Habari za Punde

Halmashauri Nchini Zatakiwa Kutambua, Kuhifadhi na Kuendeleza Maeneo ya Malikale Ili Yatumike Kiutalii.

 

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Ludovick Nduhiye akifungua kikao cha wadau kujadili utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 kilichofanyika leo jijini Mwanza. Wengine katika meza kuu ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Malikale, Dkt. Christowaja Ntandu (kulia) na Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Mwalimu Martin Nkwabi (kushoto)
Washiriki wa kikao cha wadau kuhusu utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Ludovick Nduhiye (hayupo pichani) leo jijini Mwanza.

Na Happiness Shayo- Mwanza                                                                                                                    

Serikali imeziagiza Halmashauri za Wilaya nchini kuhakikisha zinafanya jitihada za kutambua, kuhifadhi na kuendeleza maeneo ya malikale yaliyopo katika maeneo yao ili yatumike kiutalii. 

Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw.Ludovick Nduhiye alipokuwa akifungua kikao cha wadau cha kujadili utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 kilichofanyika jijini Mwanza leo. 

Bw. Nduhiye amesema agizo hilo ni utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008.

“Serikali za Mitaa zinashauriwa kushiriki ipasavyo katika uhifadhi, uendelezaji na utangazaji wa maeneo ya malikale kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 na Sheria ya Malikale Sura 333 hususani kifungu cha 16 kinachoelekeza Serikali za Mitaa kutunga sheria ndogondogo kwa ajili ya kuhifadhi, kulinda na kuendeleza malikale zilizopo katika maeneo yao” amesisitiza Bw. Nduhiye.

Naibu Katibu Mkuu Nduhiye amesema kuwa ni halmashauri chache sana zinazoshiriki katika kuhifadhi na kuendeleza malikale.

“Serikali za Mitaa zinazoshiriki katika uhifadhi na uendelezaji wa malikale nchini ni chache mfano, Halmashauri ya Manispaa – Iringa na Halmashauri ya Mji wa Kihistoria Mikindani, Bagamoyo na Tanga” Bw. Nduhiye ameongeza.

Aidha, ametajaidadi ya maeneo ya malikale yaliyopo nchini Tanzania kufikia 131 ambapo kati ya hayo yanayohifadhiwa na Serikali Kuu na kuwekewa miundombinu ni 18 tu sawa na asilimia 60% na kufafanua kwamba maeneo mengine yaliyobaki yanamilikiwa na watu binafsi na taasisi za umma

Pia amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ipo tayari kuzisaidia Halmashauri kuyatangaza maeneo ya malikale yaliyopo ili yahifadhiwe na kulindwa kwa mujibu wa Sheria.

Naye, Msimamizi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Kanda ya Ziwa, Gloria Munhamboamesema kikao hicho kitasaidia kuainisha maeneo mapya ya vivutio vya malikale vitakavyosaidia kuongeza mazao mapya ya utalii na kuongeza kipato kwa wananchi wanaohusika na utunzaji wa malikale hizo.

Kikao cha wadau cha kujadili utekelezaji wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008 kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Watendaji wa Halmashauri za Mkoa wa Mwanza na wadau kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustion, Makumbusho ya Kanisa Katoliki Bujora na Mwakilishi wa Utemia wa Ng’wanza(Mwanza).

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.