Habari za Punde

Ufungaji wa Maonyesho ya Wajasiriamali wadogo wadogo Kariakoo

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Juma Hassan Reli akizungumza na watendaji wa Zssf na wajasiriamali katika ufungaji  wa maonyesho ya Wajasiramali yaliofanyika kiwanja cha kufuruhashia watoto Kariakoo
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Sabra Issa Machano akizugumza machache na kumkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza na watendaji na wajasiriamali katika ufungaji wa maonyesho ya wajasiriamali  huko Kariakoo Zanzibar.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF Sabra Issa Machano akizugumza machache na kumkaribisha Mgeni rasmi kuzungumza na watendaji na wajasiriamali katika ufungaji wa maonyesho ya wajasiriamali  huko Kariakoo Zanzibar.

Mkurugenzi  Mwendeshaji wa ZSSF Sabra Issa Machano akimkabidhi cheti  Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Juma Hassan Reli katika hafla ya ufungaji  wa maonyesho ya Wajasiramali yaliofanyika kiwanja cha kufuruhashia watoto Kariakoo.
Picha na Fauzia Mussa - Maelezo Zanzibar.

Na Fauzia Mussa,     Maelezo Zanzibar       20/12/2020.

Wajasiriamali wametakiwa kutengeneza bidhaa zenye kiwango na kuzitumia fursa za maonesho ya kibiashara kutangaza biashara zao na kujipatia kipato ili kupunguza tatizo la ajira nchini.

Akizungumza katika ufungaji wa tamasha la tatu la maonesho ya wajasiriamali katika kiwanja cha kufurahishia watoto Kariakoo Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Juma Hassan Reli amesema kuzitumia fursa za maonesho ya kibiashara kutawasaidia wajasiriamali kujitangaza na kuweza kujipatia wateja kutoka sehemu mbalimbali.

Amesema Maonesho ya biashara ni fursa muhimu kwa Wajasiriamali ili kuweza kukuza soko la bidhaa zao na kuwapatia nafasi  ya kukutana na wafanyabiashara wenzao kubadilishana uzowefu ambao utaendeleza sekta ya biashara nchini.

“Ni vyema kuacha kufanya biashara kwa mazoea ningewaomba wajasiriamali wazitumie fursa za mafunzo ili kupata taaluma na ujuzi wa kufanya biashara  kisasa ili kuendana na mabadiliko ya sayansi teknolojia” alisema katibu mkuu.

Alifafanua kuwa elimu ya ujasiriamali na mafunzo ya biashara ni muhimu kwa mjasiriamali ambae ana malengo ya kuinua biashara zake na kupiga hatua ya kimaendeleo

Amesema hivi sasa wafanyabiashara wengi wanatumia teknolojia ya mawasiliano hasa kupitia mitandao ya kijamii ambayo hutumiwa nawatu wengi katika kuzitangaza biashara zao ili kukuza soko la bidhaa hizo.

Aidha Katibu huyo ameupongeza Mfuko wa Hifadhi  ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kwa kuandaa tamasha hilo ambalo  linaenda sambamba na   azma ya Serikali ya awamu ya nane ya kuwanyanyua wafanyabiashara wadodgowadogo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwezeshaji Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) Sabra Issa Machano ameongeza muda wa maonesho hayo hadi tarehe 26 Disemba 2020 ikiwa ni kutekeleza maombi ya wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo ya kutaka kuongezewa muda.

“Kwa uwezo nilionao ninayaongeza muda  maonesho haya mpaka tarehe 26 mwezi huu na watu wataendelea kuingia bure katika viwanja hivi hadi tarehe niliyoisema” alisema Mkurugenzi.

Nao wajasiriamali walioshiriki katika Tamasha hilo wameushukuru uongozi wa ZSSF kwa kuwaongezea muda na kuwaomba kufanyika kwa tamasha hilo zaidi ya mara tatu kwa mwaka.  

Tamasha hilo la tatu la maonesho ya wajasiriamali limedhaminiwa na Mashirika mbali mbali ikiwemo   CRDB, NMB, NHIF, TPB pamoja na Vigor Group of Company.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.