Habari za Punde

Serikali Itatowa Ushirikiano Wake na Kuhakikisha Rasilimali Fedha Inatengwa Kwa Ajili ya Mpango Huo wa MKURABITA. -Dk. Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA ) walipofika Ikulu kwa mazungumzo na kujitambulisha leo, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi  ameuahidi uongozi wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwamba Serikali itaendelea kuziunga mkono juhudi zao kwani wanachokifanya ni kutekeleza ahadi zilizotolewa kwa wananchi wakati wa Kampeni.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokuwa akizungumza na Kamati ya uongozi wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), mara baada ya kutoa taarifa ya utekelezaji wake wa kazi kuanzia Novemba 2004 hadi Januari 2021.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa kwa vile jambo hilo ni miongoni mwa vipaumbele vilivyowekwa na Serikali, aliahidi kwamba Serikali itatoa ushirikiano wake na kuhakikisha rasilimali fedha inatengwa kwa ajili ya Mpango huo wa (MKURABITA).

Alisema kwamba kuhusu rasilimali watu na teknolojia ni vitu muhimu sana hivyo, Serikali itahakikisha bajeti inayotengwa inaendana na kuwepo kwa watu wanaoweza kuifanya kazi hiyo pamoja na mifumo ya kisasa ya kiteknolojia ili kazi ifanyike vyema zaidi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi zake kwa kazi nzuri zinazofanywa na Mpango huo wa (MKURABITA)  na kusisitiza kwamba kazi hiyo ni nzuri na itasaidia kutokana na kuendana na vipaumbele vya Serikali vya kuwasaidia wanyonge.

Rais Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa Bajeti iliyowekwa na kutoa shukurani kwa kazi kubwa zinazofanywa na (MKURABITA)  ikiwa ni pamoja na kutumia TZS Milioni 440.1 kwa Zanzibar ambazo zimewezesha kufanya mambo kadhaa ikiwemo kutatua migogoro ya ardhi ambayo amekuwa akiizungumzia mara kadhaa.

Alisema kuwa mpango huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kufufua mtaji mfu sambamba na kuweka sawa masuala ya hati miliki pamoja na kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya ardhi.

Aliongeza kwamba vituo jumuishi ndio mfumo mzuri wa biashara za kisasa ambapo (MKURABITA) imekuja na mfumo wake ambapo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo inao mfumo kama huo wa kuwa na kituo kimoja katika Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) ambacho kitarahisisha kutoa huduma kwa wawekezaji.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mbali ya kuwafikiria wafanyabiashara na wawekezaji  wakubwa ni vyema wakafikiriwa na wale wadogo, na kuwapongeza kwa kuanzisha vituo hivyo pamoja na mipango yao ya kufikisha vituo hivyo kwa kila Wilaya hapa Zanzibar.

Aidha,Dk. Mwinyi aliunga mkono maelezo ya taarifa hiyo ya kuendeleza mafunzo kwa wahusika, vifaa vitaendelea kuhitajika maana kila mpango ukikua vifaa vitahitajika, kusajili wajasiriamali 1500, kurasimisha viwanja 5,713 na kuwaunganisha wafanyabiashara na taasisi za fedha hizo zote ni ahadi zake katika uchaguzi.

Alisisitiza kwamba wafanyabiashara wadogo wadogo aliwaahidi kwamba hawatoachwa kwani walikuwa wakilalamikia mfumo ambao hauko rafiki kwao, hivyo Vituo Jumuishi vitajibu mengi katika  yote hayo pamoja na kuondosha urasimu na kuwaunganisha na Benki.

Sambamba na hayo, alipokea salamu za pongezi zilizotolewa kwake pamoja na kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli kwa ushindi wa kishindo walioupata pamoja na juhudi kubwa wanazozichukua za kuimarisha uchumi.  

Mapema Makamo Mwenyekiti wa Bodi ya (MKURABITA) Immaculata Mwanja Senje alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa ushindi mkubwa alioupata ambao Wazanzibari walionesha imani kwake na wao wanathibitisha kwa vitendo kutokana na ahadi zake na zile za CCM.

Halikadhalika, kwa niaba ya uongozi huo alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa ushindi alioupata na kueleza kwamba ushirikiano wao utaisaidia Tanzania kufika mbali.

Alieleza kwamba lengo la ziara yao ya siku 4 hapa Zanzibar iliyoanza mnamo Februari 07, 2021 hadi leo Februari 11, ilikuwa ni kuja kuangalia shughuli zinazofanywa na Mpango wa (MKURABITA) hapa Zanzibar na hasa zile zilizopangwa kufanyika katika mwaka huu wa fedha.

Alisema kuwa katika ziara yao hiyo wamepata fursa ya kukutana na wananchi, wamezindua kituo Jumuishi walichokizindua na kugawa hati za matumizi ya ardhi na kufarajika kwa muitikio wa wananchi pamoja na mashirikiano mazuri waliyoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kwamba (MKURABITA) ilianzishwa kwa tamko la Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa mnamo Septemba 30, 2003 na kuanzishwa rasmi mnamo mwaka 2004 ambapo ilianzishwa kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Makamo Mwenyekiti huyo alisema kuwa  kazi ama shughuli zinazotekelezwa na (MKURABITA), kwa sasa ni Urasimishaji Ardhi Vijini, Urasimishaji Ardhi Mijini, Urasimishaji Biashara na Ujengaji uwezo wa wananchi Kiuchumi kwa njia ya mafunzo ya namna ya kutumia haki milki zao kiuchumi.

Alisema kuwa (MKURABITA), imekuwa ikitoa fedha kwa kila bajeti ambapo tokea kuanzishwa kwakwe kwa upande wa Zanzibar Mpango huo umeweza kutoa jumla ya TZS Milioni 440.1 kwa Zanzibar, ambapo fedha hizo zimesaidia kuendesha shughuli hizo.

Alieleza kufarajika na hotuba za Rais Dk. Mwinyi pale anaposema kuwa mionghoni mwa mambo ambayo atayapa kipaumbele ni kutatua migogoro ya ardhi na kazi kubwa inayofanywa na Mpango huo ni hilo hivyo, wamepata faraja kutokana na uongozi wa Kitaifa kutilia mkazo jambo hilo ambapo kwa upande wao itawarahisishia kazi.

Aidha, alisema kuwa katika kurahisisha urasimishaji na uendeleza wa shughuli za biashara (MKURABITA), ilianzisha mfumo wa urasimishaji biashara kwa kutumia Vituo Jumuishi vya Urasimishaji na Uendelezaji wa Biashara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Aliongeza kuwa lengo la vituo hivyo ni kurahisisha na kuharakisha urasimishaji wa biashara kwa kuwezesha wadau wa urasimishaji kutoa huduma za urasimishaji na uendeleza biashara sehemu moja.

Sambamba na hayo, Makamo Mwenyekiti huyo alieleza kuwa hadi kufikia Februari 2021, vituo 12 vya Urasimishaji na Uendelezaji biashara vimeanzishwa katika Halmashauri mbali mbali nchini ambapo kati ya vituo hivyo kimoja kimeanzishwa Wilaya ya Mjini kwa upande wa Zanzibar.

Nae Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said alieleza haja kwa Kamati ya uongozi huo wa (MKURABITA), kuvitumia vyombo vya habari kuyatangaza mafanikio waliyoyapata kwani ni makubwa.

Kwa upande wake Dk. Seraphia Mgembe ambaye ni Mratibu wa Mpango wa (MKURABITA), alieleza kuwa wamefarajika kwa kiasi kikubwa kwa kurahisishiwa kazi zao kutokana na kumuona Rais Dk. Mwinyi akikukutana na wananchi wa chini na kusikiliza changamoto zao huku akitafuta njia za kuzitafutia ufumbuzi.

Dk. Mgembe alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kutambua na kufahamu azma ya Mpango huo ambao umeanza kuwaletea mafanikio makubwa katika shughuli zao za kimaendeleo huku akieleza azma ya (MKURABITA) kuanzisha kituo Jumuishi kisiwani Pemba.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.