Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Amekutana na Uongozi wa Jumuiya ya Wazee Wastaaf Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akimsikiliza Katibu wa Jumiya ya Wastaafu Zanzibar Bi.Salama Kombo Ahmed akielezea malengo ya Jumuiya yao katika kusimamia mazingira ya Wazee waliostaafu katika Utumishi wa Umma, walipofika Ofisi kwa mazungumzo  
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Viongozi wa Jumuiya ya Wazee Wastaafu Zanzibar Afisini kwake Vuga.
 

Na.Othman Khamis OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alikutana na Uongozi wa Jumuiya Wazee Wastaafu Zanzibar ili kubadilishana mawazo  mazungumzo yaliyofanyika Afisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Mh. Hemed alisema Serikali itaendelea kuwaheshimu Wazee wote Nchini kwa kuwapatia huduma stahiki ikitimiza wajibu wake ili waendelee kupata utulivu wa maisha yao  huku ikizingatia kuwa mchango wao ndio uliosababisha Taifa hili kufikia hatua kubwa ya maendeleo.

Mheshimiwa Hemed alisema Serikali inaelewa changamoto na matatizo mengi yanayowakumba Wazee katika maisha yao ya kawaida na ndio maana hulazimika kufanya utafiti wa kutosha unaosaidia kupata muelekeo wa kuwajengea mazingira rafiki.

Alisema katika hatua ya kuyakidhi mahitaji yao ya lazima Wazee , Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wote imekuwa na mfumo wa kuangalia mazingira ya hali ya uchumi inavyozunguuka na pale inaporuhusu haioni tatizo nguvu hizo kuzielekeza kwa Wazee hao waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa wakati wa utumishi wao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akitoa ushauri kwa Viongozi hao wa Jumuiya Wastaafu alisema ipo haja ya kuendelea kutoa Elimu kwa Watumishi wanaokaribia kustaafu ili pale watakapofikia muda waendelee na maisha yao bila ya wasi wasi wowote.

Mheshimiwa Hemed alisema Watumishi wengi wanapopata barua ya kumaliza muda wao wa Utumishi huchanganyikiwa huku wakijisahau kwamba wapo Vijana wengi waliomaliza masomo yao ambao wanahitaji kuziba nafasi zao  kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma Serikalini.

Mapema Katibu wa Jumiya ya Wastaafu Zanzibar Bibi Salama Kombo Ahmed alisema Wazee wengi Nchini wamefuharia uwepo wa Sheria iliyowashirikisha moja kwa moja wazee wenyewe ingawa bado haijawa na Kanuni zake.

Bibi Salama alisema Jumuiya ya Wastaafu Zanzibar iliyoasisiwa mnamo Mwaka 2001 pamoja na mambo mengine inaendesha mradi wa kuwaelimisha Wazee kupitia Mabaraza yao ya shehia Unguja na Pemba ili kutambua kwamba Miaka 60 ya ustaafu sio mwisho wa Maisha yao.

Katibu wa Jumuiya hiyo ya Wastaafu Zanzibar kwa niaba ya wanajumuiya wameishukuru Serikali Kuu kwa uamuzi wake wa kuendelea kuwapatia Pencheni kila mwezi sambamba na ile ya Shilingi 20,000 kwa Wazee wa Zaidi ya Miaka Sabini.

Hata hivyo Bibi Salama alisema zipo baadhi ya changamoto zinazoendelea kuwasumbua Wazee akizitaja kuwa ni pamoja na ukosefu wa Kitambulisho ili kuwapa uangalizi wa huduma za Afya na Hospitali pamoja na Uwakilishi wa Wazee katika Mabaraza ya Kutunga Sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.