa Sekta ya Afya kucheleweshewa haki zao yakiwemo yale ya muda wa ziara wa kazi pamoja na madeni makubwa ya Huduma za Umeme mambo ambayo kama hazikuchukuliwa hatua za dharura yanaweza kuleta athari muda si mrefu.

Mapema Daktari Dhama wa Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Dr. Mbwana Hamad Shoka alisema upatikanaji wa huduma za Mama na Mtoto kwenye Hospitali hiyo zinaendelea kuimarika na kupelekea vifo vya akina Mama na Watoto vimepungua.

Hata hivyo Dr. Mbwana alisema bado upo upungufu wa Wauguzi wa kusimamia huduma hizo kutokana na ongezeko la Akina Mama wanaohitaji huduma hizo muhimu zinazopaswa kuwa na uangalifu wa hali ya juu.

Akigusia Kitengo cha Upasuaji kwenye Hospitali hiyop ya Wilaya Daktari Dhamana Mbwana alisema Hospitali hiyo imefanikiwa kuwa na jingo la kisasa kwa ajili ya shughuli za upasuaji lililojengwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo.

Alisema huduma za upasuaji wa maradhi mbali mbali chini ya usimamizi wa Mtaalamu kutoka Nchini Ujerumani Dr. Hans tayari zimeanza takriban Miaka miwili sasa.

Daktari Mbwana alifahamisha kwamba huduma za upasuaji zinaweza kuimarika zaidi endapo kutachukuliwa juhudi za makusudi za kukamilisha baadhi ya vifaa muhimu ndani ya Chumba hicho kinachotoa huduma muda wote wa saa 24 kutegemea uwepo wa Mgonjwa anayehitaji kupatiwa huduma hiyo.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata wasaa wa kuzikagua Nyumba zinazojengwa na Serikali kupitia Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa kwa ajili ya Wananchi waliopatwa na Maafa zinazoendelea kujengwa katika Kijiji cha Tumbe  Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Makame Khatib alimueleza Mh. Hemed kwamba Nyumba hizo 15 zitakazokuwa na uwezo wa kuchukuwa Familia Mbili kwa kila nyumba  zimekwenda sambamba na uwezo wa Skuli, Maduka, Msiki pamoja na Kituo cha Afya.

Nd. Makame alisema Mradi huo umezingatia upatikanaji wa huduma zote muhimu anazopaswa kuzipata Mwanaadam ili Wananchi watakaobahatika kuishi eneo hilo wasisumbuke kufuata huduma nyengine masafa ya mbali.

Akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Tumbe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla aliwataka waendelee kusimamia Amani ya Taifa wakati Serikali inajipanga kuwapatia Maendeleo kama ilivyoahidiwa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.