Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Akutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwahakikishia Wanajumiya ya Wafanyabiashara azma ya Serikali Kuu katika kuwapa ushirikiano kweye majukumu yao.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema fursa nyingi zinazopatikana ndani ya Sekta Binafsi zinaweza kuleta mabadiliko makubwa ya Kiuchumi kwa Taifa endapo zitatuzimwa viruzi na wasimamizi husika.

Akizungumza na Viongozi wa  Bodi ya Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar Afisini kwake Vuga Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Sekta Binafsi ina mchango mkubwa katika Maendeleo ya Taifa na ustawi wa Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini.

Alisema kwa vile Sekta Binafsi inaweza kufanya vyema katika suala zima la Ajira, Serikali Kuu imejikita Zaidi kufanya Kazi kwa ukaribu  na Sekta hiyo kupitia Jumuiya ya  Wafanyabiashara ili kuona malengo ya pande zote mbili katika ongezeko la Mapato yanafanikiwa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Uongozi wa Bodi hiyo kwa mtazamo wake wa kwenda sambamba na kasi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane jambo ambalo limeanza kuleta faraja hasa kitendo chao cha kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa iliyoanza utekelezaji wake Mwaka 2020/2050.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi huo wa Bodi ya Jumiya ya Wafanyabiashara Zanzibar kuangalia mapungufu yaliyomo ndani ya baadhi ya Sheria zenye kuleta utata ili yaweze kufanyiwa marekebisho na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Washirika wa Biashara.

Mheshimiwa Hemed aliwakumbusha Viongozi wa bodi hiyo kuendelea na jukumu lao katika utoaji wa Elimu juu ya umuhimu  wa Wafanyabiashara[WU1]  kulipa kodi jambo ambalo halina mjadala kwa vile ni wajibu wao kufanya hivyo.

Alisema wapo baadhi ya Wafanyabiashara wenye tabia ya kupinda sheria zilizowekwa na badala yake kuendeleza dharau zinazojaa kiburi kinachopelekea wakati mwengine kutumia kisingizio cha majina ya Viongozi ambao hawaelewi kama wanawachafulia Heshima yao.

“ Baadhi ya Wafanyabiashara wanawachafulia viongozi na matokeo yake kusambaa mitandaoni kitendo ambacho Bodi ya Jumuiya ya Wafanyabiashara ina dhima ya kutoa Taaluma kwa Wafanyabiashara ili haki ya kulipa kodi ifanyike kwa vile haina mjadala”. Alisema Mh. Hemed.

Akizungumzia suala la Wataalamu Wazawa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema azma ya Serikali Kuu iko pale pale katika kuwatumia Wataalamu wake kwenye miradi mbali mbali ya Kiuchumi na Ustawi wa Jamii.

Alisema tabia ya kuwadharau Wataalamu Wazalendo mbali ya kuwavunja moyo lakini pia inashindikana kuzitumia Rasimlali zilizopo ikiwemo Taaluma waliyopatiwa Wataalamu hao Wazawa inayotokana na nguvu kubwa iliyotolewa na Serikali yenyewe.

Mapema Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Kitaifa ya Wafanyabiashara Zanzibar Bwana Ali Amour alisema Sekta binafsi tayari imeshaweka mkazo wa kuona Malengo yaliyokuwemo ndani yaDira ya Taifa ya Mwaka 2020/2050 yanafikiwa.

Bwana Ali Amour alisema  katika kuunga mkono hatua hiyo muhimu kwa Maendeleo na Uchumi wa Taifa  Bodi imeamuwa kubadilisha Mpango Kazi wake wa Miaka Mitatu na kusogeza mbele Miaka Mitano ili kwenda sambamba na kasi ya Serikali Kuu iliyopo hivi sasa.

Alisenma nguvu kubwa zitalenga katika uhamasishaji wa ulipaji wa Kodi halai ambapo Serikali itawajibika kuendelea kujenga mazingira bora katika kuwapatia Taaluma Watendaji na wasimamizi wa Taasisi zake ili waendelee kusimamia majukumu yao kwa uadilifu na Uzalendo mkubwa.

Nao baadhi ya Wajumbe wa Bodi hiyo walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Ajira Laki Tatu zilizoainishwa ndani ya Ahadi ya Serikali zinaweza kupatikana kama kutaandaliwa mazingira rafiki kwa kushirikisha Sekta zote zile za Serikali na Sekta Binafsi.

Walisema ushirikishwaji wa Serikali za Mitaa katika maandalizi ya uanzishwaji wa Miradi ya Uwekezaji karibu na maeneo ya Wananchi kwa kuwahamasisha Wafanyabiashara kutumia fursa hizo kunaweza kuwa miongoni mwa njia za kuongeza nafasi ya ajira Nchini.

Wajumbe wa Bodi hiyo walibainisha wazi kwamba maeneo mengine ya kilimo yaliyopo katika Vijiji vya Kibuteni, Nganani na Mtule endapo yatajengewa mazingira bora ya miudombinu ya Umeme na Bara bara hata zile za Kifusi yanaweza pia kuwa chanzo cha fursa hizo za ajira.

Walisema upo ushahidi ulioanza kubainisha wazi kwamba maeneo hayo yameanza kuwa Mkombozi kwa ajira za Vijana walio wengi unaokwenda sambamba na upatikanaji wa bidhaa za Matunda zinazoweza kutosheleza mahitaji hasa kwa Mahoteli yaliyopo Zanzibar.

Walishauri kuimarishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo kilichopo Kizimbani ili kiwe na uwezo kamili wa vifaa vitakavyosaidia kutoa Taaluma kwa Wakulima hasa suala zima la Utafiti wa Udongo unaohitaji matumizi sahihi ili kujua Kilimo gani kinachopaswa kuendelezwa katika maeneo mbali mbali Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.