Habari za Punde

Mazrui akabidhiwa Wizara rasmi: Amewataka watendaji kujenga umoja na mashirikiano

 Aliekuwa Kaimu Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Simai Muhammed Said (kushoto) akimkabidhi vitendea kazi Waziri wa Wizara hiyo Ahmed Nassor Mazrui alipomkabidhi Wizara yake, (kulia) Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Omar Dadi Shajak.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar Ahmed Nasor Mazrui akizungumza na watendaji wakuu wa Wizara katika kikao cha makabidhiano ya wizara hiyo hafla iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Baadhi ya watendaji wakuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar wakisikiliza hutuba ya Waziri wao baada ya kukabidhiwa rasmi wizara hiyo.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Ahmed Nasor Mazrui (kulia) na aliekuwa kaimu wa Wizara hiyo ambae ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Muhammed Said wakifurahia kitu baada ya makabidhiano.

Picha na Makame Mshenga.

 Na Ramadhani Ali – Maelezo                  05.03.2021

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Ahmed Nassor Mazrui amewataka wafanyakazi wa Wizara hiyo kujenga umoja na kufanyakazi kwa mashirikiano ili kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya nane ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Amesema Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na kuwapatia wananchi huduma bora hivyo kila mfanyakazi anatakiwa kutekeleza majukumu yake ili kufikia matarajio aliyoweka.

Waziri Mazrui alieleza hayo wakati wa hafla ya kukabidhiwa Ofisi na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohammed Said aliekuwa akikaimu Wizara hiyo chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa .

Amesema Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsi na Watoto ni Wizara muhimu inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wote hivyo mashirikiano ya dhati na umoja kwa watendaji ni jambo la msingi.

Amewataka Wafanyakazi wa Wizara hiyo kila mmoja ahakikishe anatoa huduma bora kwa wananchi bila ya ubaguzi na kuweka mbele uzalendo wakati wanapotoa huduma.

Waziri wa Afya aliwakumbusha wafanyakazi wa Wizara hiyo umuhimu wa kufuata maadili ya kazi ikiwa ni pamoja na kutunza siri na kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa wanapofika kwenye vituo vyao.

Alishauri kila mfanyakazi wa Wizara ya Afya kuwa tayari kwenda na mwendo wa kasi wa awamu iliyopo madarakani ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanazostahiki bila ufumbuzi.

Aliekuwa Kaimu Waziri wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Simai Mohammed Said alikumbusha kuwa baada ya kufanyika ugatuzi, huduma za afya za msingi hivi sasa zimehamishiwa Manispaa na Halmashauri za Wilaya lakini Wizara ya Afya ndio yenye wawajibu wa kupeleka mahitaji muhimu ya dawa kwa lengo la kuimarisha huduma katika vituo hivyo.

Amewashauri wafanyakazi wa Wizara kuwa wabunifu katika kuiletea maendeleo Wizara ya Afya na kuzitafutia ufumbuzi kero zinazowakabili wananchi wa kawaida badala ya kuwa walalamikaji. 

Alisema shauku ya Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi ya kuharakisha maendeleo ya wananchi ni kubwa hivyo ni muhimu kwa wafanyakazi kubadilika na kwenda sambamba na matarajio ya Serikali na wananchi.

Ahmed Nassor Mazuri aliteuliwa kusimamia Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsi na Watoto katika Serikali ya nane ya Umoja wa Kitaifa na aliapishwa jana Ikulu na leo amekabidhiwa rasmi Wizara yake.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.