Habari za Punde

TMDA YATOA MAFUNZO KWA WAKAGUZI

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

PAMOJA na udhibiti katika vituo vya forodha na masoko kuimarishwa katika mkoa wa Tanga bado kuna changamoto ya kuwepo kwa dawa ambazo hazijasajiliwa ikiwa ni pamoja na baadhi ya maduka vibali na wataalam wenye sifa.

Akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wakaguzi wa dawa, mratibu wa ofisi za kanda makao makuu ya mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA) Henry Ilunde alisema kuwa hali hiyo inapelekea kufanyika kwa ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria.

Ilunda alieleza kwamba mamlaka inahitaji wakaguzi wenye weledi katika kutambua dawa, vifaa tiba na vitendanishi visivyofaa kwa matumizi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha, kuwezesha, kukuza viwanda vya dawa nchini.

"Pamoja na changamoto mbalimbali za kudhibiti napenda kuwafahamisha kuwa TMDA imepata mafanikio makubwa yaliyoifanya kutambuliwa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2018 kama taasisi kiongozi katika Afrika kwa udhibiti wa dawa" alithibitisha.

Aidha alieleza kwamba katika kukabiliana na changamoto zilizopo, mamlaka imetoa mafunzo hayo kwa kuzingatia masuala muhimu kwa wakaguzi ikiwa ni pamoja na kuwakumbusha juu ya maadili na taratibu za kazi katika kutimiza majukumu yao.

Alifafanua kuwa wakaguzi hao pia wamepewa uelewa juu ya sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya TMDA ambayo itawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua stahiki pale inapohitajika.

"Mamlaka itawapa wakaguzi elimu ya jinsi ya kubaini dawa na vifaa tiba bandia, duni na visivyosajiliwa katika soko, uelewa wa mwongozo wa usambazaji bora wa dawa pamoja na uelewa wa kanuni za udhibiti wa matangazo ya biashara za dawa na vifaa tiba" aliongeza.

Hata hivyo Ilunde alieleza kwamba mnamo julai 1, 2019 serikali kupitia sheria ya fedha ya mwaka 2019 ilihamisha jukumu la udhibiti wa chakula na vipodozi na kuhamishia kwenye Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na kuacha TMDA kubaki na udhibiti wa dawa, vifaa tiba ma vitendanishi pekee.

"Ikumbukwe kwamba ubora, usalama na ufanisi wa dawa na vifaa tiba ni jambo muhimu katika kuinua na kuboresha afya ya jamii na kuongeza kuwa hadi sasa zaidi ya asilimia 80 ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi vinavyotumika nchini vinatoka nje ya nchi" alisema.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.