Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Ajumuika na Wanaichi wa Kijiji cha Mpapa Katika Sala ya Ijumaa leo 1-1-2021.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleima Abdulla akisalimiana na Waumini wa Dini ya Kiislamu alipofika katika Kijiji cha Mpapa Wilaya ya Kati kwa ajili ya  kujumuika katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Uzini Sheikh Othman Ali Maulidi kwa niaba ya Waumini wa Kijiji cha Mpapa akitoa shukrani kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Sumeiman baada ya kumaliuzika kwa Ibada ya sala ya Ijumaa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleima Abdulla akiagana na baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Mpapa mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewakumbusha Wazazi na Walezi kuendelea kuwajibika katika malezi ya Watoto wao ili kuwaepusha na maangamizi ya mmong’oko wa Maadili unaoendelea kuwaathiri Watoto wengi katika mitaa mbali mbali Nchini.

Mheshimiwa Hemed Suleiman ametoa kumbusho hilo wakati akisalimiana na Waumini wa Dini ya Kiislamu wa Kijiji cha Mpapa na Vitongoji vyake ndani ya Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ujumaa katika Msikiti Mkuu wa Kijiji hicho uliopo mkabala wa Nyumba za Maendeleo Mpapa.

Alisema tabia ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia ulimwenguni hasa kupitia mitandao ya Kijamii ikiridhiwa na Wazee kuwaachia Watoto wao wafanye watakavyo litarejea kuwa dhima kwao na vyema wakajitathmini kwamba wao ndio watakaobeba jukumu hilo.

Mheshimiwa Hemed aliwaeleza Waumini hao kwamba zipo tabia za baadhi ya Watoto ndani ya Mitaa hazipendezi hasa uvaaji wao wa Nguo na huku wakishuhudiwa na Jamii Wakiwemo pia Wazazi wao lakini inashangaza kuona mfumo huo wa maisha unaonekana kama ni maendeleo ya kawaida.

Akizungumzia ujenzi wa Nchi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uchaguzi Mkuu Nchini tayari umeshamalizika takriban Miezi Miwili sasa iliyopita na liliopo mbele ya Wananchi kwa wakati huu ni kuchaka kazi kwa lengo la kujipatia riziki ya halali na kulisaidia Taifa Kimapato.

Alisema wajibu wa kushirikiana baina ya Wananchi na Viongozi katika melekeo wa Maendeleo ni dhima inayomuwajibikia kila Mwananchi kuitekeleza vilivyo bila ya kujali utofauti wao iwe  wa Kisiasa, Imani za Dini na hata maeneo wanayotoka.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwaeleza Wananchi kwamba Serikali Kuu inaelewa changamoto zinazowakibili Wananchi katika maeneo mbali mbali Nchini na kwa kulitambua hilo ndio maana ikajikita katika kupambana na rushwa, Ubadhirifu na Uzembe  ili rasilmali ya Taifa iweze kuzishughulikia changamoto hizo.

Alisema Taifa limeibiwa sana na katika njia ya kuirejeshea Heshima na Hadhi yake Serikali Kuu italazimika kuchukuwa hatua za kinidhamu dhidi ya Watu wote waliohusika na ubadhirifu huo ambapo pia itakuwa makini katika hilo bila ya kumuonea yule asiyehusika.

Aliwataka Wananchi kuzingatia umuhimu wa kudumisha Amani, Upendo, Ushirikiano na Mshikamano miongoni mwao ili ile kiu ya Serikali katika kuwahudumia Wananchi wake iende kwa kasi mno.

Alitahadharisha kwamba wapo Watu katika baadhi ya Mataifa Ulimwenguni waliojaribu kuichezea Amani kwa utashi wao binafsi na matokeo yake kwa sasa wameingia kwenye majanga yaliyopelekea hata kuzuka kwa vurugu za wenyewe kwa wenyewe na kusababisha kukatisha maisha ya baadhi ya Watu.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Waumini wa Dini ya Kikslamu wa Kijiji cha Mpapa Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jimbo la Uzini Sheikh Othman Ali Maulid  alisema Wananchi hao wanaendelea kuipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane kwa juhudi ilizoanza kuchukuwa za kuwasogezea Maendeleo Wananchi wake.

Sheikh Maulid alitolea mfano Wananchi wa Jimbo hilo walioanza kupata huduma za msingi baada ya Viongozi wa Jimbo hilo kuanza kuzipatia ufumbuzi baadhi ya changamoto mbali mbali zinazowasumbuwa Wananchi hao.

Mapema akitoa Hotuba ya Sala ya Ijumaa Imam wa Sikiti huo wa Ijumaa wa Mpapa Sheikh Miraji Msoma alikumbusha umuhimu wa Waumini kupenda kufanya kazi kwa vile hiyo ni miongoni mwa Ibada inayowawajibikia kuitekeleza katika maisha yao ya kawaida.

Imam Miraji alisema kitendo cha kufanya Kazi ambacho kilikuwa kikisisitizwa na Viongozi mbali mbali wa Dini waliopita humjengea Heshima kubwa Muumini katika Jamii iliyomzunguuka kwa vile huendelea kupata riziki ya halali iliyoelezwa hata katika Maandiko na Vitabu vya Dini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.