Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt.
Faustine Ndugulile akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Bunge
Jijini Dodoma. Kushoto ni Mulembwa Munaku, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo
na kulia ni Prosper Minja, Afisa Habari wa Bunge
Na Faraja Mpina, WMTH, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile ametoa maelekezo kwa Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula
kuitisha kikao cha wataalamu wa mifumo ya TEHAMA siku
ya tarehe 31/03/2021 kitakachoongozwa na wataalamu kutoka katika Wizara hiyo
kwa lengo la kufanya tathmini ya mifumo ya TEHAMA ya kifedha iliyopo nchini.
Akizungumza katika kikao chake na waandishi wa
habari katika ukumbi wa
Bunge jijini Dodoma, Dkt. Ndugulile
amesema kuwa amechukua hatua hiyo kutokana na Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe.
Samia Suluhu Hassan pamoja na ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa
Fedha za Serikali (CAG), Dkt. Charles Kichere
iliyowasilishwa kwake kuonesha kuna changamoto katika mifumo hiyo na Wizara
yake imechukua jambo hilo kwa uzito mkubwa.
“Nimemuelekeza Katibu Mkuu wangu kuchukua hatua
za haraka kwa kuitisha kikao cha wataalamu wa TEHAMA ili kufanya tathmini ya mifumo hiyo, idadi yake,
changamoto za utengenezaji, uendeshaji na uendelezaji wa mifumo hiyo hapa
nchini pamoja na changamoto ya mifumo hiyo kutosomana na kutobadilishana taarifa”,
alieleza Dkt. Ndugulile
Aidha, alisisitiza kikao hicho kuwahusisha
wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora; Ofisi ya Rais - TAMISEMI; Wizara ya Fedha na
Mipango; Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Fedha
za Serikali; Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA); Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL); Kituo cha Kuhifadhi Data cha Taifa (NIDC); Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya
Serikali Mtandao (eGA).
“Natoa wiki moja kwa wataalamu hawa kufanyia
kazi jambo kubwa lililogusiwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la changamoto ya
mifumo hiyo kuruhusu mianya ya upotevu wa mapato na usalama wa mifumo hii na
kutoa mapendekezo ya maboresho ya nini kifanyike ili kuhakikisha mianya hiyo
inazibwa, usalama wa mitandao unakuwepo na kunakuwa na mifumo inayosomana
ambayo haitaruhusu kupoteza mapato ya nchi”, alisisitiza
Dkt. Ndugulile
Aliongeza kuwa Wizara yake itafanyia kazi
mapendekezo hayo ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za kuboresha na yale ambayo
yatahitajika kushughulikiwa na mamlaka ya juu yatachukuliwa na kupelekwa kwa
hatua nyingine zaidi.
“Jukumu kubwa la Wizara hii ni kutoa miongozo, usimamizi wa mifumo ,
uendelezaji na kuhakikisha nchi inakuwa na matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA
na usalama wake, mifumo mingi iliyokuwa inatumiwa na
Serikali ilikuwa inatoka nje ya nchi na fedha nyingi zilitumika kwa uendeshaji
na kulipia leseni lakini kwa sasa zaidi ya asilimia 80 ya mifumo inayotumika
nchini na ndani ya Serikali
imetengenezwa na wataalamu wetu wazalendo”, alisisitiza Dkt. Ndugulile
Alisema kuwa jukumu kubwa alilonalo katika Wizara hiyo ni kuhakikisha inajenga uwezo wa
wataalamu wa ndani ya nchi kuhakikisha mifumo mingi inaweza kutengenezwa hapa
hapa nchini katika ubora unaoendana na
mahitaji ya nchi na usalama dhidi ya udukuzi ambao unaweza kufanyika kwa
kutumia mifumo ya iliyotengenezwa mahali pengine.
“Naomba niwaambieni kuwa TEHAMA ni sehemu ya
siasa, biashara, ni masuala ya kiusalama na sisi kama Wizara tuna jukumu la
kuhakikisha sekta za kiuchumi na fedha zinakuwa na mifumo imara, sekta za
huduma ya kijamii kama vile afya, elimu na maji zinakuwa na mifumo salama na
sekta zinazohusika na mambo ya ulinzi na usalama nazo zinakuwa na mifumo salama
ili hata pale panapokuwa na changamoto kuhakikisha huduma za nchi zinaendelea pasipo
kuathirika”, alimalizia Dkt. Ndugulile.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
No comments:
Post a Comment