Habari za Punde

Benki ya Afrika Yaunga Mkono Juhudi za SMZ Kuimarisha Uchumi Wake Kupitia Uchumi wa Bluu.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimia na Ujumbe wa Uongozi wa Benki ya Afrika ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Dr.Nyamajeje Calleb, walipofika Ikulu jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dk. Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Bank Of Africa ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Afrika Dr.Nyamajeje Calleb (kulia kwa Rais) akiwa na Ujumbe wake Ndg.Wasira Mushi na Samira  Yassine, walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha, mazungumzo hayo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar

Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Afrika Dk. Nyamajeje Calleb akiwa amefuatana na uongozi wa Benki hiyo ambapo alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha uchumi wake hasa kupitia uchumi wa buluu.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipongeza Benki hiyo kwa kuonesha utayari wake wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi katika kuimarisha uchumi wake hasa katika sekta ya uchumi wa buluu ambayo inajumuisha utalii, uvuvi pamoja na mafuta na gesi asilia.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo hatua zinazochukuliwa na Serikali anayoiongoza katika kukuza uchumi wake ikiwa ni pamoja na mikakati iliyowekwa na Serikali anayoiongoza katika ujenzi wa bandari kubwa ya kisasa ya Magwapwani sambamba na hatua zilizowekwa katika kukukuza uchumi wa buluu.

Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Afrika Dk. Nyamajeje Calleb alimueleza Rais Dk. Mwinyi historia ya kuanzishwa kwa Benki hiyo hapa nchini pamoja na shughuli zake inazozifanya ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Alimueleza Rais Dk. Miwnyi jinsi Benki hiyo inavyofanya shughuli zake katika kuwasaidia wananchi katika miradi yao ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo pamoja na kushirikiana na  Serikali katika kuimarisha baadhi ya miradi ya maendeleo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.