Habari za Punde

Mahakama ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Inahitajika Zanzibar - Dk. Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar, kauli mbiu ya mwaka huo ni "Wajibu wa Mahakama na Wadau wa Sheria kwa Kuendana na Kasi ya Awamu ya Nane Kushughulikia Kesi"  

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kwamba Mahakama ya Rushwa na  Uhujumu wa Uchumi inahitajika hapa Zanzibar.

Hayo aliyasema leo katika Maadhimisho ya 10 ya Siku ya Sheria Zanzibar , hafla iliyofanyika katika ukumbi ya Sheikh Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar, ambapo viongozi mbali mbali walihudhuria kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliitakaMahakama ijipange kwa lengo la kuanzisha kwa Mahakama hiyo kutokana na umuhimu wake mkubwa hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kufurahishwa kwake kuona kwamba maelekezo ya kuanzishwa kwa Mahakama  maalum ya udhalilishaji yametekelezwa hatua ambayo itasaidia kuharakisha kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa kesi za aina hiyo ili kuondoa malalamiko yaliopo.

Alieleza kuridhia kuajiriwa kwa mahakimu zaidi kama ilivyoombwa na Jaji Mkuu.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa  nivyema mahakama ikaimarisha juhudi za kutoa elimu ya sheria kwa kuzingatia mahitaji ya kiuchumi na kijamii pamoja na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.

Alisema kuwa kuendeleza utawala bora ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nane kwani imepania kumarisha uwajibikaji, kupiga vita vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na utoaji wa haki kwa wananchi kwa misingi ya usawa.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ucheleweshaji wa kesi katika mahakama una athari nyingi za kiuchumi na kijamii.

Aliongezakuwa hatua hiyo inarefusha kipindi cha huzuni, majonzi na machungu pasi na ulazimu kwa wadai haki.

Kadhalika,alisema kuwa ucheleweshahi wa kesi unasababisha hasara na ongezeko la gharama kwawadai haki zinazohusiana na masuala ya fedha, mali na shughuli nyengine za biashara.

Hivyo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba maswali hayo ni lazima yatimizwe kwa upana zaidi na mahakama na kuwachukulia hatua majaji na mahakimu wazembe na wacheleweshaji wa kesi kwa makusudi ili kukidhi matakwa binafsi.

Alisisitiza kwamba Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka inapaswa kuongeza kasi katika kufuatilia na kuwasilisha ushahidi kila inapohitajika kufanya hivyo.

Pia, alisema kuwa Jeshi la Polisi nalo linatakiwa kushughulikia matukio na malalamiko yanayofikishwa kwao na kuchukua hatua za haraka ili yake yanayopaswa kuchukuliwa hatua za kisheria yachukuliwe na yasibakie katika faili zao.

Aliwataka kuhakikisa kwamba taasisi hizo vile vile zinafanya kazi kwa kuzingatia hali za wanyonge ambapo baadhi ya wakati wanapodai haki zao hukumbana na safari za nenda rudi ambazo zinawagharimu nauli na wakati.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza matumaini yake kwamba Mahkama zitafanyia kazi maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli  ya umuhimu wa matumizi ya Kiswahili katika shughuli za mahakama.

Alisema kuwa hatua hiyo ni kwa ajili ya kuondosha  kiu ya Watanzania ya kutaka lugha yao itumike ipasavyo katika muhimili huo na hatimae kuwawezesha wananchi kuzifahamu vizuri sheria zinazowahusu na zinazoendesha nchi yao.

“Wakati umefika sasa kwa lugha ya Kiswahili kuchukua nafasi yake katika maeneo yote muhimu kwa maendeleo yetu”,alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Pamoja na hayo, aliwataka Mahakimu, Majaji na Wataalamu mbali mbali wa sheria katika muhimili huo wa Mahakama kutoa ushauri kwa Baraza la Wawakilishi pamoja na taasisi za Serikali katika hatua mbali mbali za utungaji sheria zinazohitajika kwa maendeleo ya nchi.

Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alisema kuwa Mahakama imeitikia kwa dhati wito wa serikali kupitia kwa Rais kwa kuanzishwa kwa Mahkama ya maalum Udhalilishaji kama ni njia moja wapo ya kupambana na vitendo hivyo.

Alisema kuwa tayari Mahkama ameshaiunda kisheria na tayari hatua kwa Mwanasheria Mkuu zimeshafanyika kwa ajili ya kuitangaza kwenye gazeti la Serikali na kusisitiza kwamba Mahkama hiyo inaanza kazi leo (tarehe 08 Februari 2021).

Aliongeza kuwa Mahkama hiyo itakuwa maalum, na Waendesha Mashataka Maalum, Wapelezi Maalum wa Udhalilishaji, Mahakimu Maalum wa kusikiliza kesi hizo na kueleza hatua zilizochukuliwa za kuongeza Mahakimu kutokana na uhaba uliopo.

Alisema kuwa dhamira za kuimarisha misingi bora kwa ajili ya uendeshaji wa haraka wa kesi na kueleza ushauri wake wa kuimarishataasisi husika ya Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wawe wenye ujuzi na Jeshi la Polisi kuacha tabia za kuwabambikizia kesi watu wasio na hatia za kesi za aina hiyo.

Pia, aliwataka wananchi kwenda Mahakamani kwenda kutoa ushahidi kwani Zanzibar bila udhalilishaji inawezekana.

Jaji Makungu alimpongeza Rais kwa juhudi zake za kupambana na rushwa na uhujumu wa uchumi na Mahakama inapongeza juhudi hizo ambapo zitafikisha mashauri Mahakamani na kwa wale waliochunguzwa iwapo watapatikana na kesi za kujibu na kesi zikiwa nyingi Mahkama haitosita kuanzisha Mahkama  maalum ya kupambana na Rushwa na Uhujumu wa Uchumi.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa Mahkama hiyo kunawezekana na kumpongeza kwa kuteua Majaji wapya Wawili na kusema kuwa hatua hiyo itapelekea kufikia kwa lengo la kutimiza ahadi yake ya kuwa na Jaji Mkaazi Pemba na kusema kuwa kabla ya mwezi wa Julai kutapelekewa Jaji huko Pemba kwa azma ya kuondoa kukaa muda mrefu kwa kesi kusubiri Majaji kutoka Unguja.

Kwa upande wake  Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuteua Majaji wa Mahkama Kuu ya Zanzibar pamoja na kueleza hatua za Wizara hiyo ya kuanzisha kwa Skuli ya Sheria ambapo masomo yake yanatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Nae Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dk. Mwinyi Talib Haji alisema kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu isemayo “Wajibu wa Mahkama na wadau wa sheria wa kuendana na kazi ya Awamu ya Nane katika kushughulikia kesi” inakusudia kuamsha ari kwa watendaji wa Mahkama na Wadau wake kushughulikia kesi kwa ari kasi ile ile ya Awamu ya Nane

Alisema kuwa Ofisi yake itaendelea kutekeleza kwa uwelezi na umakini mkubwa shughuli za kisheria zitakazoelekezwa kwao au atakazoziagiza Rais kama ilivyoelekezwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Mwanasheria Mkuu huyo alieleza kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imejipanga kutekeleza mambo mambo mbali ikiwa ni pamoja na kutekeleza kesi kwa wakati, miswada na kanuni kuhakikisha inatoka kwa wakati na kwamwe haitokuwa kikwazo cha kupoteza haki.

Aidha, kufanya utafiti za sheria za Zanzibar zinazotumika ama zilizopitwa na wakati zinazoweza kurekebishwa ama kufutwa, jambo jengine alilolitaja ni kupiga vita rushwa na kupinga utuamiji vibaya cheo cha umma, na kueleza jinsi Ofisi hiyo itakavyowajengea uwezo Mawakili wake na wale wa Serikali wanaoshughulikia mikataba.

Aliahidi kumunga mkono suala zima la uzembe kazini na watasimamia kesi katika mahakama jambo ambalo halitopata nafasi kwani uzembe unachangia kwa kisi kikubwa kupoteza haki za watu kuviza malengo ya Taifa kiuchumi na kijamii.Aidha, Mwanasheria Mkuu huyo alisisitiza haja ya maadili ya kazi na kusimamia haki.

Kwa upande wa  kuimarisha uchumi alisema kuwa Rais Dk. Mwinyi amedhamiria kuimarisha uwekezaji na uchumi wa buluu na pia kupanua wigo huo mipango ya kibiashara itaimarika na kupelekea migogoro ya kibiashara kuwepo, hivyo iwapo itaibuka alisema kuwa Mahakama ya biashara itumike rasmi katika kutatua migogoro hiyo.

Nae Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Muumin Khamis Kombo alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imekuwa ikipambana na rushwa ubadhilifu wa mali ya umma na udhalilishaji, hivyo wananchi wamejenga imani kubwa kwa Serikali.

Hatua hiyo ni ujasiri na umahiri wa utekelezaji wa wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na kusisitiza kwamba uhalifu wa kiuchumi ni uhalifu mkubwa.

Aliongeza kuwa mahakama inawajibika katika kutekeleza kazi zake ili kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Nane katika kusimamia weledi na maadili katika utoaji wa haki.

Alisema kuwa suala la udhalilishaji ni kubwa hivyo, imefika wakati wa kutambua kwamba udhalilishaji unahitaji taaluma ya kisayansi ili kubaini vyanzo vya uhalifu huo.

Akitoa salamu za Mawakili wa Zanzibar, Rais wa Chama cha Mawakili Slim Said Abdullah alisema kuwa Mamlaka yenye kauli ya Mwisho katika Jamhuri ya Muungano ni Mahkama hivyo, Katiba inataka jukumu la kutoa haki litekeleze ipasavyo  na Mahkama hasa ikizingatiwa kwamba taasisi hiyo ina wadau wengi.

Alitoa ushauri wa kuwa na utaratibu wa kuwawekea Majaji Malengo hatua ambayo imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa jambo ambalo tayari kwa upande wa Tanzania Bara limeshaanza kufanyika.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.