Habari za Punde

Wafanyabiashara Kutoka Nchini Kenya Wakaribishwa Kuwekeza Zanzibar -Dk.Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Gavana wa Mombasa Nchini Kenya Mhe. Ali Hassan Joho, alipofika Ikulu Zanzibare kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la  Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Gavana wa Mombasa Nchini Kenya Mhe. Ali Hassan Joho (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo akiwa na Ujumbe wa Wafanyabiashara kutoka Kenya.

RAISwa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewakaribisha wafanyabiashara wa nchini Kenya kuja kuekeza na kufanyabiashara Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba pande mbili hizo zina historia katika sekta ya biashara.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Gavana wa Mombasa Kenya Ali Hassan  Joho akiwa amefuatana na ujumbe wa baadhi ya wafanyabiashara kutoka Mombasa ambao wameonesha kiu yao ya kufanya biashara kati ya Mombasa na Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alimueleza Gavana Ali Hassan Joho kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na wafanyabiashara ambao wana lengo la kuekeza na kufanya biashara hapa Zanzibar.

Alisisitiza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati maalum katika kuwavutia wafanyabiashara pamoja na wawekezaji ambapo kwa kupitia Mamlaka yake ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) itaendelea kuweka mazingira mazuri.

Alieleza kwamba pande zote mbili za visiwa vya Zanzibar tayari hatua za makausudi zinachukuliwa katika kuhakikisha shughuli za uwekezaji pamoja na kuwavutia wafanyabiashara zinatekelezwa kwa Unguja na Pemba.

Alisema kuwa Serikali imeweka milango wazi kwa wawekezaji na wafanyabishara kuja kufanya shughuli zao hizo katika sekta wanayoitaka huku kwani Sera, sheria na taratibu za kuhakikisha biashara kati ya pande mbili hizo zinafanyika vizuri.

Pamoja na hayo, alivutiwa na nia ya wafanyabiashara wa Mombasa kutaka kufanya biashara ya sukari inayotoka katika kiwanda cha sukari cha Mahonda cha Zanzibar na kupeleka katika soko la Mombasa na kueleza kwamba hatua hiyo itapanua soko la bidhaa hiyo.

Rais Dk. Mwinyi alimpongeza Gavana wa Mombasa nchini Kenya Ali Hassan Joho kwa kuja Zanzibar akiwa ameambatana na wafanyabiashara wa Mombasa na kumueleza kwamba Zanzibar iko tayari kuwakaribisha ndugu zao wa Mombasa kufanyabiashara nao.

Tanzania na Kenya zinauhusiano wa muda mrefu hasa kwa upande wa Mombasa na Zanzibar ambapo pande mbili hizo zina historia ya biashara.

Mapema Gavana wa Mombasa Kenya Ali Hassan  Joho alimueleza Rais Dk. Mwinyi lengo la azma ya safari yake kuja kuitembelea Zanzibar akiwa pamoja na wafanyabiashara wa Mombasa wakiwa na malengo ya kufanyabiashara kati ya pande mbili hizo.

Alisema kuwa wafanyabiashara hao wako tayari kufanyabiashara zao kati ya pande mbili hizo na baadhi yao wameshaanza mchakato wa biashara zao kwa kuamini kwamba soko la biashara hapa Zanzibar lipo.

Gavana Joho alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba historia inaoneshwa kwamba Zanzibar na Mombasa zina uhusiano na ushirikiano wa miaka mingi  hivyo, ni vyema ukaimarishwa.

Sambamba na hayo, Gavana Joho alieleza kwamba kwa upande wa sekta ya utalii kutokana na sehemu mbili hizo mazingira yake katika sekta hiyo kushabihiana ni vyema pakawepo mashirikiano ili kila upande uziidi kupanua wigo kwa mwenziwe kwa azma ya kukuza sekta hiyo.

Nao Wafanyabiashara waliofuatana na Gavana huyo wa Mombasa walieleza kiu yao kwa Rais ya kutaka kufanya biashara kati ya pande mbili hizo.

Wafanyabiashara hao walieleza kwamba wanaamini soko la Zanzibar litawasaidia kwa kiasi kikubwa pamoja na kuwasaidia wananchi wa Zanzibar kwani watapata kuuza biasharaa zao karibu kuliko wanavyofanya hivi sasa ambapo biashara zao wanafanya katika nchi zilizo mbali na Mombasa kama vile Burundi, Zambia, Congo na nchi nyenginezo.

Pamoja na hayo, walieleza kwamba badala ya kuingiza sukari kutoka nchi za Brazil na nyenginezo ni bora wakaagiza sukari kutoka Zanzibar ambako ni karibu na nchi yao.

Hivyo, Wafanyabiashara hao walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kasi yake ya kuimarisha uchumi wa Zanzibar sambamba na juhudi kubwa anazozichukua za kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara mbali mbali hatua ambayo itaipaisha Zanzibar kiuchumi.

 

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alifika Hospitali kuu ya Rufaa ya MnaziMmoja kwa ajili ya kuwakagua majeruhi wa ajali ya gari iliyotokea asubuhi ya leo huko Kitogani, Mkoa wa Kusini Unguja ambayo imewahusisha wafanyakazi wa kitengo cha habari cha Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

 

Akiwa ameongozana na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kuwakagua majeruhi hao waliopata ajali hiyo na kuwaombea kupona kwa haraka huku akimuombea kwa Mwenyezi Mungu kumlaza mahala pema peponi mmoja wa wafanyakazi hao aliyefariki dunia.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.