Habari za Punde

Ufungaji wa Tamasha la saba la Biashara, Serikali kushirikiana na wafanya biashara

 Issa mzee     Maelezo 18/01/2021

 Kaimu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mh Mudrik Ramadhan Soraga amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wafanya bishara  ili  kufanikisha mikakati na mbinu za biashara kwa lengo la kuendeleza maendeleo  ya biashara  hapa nchini.

Akizungumza katika ufungaji wa Tamasha la saba la biashara lilifonyika katika viwanja vya Maisara Mjini Unguja amesema uwepo wa matamasha ya biashara nchini unawawezesha wafanya biashara wa ndani na nje ya Zanzibar kuweza kubadilishana mbinu za biashara na kukuza soko la bidhaa hasa kwa wafanya biashara wadogo ambao wanahitaji kukuza biashara zao.

Alisema kuwa Wizara ya Bishara na Maendeleo ya Viwanda itajitahidi kufanya kila linawozekana ili kuhakikisha tamasha hilo linaendelea kufanyika kila mwaka na kutoa  fursa mbalimbali za biashara ndani na nje ya Zanzibar ikiwemo Masoko ili kuwawezesha wafanya biashara kukuza mitaji  yao na hatimae kukuza uchumi wa Zanzibar.

“Tamasha hili limeleta faida kubwa limetoa fursa nyingi kwa wafanya biashara wetu na wa nje ya Zanzibar hasa wafanyabishara wadogo ambao wameweza kujitangaza kibiashara na kuweza kupeana mbinu mbalimbali za biashara pamoja na kubadilishana uzoefu na limewawezesha wananchi wetu kupata bidhaa mbambali kwa bei nafuu.” Alisema Waziri

Alieleza kuwa Tamasha hilo limeweka historia nzuri kwa wafanya bishara kutokana na mauzo kuwa juu pamoja na wafanya biashara kuwa wengi  ambapo zaidi ya wajasiriamali 200 wameweza kushiriki katika Tamasha hilo na kuweza kuuza bidhaa zao kwa kiwango kikubwa.

Aidha Waziri huyo aliwataka wafanya biashara kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali pamoja na  kuzisajili biashara zao ili ziweze kutambulika na kuwa rasmi hatimae kuweza kuondoa changamoto za biashara na kuiwezesha Serikali  kukusanya kodi kwa urahisi  kwa maendeleo ya nchi.

Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mh Juma Reli amesema malengo ya Tamasha hilo yameweza kufanikiwa kwa asilimi kubwa kutokana na soko na mauzo ya bidhaa kuwa juu kwa asilimia kubwa na kupelekea baadhi ya wafanya biashara kuuza bidha zote na kupata faida kubwa.

Alisema kuwa Wizara bado inaendelea kubuni mbinu na mikakati mbalimbali ambayo itazidi kuboresha Tamasha hilo ikiwemo kuanzisha mashindano ya bidhaa, mafunzo ya ubunifu na mbinu za biashara ili kuzidisha ubora wa bidhaa na kulifanya Tamasha hilo lizidi kuwa bora na kuleta tija kwa wafanya biashara,Serikali na wananchi kwa ujumla.

“ Mara hii wafanya biashara wengi wameshiriki katika Tamasha hili hapa Maisara zaidi ya wafanya biashara 360 wameweza kushiriki katika tamasha hili na  hii ni  kutokana na kuwepo kwa huduma zinazohitajika pamoja na mwitikio mzuri wa wananchi na tunatarajia mwakani watazidi idadi hii,” alisema Katibu Mkuu.

Aidha Katibu Mkuu huyo alisema Tamasha hilo linatarajiwa kufanywa mara mbili kwa mwaka  na  kutaka lifanyike katika  eneo la kudumu  huko Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” nje kidogo ya Mjini wa Zanzibar.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Mh Idrissa Kitwana Mustafa amesema Serikali ya Mkoa itahakikisha kuwepo ulinzi na usalama muda wote wa Tamasha hilo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wote waliofanikisha kufanyika Tamasha hilo.

Katika Tamasha hilo Mh Mudrik Ramadhan Soraga alikabidhi vyeti kwa wadhamini na washiriki wa Tamasha hilo ikiwemo benki ya NMB,CRDB,VIGOR,MELISHA,ZCTV na ZICTA samabamba na kuto zawadi kwa mabanda bora ikiwemo ZSSF.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.