Habari za Punde

RC Kaskazini Unguja Amepiga Marufuku Upigaji wa Ngoma za Vigodoro.

MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud akisoma Muelekeo wa Serikali ya Mkoa huo jinsi alivyojipanga katika miaka mitano ijayo  alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika Ukumbi wa Mkoa wa  Kaskazini Unguja Mkokotoni.

Baadhi ya Waandishi wa habari wakifatilia Muelekeo wa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja uliosomwa na  Mkuu wa Mkoa huo  Ayoub Mohammed Mahmoud huko Ofisini kwake Mkokotoni  .

Picha na Maryam Kidiko – Maelezo Zanzibar.

Na. Mwashungi Tahir. Maelezo 

MKUU wa Mkoa  Kaskazini Unguja Ayoub Mohammed Mahmoud amepiga marufuku ya upigwaji wa ngoma za vigodoro pamoja na khanga moja kama khanga moko  ikiwa sio utamaduni wa Wazanzibar .

Ameyasema hayo huko katika ukumbi wa Mkoa wa  Kaskazini Unguja wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jinsi alivyojipanga katika miaka mitano ijayo  kuhusu muelekeo wa Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja katika awamu ya nane.

Amesema kumekuwa na kawaida kwa wananchi kutoka katika sehemu mbali mbali   ya Zanzibar kuja katika Mkoa huo kucheza ngoma hizo na kuvunja mila na utamaduni ziliopo .

“Sio ruhusa kwa wakaazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja na wananchi kutoka sehemu nyengine  kuja kupiga ngoma na kucheza kwani ngoma hizo zimekosa  maadili”, alisema Ayoub.

Aidha amesema Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Unguja imelenga katika sekta ya Utalii kwani Mkoa huo una vivutio vingi ikiwemo mahoteli na mikahawa mikubwa na fukwe ambapo wananchi watapata kujua sehemu hizo.

Pia ameendelea kusema jinsi Mkoa ulivyolenga mambo mbali mbali yanayohusu jamii ikiwemo kilimo, mifugo, maji safi na salama, elimu , afya, barabara pamoja na michezo.

Hata hivyo amesema Serikali ya Mkoa huo imelenga katika kuimarisha viwanda vya kusindika vyakula kama mananasi  na mboga mboga ili wakulima wapate kuepukana na  hasara katika mazao yao wanayolima kila msimu.

Sambamba na hayo amesema Serikali ya Mkoa na kushirikiana na Serikali kuu katika  kudhibiti vyema masuala ya vitendo vya udhalilishaji, madawa ya kulevya, pamoja na rushwa na kuahidi hatovifumbia macho kwani vinarudisha nyuma maendeleo ya Taifa.     

Ayoub ameahidi kulisimamia suala zima kilimo cha umwagiliaji maji, kuboresha wafugaji na kuweka mazingira kuwa katika hali ya usafi. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.