Habari za Punde

Chanjo ya Kujikinga na Covid 19 Inayotarajiwa Kutolewa Nchini na Hiari na Hakuna Mtu Atakayelazimishwa.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pia Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Dk.Hussein Ali Mwinyi  alipokuwa akizungumza na Wananchi na Wanachama wa Chama hicho wa Wilaya ya Kaskazini "B" katika mkutano wa kuwashukuru uliofanyika leo katika  Ofisi za   CCM Mahonda (kushoto)  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Mhe.Iddi Ali Ame

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa corona ambayo inatarajiwa kutolewa nchini ni hiari na hakuna mtu atakayelazimishwa kufanya hivyo kwa nguvu.

Dk.Mwinyi alisema hayo huko katika Ofisi za Chama Cha Mapindizi (CCM) Mahonda Mkoa wa kaskazini Unguja wakati akizungumza na viongozi wa CCM wa Mkoa huo katika ziara ya kuwashukuru wananchi na wana CCM wa Mkoa huo baada ya kukichaguwa chama hicho kushika hatamu ya kuongoza dola katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana.

Alisema kuwa Serikali italeta chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa Corona lakini hiyo itakuwa hiari kwa mtu anayehitaji na silazima kama baadhi ya wananchi wanavyodai kiasi ya kuzusha taharuki.

Kwa mfano alisema chanjo hiyo itatolewa kwa mahujaji wanaotarajiwa kufanya ibada ya Hijja huko Makka, Sauda Arabia ambayo ni sehemu ya masharti ya Serikali hiyo kwa mahujaji watakaotekeleza ibada ya Hijja ili kupunguza uwezekano wa kuibuka kwa mripuko wa maradhi hayo.

''Ndugu wananchi napenda kuweka wazi na bayana  suala hili.....chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa corona ni hiari na hakuna atakaye lazimishwa ingawa kwa upande wa mahujaji Serikali ya Sauda Arabia wametutaka mahujaji watakaofanya ibada hiyo lazima wapewe chanjo''alisisitiza.

Katika hotuba yake hiyo Rais Dk. Mwinyi amesema kuwa katika kipindi cha miezi sita akiwa katika madaraka niamefanikiwa kujenga nidhamu na uwajibikaji na kuweka vizuri misingi ya  matumizi ya fedha za umma.

Alisema katika kipindi cha miezi sita amefanya mambo makubwa matatu ikiwemo kujenga mashikamano kwa wananchi wa Zanzibar kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye lengo la kuleta maridhiano ya kisiasa.

Dk. .Mwinyi alisema maridhiano hayo yamefunguwa milango ya wananchi kuelewana na kuondosha siasa za chuki na uhasama zilizokuwepo ambazo kwa kiasi kikubwa zilirudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

''Huwezi kupata maendeleo kama wananchi wako hawana amani...wanagombana na kujenga chuki na uhasama katika kipindi cha miezi sita tumefanikiwa kuwaunganisha wananchi wote na sasa wanafanyakazi pamoja na kuweka pembeni tofauti zao''alisema.

Aidha, alisema katika kipindi cha miezi sita amekuwa akifanyakazi kuweka vizuri mifuko ya ukusanyaji wa kodi ambayo kwa kweli ilikuwa haipo vizuri huku ikiwa chanzo kikubwa cha upotevu wa mapato.

Alisema mapato yamekuwa yakivuja katika taasisi zake na kutoa mfano wa Shirika la Umeme la Zanzibar (ZECO) ambalo halifanyi vizuri katika makusanyo yake kwa sababu hakuna mifumo mizuri.

''Mapato yanapotea ambapo katika kipindi cha miezi sita tumefanya kazi ya kudhibiti na kuongeza ufanisi wa uwajibikaji kwa watendaji walio kabidhiwa dhamana''alisema Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, aliwajuulisha wananchi malengo yaliyowekwa ambayo yamo katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ikiwemo ujenzi wa bandari na miundombinu yake tayari wawekezaji wapo wanatusubiri sisi.

Alisema ujenzi wa miundombinu hiyo kwa kiasi kikubwa itasaidia kutengeneza ajira zipatazo 300,000 katika sekta mbalimbali ikiwemo kazi za ujasiriamali na wavuvi.

''Hiyo ndiyo mikakati yetu kujenga miundombinu ya bandari huko Mangapwani na Mpigaduri Maruhubi...tunakwenda vizuri katika kipindi cha miezi sita''alisema.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza miongoni mwa mikakati iliyowekwa na Serikali yake katika kuliimarisha zao la karafuu ikiwa ni pamoja na kuanzisha kiwanda cha kusarifu karafuu hapa hapa Zanzibar ambapo tayari wawekezaji wameshajitokeza.

Alirejea kauli yake ya kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuishughulikia migogoro yote ya ardhi, huku akielez aazma ya Serikali anayoingoza ya kujenga kilomita 200 za barabara za ndani na kilomita 200 za barabara kuu za Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ahadi alizozitoa kwa upande wa Serikali na Chama ahadi zake zote zipo pale pale, pia, alieleza haja kwa jamii kuwatizama watu wenye ulemavu kwa jicho la huruma.

Mapema mwenyekiti wa chama cha mapinduzi mkoa wa kaskazini Unguja Iddi Ame Haji alimpongeza Rais Dk.Hussein Mwinyi kwa kuanza vizuri katika uongozi wake wa kuiongoza Zanzibar katika awamu ya nane.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Kaskazini Unguja kinamuunga mkono Dk.Mwinyi katika kipindi cha uongozi wa miezi sita ya kuongozi Zanzibar ambapo wameshuhudia kuwepo kwa maridhiano ya kisiasa yaliyofungua  milango ya maelewano kwa wananchi wote.

 'Sisi wananchi na wanachama wa C C M Mkoa wa kaskazini Unguja tunakuunga mkono katika uongozi wako ambapo umeanza vizuri kuelekea katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi''alisema Haji.

Mapema Rais Dk. Mwinyi aliwapa nafasi viongozi hao ya kuzungumza ambapo walieleza changamoto zinazowakabili pamoja na kutoa ahadi ya kuendelea kumuunga mkono katika uongozi wake kutokana na kasi kubwa ya maendeleo aliyoanza nayo na hatua anazozichukua kwa wabadhirifu wa mali ya umma.

 Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.