Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Ajumuika na Wananchi Katika Sala ya Ijumaa Msikiti wa Machomane Chakechake Pemba leo.

Makamu Wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akitoa salamu kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya UIjumaa katika Msikiti wa Machomane Chake Chake Pemba.
Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu wakifuatilia Hotuba ya Sala ya Ijumaa iliyotolewa na Sheikh Ali akisisitiza umuhimu kwa Waumini kuzingatia suala la Uadilifu unaowasogeza zaidi kwenye ucha Mungu.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdullah amewakumbusha Waumini wa Dini na Wananchi waendelee kuwa na subra katika kipindi hichi baada ya Taifa kupata Mtihani wa msiba kufuatia kifo cha Rais wa Awamu ya Tano Tanzania Marehemu Dr. John Pombe Joseph Magufuli.

Mh. Hemed Suleiman Abdullah alitoa kumbusho hilo  wakati akitoa salamu  kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu  mara baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa  katika Msikiti wa Machomane Chake Chake Kisiwani Pemba akianza ziara ya Siku Tano Kisiwani humo.

Alisema kifo ni Ibada na wajibu ambao kila kiumbe au nafsi yenye uhai itaonja na hatimae kurejea kwa yule aliyeziumba ambae ni Mwenyezi Mungu aliyeumba Mbingu na Ardhi.

Alieleza kwamba licha ya Mtihani huo wa Taifa  ni budi kwa Waumini na Wananchi wakaendelea kujenga matumaini makubwa ya jinsi Uongozi wa Serikali Kuu ulivyojizatiti kuwapatia huduma za msingi zitakazostawisha Maisha yao ya kila Siku.

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema katika  kufanikisha hayo alibainisha kwamba wakati Ahadi na Azma ya Serikali iko wazi muendelezo wa yale wanayoyatarajia Wananchi yataendelea kusogea kadri siku zinavyosonga mbele.

Akigusia vitendo vya udhalilishaji vinavyoleta aibu ndani ya Jamii Mh. Hemed alisema Serikali Kuu imefikia maamuzi ya kuondoa dhamana kwa watuhumiwa wa vitendo vya udhalilishaji kwa lengo la kudhibiti vitendo hivyo viovu visivyokubalika hata katika Sheria, Taratibu na Vitabu vya Dini.

Alitahadharisha kwamba Vyombo vya Dola tayari vimeshajipanga kukabiliana na vitendo hiyo vya Udhalilishaji na kuonya kwamba Kiongozi atakayeamua kusimamia suluhu katika jambo hilo kwa sasa atalazimika kuachia dhamana aliyokabidhiwa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman aliwasisitiza Wazazi na Walezi katika maeneo yote Nchini kuendelea kusimamia nyendo za Watoto wao hasa wakati wa mafunzo ya ziada ili kuwasidia kuwepuka dhidi ya majanga hayo ya udhalilishaji.

Kuhusu mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaokaribia siku chache zijazo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Wazazi wana jukumu la kuhakikisha Watoto wao wanashiriki vyema katika kujifunza Kitabu kitukufu cha Quran.

Alisema wajibu huo ni vyema ukaenda sambamba na Jamii ya Waumini kuendelea kuwafanyia wema Watoto yatima wenye haki ya kutunzwa kama walivyo watoto wengine katika Jamii iliyowazunguuka.

Akitoa Hotuba ya sala ya Ijumaa Sheikh Ali alisisitiza umuhimu wa uadilifu miongoni mwa Waumini ikiwa ni nguzo muhimu kwao katika kufikia ucha mungu uliotukuka.

Sheikh Ali aliwaeleza Waumini hao kwamba uadilifu lazima uzingatie haki hata kama utamuumiza Tajiri au fakiri ambao baadhi yao wanaangalia zaidi  kuridhisha nafsi.

Alifahamisha kwamba pale inapotokea ugomvi au hitilafu baina ya Waumini suluhu ni jambo la msingi na wajibu itakayozingatia uadilifu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.