Habari za Punde

Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani. Wanawake ni Nguzo Katika Kukuza Uchumi.

Na. JovinaBujulu - MAELEZO

Siku ya Wanawake Duniani husherehekewa kila mwaka ifikapo tarehe 8, Machi, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa unaotolewa na kundi la wanawake duniani katika mchakato wa maendeleo ya nchi huku ukichagiza juhudi kubwa za kutambua ushiriki wao katika nyanja zote za kukuza uchumi.

 Tanzania kama nchi nyingine, nayo inasherehekea siku hii ambapo wanawake hupata fursa ya kuwa na midahalo, semina na mikutano ambayo huwapa nafasi ya kuonesha na kueleza mafanikio yao ikiwa ni pamoja na kuonesha shughuli mbalimbali za ujasiriamali ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi za Afrika zilizoridhia mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambayo inaelezea haki za kichumi kwa kila mtu. Mikataba hiyo ni pamoja na wa Kimataifa wa Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni ya mwaka 1966.

Ibara ya 6 ya Mkataba huo inalinda haki za kiuchumi kama vile haki ya kufanyakazi na haki ya kuchukua hatua nyingine zinazowapa wanawake fursa sawa za kuajiriwa na kujiendeleza kitaaluma na fursa nyingine za kiuchumi.

Serikali imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kujenga uwezo wa wanawake ili waweze kujitegemea na kuweza kufanya maamuzi ya juu

ya maisha yao ikiwa ni pamoja na kutekeleza maamuzi hayo kwa kutumia rasilimali zilizopo, bila kuingiliwa au kubughudhiwa na mtu, taasisi au chombo chochote kwa sababu tu wao ni wanawake.

Kwa kutambua mchango wa wanawake nchini, Serikali ya Awamu ya Tano iliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa inawapatia wanawake asilimia nne ya mapato ya ndani ya Halmashauri hizo ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kuweza kuchangia pato la Taifa.

Tangu kuingia madarakani Serikali ya Awamu yaTano, inayoongozwa na Rais John Magufuli na kutangaza Sera ya viwanda na uchumi wakati, wanawake wamekuwa na muitikio mkubwa sana ambapo matokeo yake yanaonekana kutokana na shughuli mbalimbali wanazozifanya.

Wanawake nchi nzima wameanzisha vikundi vingi vya ujasiriamali ambavyo vinapatiwa mikopo ya Halmashauri hivyo kuwawezesha kuanzisha shughuli mbalimbali ambazo zimeweza kuwainua kutoka katika ngazi ya mtu mmoja mmoja, familia, jamii hadi Taifa. Shughuli zinazofanywa kutokana na mikopo ya vikundi hivyo ni pamoja na ushonaji, utengenezaji batiki, sabuni za maji, kilimo cha bustani, na ufugaji wa sungura,ng’ombe,mbuzi na kuku.

Kwa kutambua mchango wa wanawake katika kukuza uchumi duniani Kitengo cha Masuala ya Wanawake cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kinasema“ Kuwekeza katika kuwawezesha wanawake kiuchumi huelekeza moja kwa moja kwa usawa wa kijinsia, kuuangamiza umaskini na ukuaji jumuishi wa uchumi”.

Katika kipindi cha miaka mitano kuanzia 2015-2020, Serikali ya Tanzania imetoa jumla ya shilingi bilioni 63 ikiwa ni mikopo yenye masharti nafuu ili kuwawezesha kiuchumi wanawake wajasiriamali 938,802. Mikopo hiyo imewajengea ujasiri wanawake, kukuza ujuzi na mbinu za ujasiriamali, kujiunga na mitandao ya masoko na kuchangia pato la Taifa.

Akizungumza katika Kongamano la kiuchumi kwa Wanawake wajasiriamali lililofanyika mkoani Singida mwaka jana,Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Patrick Golwike alisema kwamba Serikali imeanzisha Mwongozo wa kuwahamasisha wanawake kuanzisha na kujiunga na vikundi vya kiuchumi ili kujipatia mikopo na kukuza mitaji yao.

Hivi karibuni Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kiliandaa mkutano kuhusu Wanawake katika uongozi ambapo Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa ATE, Dkt. Aggrey Mlimuka alisema kuwa utafiti unaonesha taasisi zinazoongozwa na wanawake zinamatokeo chanya, ongezeko la uzalishaji na ukuaji wa uchumi.

Naye mjasiriamali wa kutengeneza na kuuza batiki, Alphonsina Masawe kutoka katika kikundi cha Jipe Moyo amesema kuwa kutokana na Serikali kuwawezesha kiuchumi ameweza kujikimu katika kuihudumia familia yake ikiwa ni pamoja na kulipa kodi mbali mbali ikiwemo kodi ya pango katika sehemu anapofanyia biashara yake na kodi ya Serikali.

Akifungua Wiki ya Viwanda ya Wanawake katika Maonesho ya Biashara yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake WafanyaBiashara Tanzania (TWCC), yanayofanyika jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara,  Exaud Kigahe amesema kuwa shughuli zinazofanywa na wanawake zimekuwa zikichangia pato kubwa la Taifa na ukuaji wa uchumi kwa ujumla hapa nchini.

“Kauli mbiu ya maonesho haya “Mwanamke na Uwekezaji wenye Tija kwa Maendeleo Endelevu ya Viwanda”, inaendana na dhima ya maonesho haya pamoja na sera ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambaye amekuwa akihimiza uwepo wa viwanda na tumeshuhudia maendeleo makubwa ya uchumi wa kati na katika mafanikio hayo wanawake wamechangia kwa kiasi kikubwa”, amesema Naibu Waziri Kigahe.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.