Habari za Punde

Rais Dk Hussein Ali Mwinyi aagiza kutafutwa eneo muafaka kwa ajili ya wafanyabiashara waliopo eneo la kijangwani

                                         

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wafanyabiashara wa Soko la Kijangwani Komba wapya  na kuwataka kuendelea kufanya biashara hapo mpaka watakapopatia eneo  jingine kuendelea na Biashara zao. 

                     

RAIS wa  Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi  ameutaka Uongozi wa Serikali ya Mkoa wa Mjini Magharibi kushirikiana na Uongozi wa Jiji la Zanzibar pamoja na wafanyabiashara, kutafuta eneo muafaka kwa ajili ya wafanyabiashara waliopo eneo la Kijangwani.

Dk. Mwinyi ametoa agizo hilo leo wakati alipofika eneo la kibiashara la Kijangwani, Wilaya Mjini Unguja na kuzungumza na wafanyabiashara wa hapo ambao wamekuwa katika utaratibu wa Serikali wa kuhama eneo hilo ili  kupisha mradi wa kituo cha Usafiri.

Amewataka viongozi wa taasisi hizo kufanikisha agizo hilo mapema iwezekanavyo, sambamba na kuliwekea miundo mbinu muhimu inayohitajika ili kuwawezesha wafanyabaishara hao kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Aidha, Dk. Mwinyi aliwataka viongozi hao kuhakikisha wafanyabaishara hao wanaendelea kubaki katika eneo hilo la Kijangwani wakati juhudi za kuwapatia eneo jengine litakalotumika kwa muda zikiendelea.

“Katika muda mfupi ujao tupate soko la muda ili kupisha kuanza kwa ujenzi wa mradi eneo hili”, alisema.

Alisema dhamira ya Serikali ya kuwapatia eneo la kudumu kwa ajili ya  wafanyabiashara hao litachukuwa muda, hivyo ni vyema wakati huu juhudi zikafanyika kupata eneo la muda ambalo litakidhi mahitaji ya kibiashara.

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali itaendelea na dhamira yake ya kuwawekea mazingira bora wafanyabiashara wa Zanzibar na hivyo akawataka kuunga mkono azma ya Serikali ya kuanzisha mradi huo wenye manufaa makubwa kwa wananchi.

Vile vile Rais Dk. Mwinyi aliwataka kutoa mashirikiano kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuifanya Zanzibar inakuwa katika mazingira ya usafi muda wote.

Mapema, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Hassan Khatib alisema Ofisi yake ilalilazimika kuchukua hatua za kuwaondosha wafanyabaishara hao  eneo la Kijangwani, kwa kuzingatia mradi uliolengwa kutekelezwa eneo hilo uko karibu kuanza.

Alisema kabla ya hatua za kuwataka wafanyabiashara hao kuhama eneo hilo, walifanya utafiti na kubaini vibanda vingi viliopo eneo hilo vilivyojengwa kwa ajili ya biashara   vimehamwa na wahusika kurejea Darajani.

Alieleza kuwa kabla eneo hilo lilikuwa na wafanyabaishara wapatao 600, idadi ambayo imepungua hadi kufikia wastani wa wafanyabiashara 50 katika siku za hivi za hivi karibuni.

Aidha, alisema katika mkakati wa kuhakikisha wafanyabaishara wa eneo hilo wataweza kuendelea vyema na shughuli zao, walilazimika kuyakagua maeneo tofauti, ikiwemo Saateni na Kibandamaiti na hatimae kulichagua na eneo la Ijitmai ya zamani kutokana na mazingira yaliopo.

Nae, mmoja wa viongozi wa wafanyabiashara wa eneo hilo la Kijangwani Maryam Abdalla alisema hatua ya kuwahamisha eneo hilo na kuhamishia biashara zao katika eneo la ijtmai ya zamani, itasababisha kuua kabisa mitaji yao kibiashara.

Kiongozi huyo alisema kwa umoja wao wafanyabaishara hao hawakaidi agizo la kuhama eneo hilo kwa vile wanatambua kabla kuwa walipewa kulitumia kwa muda, lakini haliwawezesha kupata faida kwa vile soko kuu la Mwanakwerekwe lipo hatua chache na eneo hilo.

Alitumia fursa hiyo kumuomba Rais Dk. Mwinyi kuwapatia eneo la kudumu lililo muafaka na lililo na miundombinu ili kuendeshea biashara zao, kwa kuzingatioa ahadi yake wakati wa kampeni za Uchaguzi mkuu uliopita ya kuwawekea mazingira mazuri ya kibiashara, pale chama cha Mapinduzi kitakapopata ushindi.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.