Habari za Punde

Mbunge wa jimbo la Handeni mjini Reuben Kwagilwa atekeleza ilani ya Ccm, ahamasisha wananchi kuanza ujenzi wa shule ya msingi, atoa mabati 119

Na Hamida Kamchalla, HANDENI.

WATUMISHI wanaohitajika kuwafikia wananchi kulingana na kazi zao katika halmashauri ya mji wa Handeni wametakiwa kwenda kwenye maeneo ya kazi na kuacha mara moja tabia ya kukaa ofisini kiwasubiria wananchi kupeleka matatizo yao kwa visingizio visivyo na mashiko.

Maofisa walionyooshewa kidola ni wa idara za kilimo, elimu ardhi ambao wamekuwa wakiishia kukaa ofisini kwa madai ya kutokuwa na usafiri jambo ambalo sio la kweli wakati wananchi wana majitaji katika maeneo husika ambayo walitakiwa kufika kila wakati kwa ukaguzi hata kama hakuna kazi kwa siku husika.

Mwenyekiti wa Ccm wilaya ya Handeni Athumani Malunda alibainisha hayo kwenye msalagambo wa uchimbaji wa msingi katika eneo la Lengomi, mtaa wa Kwedigongo kata ya Mabanda ambako kunahitajika ujenzi wa shule ya msingi na kusema kuwa maofisa wanashindwa kufanya kazi zao zinawataka kutoka kwenda kutembelea maeneo wanayostahili na kuishia kukaa ofisini bila kazi.

"Ofisa kilimo, ofisa elimu na ofisa ardhi muache tabia hii ya kukaa ofisini na kisinzia wakati wananchi kule wana matatizo yanayowahusu nyinyi, mwananchi hawezi kubeba shamba akakuletea ofisini upime, wala hawezi kubeba mifugo kwenye zizi akakuletea, ofisini hakuna shule nendeni kwa wananchi mkatatue matatizo yao" alisema Malunda.

"Kuna wakati mwengine mtu anatafuta sababu ambayo haina hata mashiko, mtumishi ukimuuliza kwa nini hajaenda saiti anakujibu hana gari au mafuta, hizi gari halmashauri zimekwenda wapi, muda mwingine muwe wazi tu, mimi niko tayari kuwapeni gari yangu na ikibidi hata mafuta nitawawekeeni mafuta na kama haitoshi hata posho za kujikimu nitawapa ili mradi muwafikie wananchi mkawahudumie" aliongeza.

Naye Mbunge wa jimbo la Handeni mjini Reuben Kwagilwa alibainisha kwamba wameamua kujenga shule eneo hilo linalozunguukwa na wafugaji kwa kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa shule hiyo kutokana na wanafunzi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu kwenda shuleni huku akiwataka wananchi hao kujitolea kikamilifu ili kuharakisha ujenzi huo na watoto.

"Ndugu zangu tunaleta ujenzi wa shule hapa ili watoto wa wafugaji wasomee hapa karibu na kuacha kutembea umbali mrefu kufuata elimu, wataalam wetu watupimie maeneo yanayofaa kwa ujenzi ili tuanze mara moja watu wasiondoke bila kufanya kazi, tushirikiane kufanikisha ujenzi huu kwa haraka watoto wetu wanze kusoma" alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa ujenzi huo Kimuondari Lendawo ambaye pia ni kiongozi wa wazee wa kimila katika eneo hilo alisema kuanza kwa ujenzi huo kutawapa ari ya kumalizia shule hiyo ifikapo mwezi wa nne ili kuwapa watoto wao unafuu wa kutembea umbali mrefu na kiongeza kuwa utaleta manufaa kwa wananchi wa eneo hilo kupata fursa za kibiashara pindi shule itakapokamilika.

Lendawo alibainisha kwamba kilio cha ujenzi wa shule hiyo kina miaka mitano lakini viongozi walikiwa wakiishia kuangalia maeneo na kuondoka bila utekelezaji  na kuongeza kuwa kupitia Mbunge aliyeko sasa madarakani jitihada zinaonekana na leo kazi imeanza rasmi na kuahidi kuusimamia ujenzi huo umalizike kwa muda muafaka waliopanga.

"Furaha yangu ni kuona shule hii inajengwa na kuisha maana tumeshakaa sana kuhusu ujenzi huu sasa yapata miaka mitano, watoto wetu wanateseka kutembea kilomita 6 kwenda tu shule, hapa sasa tumepata kiongozi anayesikiliza na kutekeleza matatizo ya wananchi, kila siku tunaimba wimbo mmoja lakini sasa tunaanza ujenzi rasmi, ni furaha kwetu kwasababu watoto watasoma hapa karibu" alisema.

"Tumehangaikia ujenzi wa shule mpaka ikafikia mahali tukajikusanya kaya zilatazo 250 tukaanza kujichangisha wenyewe kila mmoja atoe shilinhi elfu 50 ili tupate shule hapa lakini hatukuwa na kiongozi wa kutusaidia kufikia malengo yetu lakini tukarudishia pesa zile, sasa tumepata kiongozi wa utekelezaji na hatutamuangusha katika ujenzi huu, kwakuwa ujenzi ni mgumu lakini tutahakikisha mpaka mwezi wa nne tumemaliza ili watoto wetu wasome" aliongeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.