Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Balozi wa Morocco Nchini Tanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni  wake Balozi wa Morocco Nchini Tanzania Mhe Abdelilah Benryane (kushoto) alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo,ambapo pia Balozi alimpongeza Rais kwa ushindi wake katika uchaguzi Mkuu uliopita.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na  mgeni wake Balozi wa Morocco Nchini Tanzania Mhe Abdelilah Benryane (kushoto) mara baada ya mazungumzo yao leo alipofika Ikulu Mjini Zanzibar.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiameeleza azma ya Zanzibar kukuza na kuimarisha uhusiano kati yake na Morocco hasa katika sekta ya utalii.

Dk. Hussein aliyasema hayo leo katika mazungumzo kati yake na Balozi wa Ufalme wa Morocco katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abdelilah Benryane, mazungumzo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Hussein alisema kwamba kutokana na Morocco kupata mafanikio makubwa katika sekta ya utalii, ni vyema Zanzibar ikapanua wigo kutoka nchi hiyo.

Alisema kuwa kwa vile Zanzibar inategemea sana sekta ya utalii katika uchumi wake itakuwa vyema kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya pande mbili hizo ili Zanzibar ipate mafanikio kama yale iliyoyapata Morocco katika sekta hiyo.

Dk. Hussein alirejesha salamu za pongezi zilizotoka kwa kiongozi wa Morocco kupitia Balozi huyo Mfalme Mohammed VI, zilizomtakia kazi njema na mafanikio katika uongozi wake mpya wa Urais wa Zanzibar huku akiahidi kuzidisha ushirikiano wake kwa nchi hiyo.

Aidha, Dk. Hussein alimueleza kiongozi huyo juhudi zitakazochukuliwa  na Serikali anayoiongoza katika kuimarisha sekta ya utalii na kusisitiza haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja katika sekta hiyo hasa ikizingatiwa kwamba Morocco ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika iliyopiga hatua kubwa katika sekta ya utalii.

Pamoja na hayo, Dk. Hussein alimueleza Balozi huyo umuhimu wa kushirikiana katika sekta nyenginezo za maendeleo hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina kiu kubwa ya maendeleo hivi sasa.

Sambamba na hayo, Dk. Hussein alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa Morocco kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo.

Nae Balozi wa Morocco katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Abdelilah Benryane,alianza kwa kumfikishia salamu za pongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kutoka kwa Mfalme wa Morocco Mohammed VI, kufuatia ushindi wa kishindo wa Urais wa Zanzibar.

Balozi huyo alimueleza Rais Dk. Hussein kwamba Morocco inajivunia uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yake na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Balozi  Abdelilah Benryane, alisema kuwa Morocco iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika sekta ya utalii, pamoja na sekta nyengine zote muhimu huku akieleza azma ya nchi yake ya kutoa nafasi za masomo katika kada mbali mbali kwa wanafunzi wa elimu ya juu wa Zanzibar ikiwa ni pamoja na nafasi za masomo ya elimu ya dini.

Balozi huyo pia, alieleza utayari wa nchi yake katika mashirikiano kupitia mafunzo ya masuala ya kitalii kupitia chuo chake ambacho kina mahusiano na nchi kadhaa za Ulaya na nyenginezo duniani

Aidha, alieleza haja ya kuwepo mashirikiano ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kwa wanafunzi wa Zanzibar na wale wa nchi yake kutokana na nchi hiyo kuwa na vyuo vingi vinavyotoa mafunzo kadhaa.

Akizungumzia juu ya sekta ya utalii, alisema kuwa nchi yake imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo na kupokea wageni wengi hasa katika program ijulikanayo ‘Azur Blue’ iliyoanzishwa na kiongozi wa nchi hiyo Mfalme Momamed VI.

Hivyo, alieleza kuwa nchi yake itakuza uhusiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa nchini mwake kuna miundombinu mingi ya kuimarisha sekta hiyo vikiwemo vyuo vya mafunzo ya kitalii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.