Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais ashiriki maziko ya Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Marehemu Mzee Makame Ussi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla wa Pili kutoka Kushoto akifariji Familia ya Mkurugenzi wa Zamani wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Mzee Makame Ussi Ali aliyefariki dunia na kuzikwa kijiji kwao Mbuyuni Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja.
 Mwanazuoni Maarufu Nchini Sheikh Khamis Abdulhamid akiongoza sala ya Maiti wakati wakimsalia amarehemu Mzee Makame Ussi Kijiji kwao Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akitabaruk kumimina udongo ndani ya Kaburi la Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar Marehemu Mzee Makame Ussi.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Mkurugenzi Mstaafu wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar  Mzee Makame Ussi Ali aliyefariki Dunia baada ya kuugua kwa kipindi kirefu amezikwa Kijiji kwake katika Kitongoji cha Kibuyuni Kijiji cha Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mzee Makame Ussi Ali aliyefariki Nyumbani Kwake Mtaa wa Shauri Moyo Mjini Zanzibar alikuwa akisumbuliwa na Maradhi ya Kisukari yaliyoambatana na udhaifu wa Afya yake kutokana pia na umri mrefu aliokuwa nao.

Mamia ya Wananchi, Jamaa, marafiki pamoja na wana Familia wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliyembatana na Viongozi tofauti wa Serikali na Vyama vya Kisiasa walishiriki mazishi hayo yaliyofanyika mapema asubuhi.

Mzee Makame Ussi Ali alipata elimu ya Dunia  sambamba na ile ya Dini kama ada ya Watoto wa Mwambao iliyomuwezesha baadae kuingia katika tanuri la ajira na kushika nyadhifa mbali mbali za Utendaji na Uongozi katika Taasisi za Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akitoa salamu za rambi rambi na mkono wa pole akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Ali Mwinyi kwa wana familia ya Marehemu Mzee Makame Ussi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema Serikali inaungana na wafika hao katika Msiba huo mzito na kuwataka wawe na moyo wa subra.

Mh. Hemed alisema mtihani wa msiba ulioikumba Familia hiyo ni wa Watu wote wakiwemo wapenzi na wangependa Mzee Makame Ussi waendelee kuwa nae lakini Mwenyezi Muungu amemuhitaji kwa vile anampenda Zaidi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa niaba ya Rais Zanzibar Dr. Hussein Mwinyi amewaomba wana Familia hiyo ya Marehemu watumie msiba huo kuendelea kuungana pamoja ikiwa ni suluhu ya kushirikiana kama zilikuwepo baadhi ya hitilafu zilizokuwa zikiwasumbua miongoni mwao.

Marehemu Mzee Makame Ussi Ali ameacha Kizuka Mmoja na Watoto Sita lakini Mmoja tayari ameshatangulia mbele ya Haki.

Mwenyezi Muungu ashushe rehema zake kwa kumnyooshea safari isiyo na shaka Marehemu Mzee Makame Ussi Ali sisi tukiwa nyuma yake. Amin.

 

 

1 comment:

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.