Habari za Punde

Wazanzibari Wana Kila Sababu ya Kuungana Pamoja Katika Kuendeleza Amani

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Waumini wa Msikiti wa Mfereji wa wima, baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti huo leo.5-3-2021.
WAUMINI wa Dini ya Kiislam wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na kuwasalimia Wananchi baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti wa  Mabuluu Mfereji wa Wima, Wilaya ya Mjini Unguja
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti wa Mfereji wa wima Wilaya ya Mjini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na kuagana na Waumini wa Dini ya Kiislam wa Msikiti wa Mfereji wa wima Wilaya ya Mjini Unguja, baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika leo 5-3-2021.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyiamewataka wananchi wa Zanzibar kuimarisha amani na umoja kwa lengo la kuiletea nchi maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika Msikiti wa Mabuluu  Mfereji wa Wima, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja,  mara baada ya kujumuika pamoja na Waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa msikitini hapo.

Katika salamu hizo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Wazanzibari wote ni wamoja hivyo, ni vyema wakauendeleza umoja na amani iliyopo sambamba na kuendelea kuwajibika ili kuiletea nchi maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema wananchi wote wa Zanzibar wana kila sababu ya kuungana pamoja katika kuendeleza amani na umoja uliopo pamoja na kuchapa kazi kwa azma ya kuiletea nchi maendeleo..

“Leo katika nchi yetu tuna amani na umoja hayo ni mambo makubwa na baada ya hapo maendeleo yatapatikana tu Inshaalllah kwa sababu sote sasa ni wamoja na kilichobaki watu wafanye kazi na kila mtu awajibike maendeleo yatapatikana tu Inshalla”,alisema Alhaj Dk. Shein.

Aidha, alisema  kuwa hivi sasa Zanzibar imejaa amani na umoja hivyo matumaini makubwa ya kupatikana kwa maendeleo yapo kwani wananchi wote wa Zanzibar ni wamoja na kilichobaki ni kufanya kazi na kuwajibika.

Alhaj Dk. Mwinyi alitoa pongezi kwa wananchi wa Jimbo hilo la Kwahani ambalo kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikuwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa kwa vipindi vitatu kwa miaka 15.

Aidha, katika salamu zake hizo aliwataka wananchi kuendelea kuchapa kazi na kuleta maendeleo makubwa nchini na kuwapongeza na kutoa shukurani kwa uongozi wa msikiti huo kwa kumkaribisha na kusali nao pamoja.

Alhaj Dk. Mwinyi aliwataka waumini wote wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote kwa jumla kumuombea dua kwani ana jukumu kubwa la kuweza kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio na uadilifu sambamba na kutenda haki kwa kila mmoja.

Mapema Sheikh Abdulkarim Said Abdallah  akisoma hotuba ya sala  ya Ijumaa,alieleza haja kwa waumini kuendeleza amani na umoja uliopo nchini na kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuwaweka Wazanzibari kuwa wamoja.

Sheikh Said alisema kuwa nchi yoyote inapotaka kupiga hatua za maendeleo jambo la mwanzo ni kuieneza amani na umoja ili maendeleo yaweze kupatikana.

Alisema kuwa nchi hiyo ikiendeleza amani na umoja maendeleo makubwa yatapatikana ambapo kwa upande wa Zanzibar mafanikio yamepatikana kutokana na viongozi wake kuitangaza amani na umoja.

Alisema kuwa hakuna maendeleo katika nchi ambayo watu wake wamepigana mapande ambapo kwa upanade wa Zanzibar hivi sasa wananchi wamekuwa wamoja kutokana na juhudi za viongozi hivyo ni vyema wananchi wakaishukuru neema hiyo ya umoja.

Katika hotuba yake hiyo, Sheikh Said alisema kuwa nchi imejaa amani na wananchi wamekuwa na mategemeo na matumaini makubwa na matarajio kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani mambo mazuri yoyote hayawezi kuja katika nchi ambayo wananchi wake wamepigana mapande.

Alisema kuwa baraka ya Mwenyezi Mungu ipo kwa watu walioshikamana na kusisitiza kwamba jamii kuwa pamoja katika kila sekta basi nchi yenyewe inajiendesha na mambo yote ya kijamii yanaimarika yakiwemo masuala ya zaka na sadaka.

Sambamba na hayo, Sheikh Said amesema kuwa Rais Dk. Mwinyi ameyafanya mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha Wazanzibari na kumchagua Makamo wa Kwanza wa Rais hivi karibuni ambaye atamsaidia.

“Wewe ni Rais ambaye unatupenda sote....na wewe ni Rais ambaye sote tunakupenda na hatukusifu tu bali tunayasema ni mambo yaliyo moyoni mwetu....sisi tuna Rais na tunaishi katika moyo wake kwani tunajua huyu Rais hataki kuwaongoza raia wengine isipokuwa sisi, na sisi haturidhii kuongozwa na mwengine yeyote isipokuwa yeye...hii Zanzibari itaneemeka kwa uongozi wa kiongozi huyu Dk. Mwinyi”,alisema Sheikh Said.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.