STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar
11.03.2021
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali
Mwinyi ameeleza haja kwa Wizara ya Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na
Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa azma ya kupeana uzoefu.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu
Jijini Zanzibar wakati alipokutana na Waziri wa Wizara ya Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
Faustine Engelbert Ndugulile pamoja na ujumbe wake waliofika Ikulu kwa ajili ya
kujitambulisha kwa Rais na kuitambulisha Wizara hiyo mpya.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema
kuwa Mashirikiano kwa Wizara hizo mbili yanahitajika hasa ikizingatiwa kwamba
Zanzibar nayo ingependa kwenda kwa kasi
katika sekta hiyo Teknolojia ya Habari hivi sasa.
Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba juhudi za
makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika
kuhakikisha malengo yaliyowekwa katika kuimarisha teknolojia ya habari hapa
nchini yanafikiwa kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Wizara hizo mbili.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi alimkaribisha
Waziri huyo na Ujumbe wake Zanzibar na kumpongeza kwa kufika Zanzibar akiwa na
ujumbe wake kwa ajili ya kujitambulisha sambamba na kukutana na uongozi wa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Nae Waziri wa Wizara ya Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.
Faustine Engelbert Ndugulile alianza kwa kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuchaguliwa
kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar na kuonesha imani kubwa kwake.
Katika maelezo yake Waziri Ndugulile
alisema kuwa Wizara hiyo imeanzishwa tarehe 5, Disemba 2021 katika maandalizi ya kuiandaa
nchi kwenda katika uchumi wa kidijitali na Mapinduzi ya Viwanda sambamba na
kutengeneza Serikali ya Kimtandao na biashara Mtandao pamoja na sekta hiyo kuweza
kuwa na mchango katika pato la Taifa.
Alisema kwamba kwa msingi huo Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli aliona ni muhimu kuwa
na Wizara ambayo itakuwa inashughulikia Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Aliongeza kuwa kwa vile baadhi ya
majukumu ya Wizara hiyo ni ya Muungano hivyo amekuja Zanzibar na ujumbe wake na kufanya mikutano
ya mashirikiano na Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ambapo pia, alifanya ziara kisiwani Pemba kwa ajili ya kuvitembelea
vituo vya Tehama.
Alisema kuwa kikao chao na Waziri wa
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
kimekwenda vizuri na ana matumaini makubwa kwamba mafanikio makubwa zaidi yatafikiwa
huku akieleza azma ya ziara yake aliyoifanya kwa upandewa Unguja na Pemba.
Alisema kuwa kuhusu mradi wa anuani za
makaazi ambao unatekelezwa hapa Zanzibar wameamua kuuengezea kasi ambao umeanza
kwa ngazi za majaribio hasa kwa Zanzibar kutokana na kuimarika sekta ya Utalii
hivyo, ni vizuri mitaa ikawa na majina na majengo yakawa na namba ili kuweza
kufikika kirahisi na mradi huo kuwa na tija zaidi sanjari na kurahisisha
biashara mtandao.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment