Habari za Punde

Wazanzibar Wapongezwa Kwa Utulivu Wao Wanaoendelea Kudumisha Amani Nchini. Mhe.Hemed

Na.Othman Khamis.OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amewashukuru Wazanzibari kwa utulivu wao wanaoendelea kuuonyesha uliopelekea kutanda kwa Amani ya Nchi inayoiwezesha Jamii kuendelea na harakati zao za Kimaisha bila ya wasi wasi.

Mheshimiwa Hemed alitoa shukrani hizo mara baada ya kukamilika kwa Futari ya pamoja aliyowaandalia iliyofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakili Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema Amani ni suala linalopaswa kuendelezwa muda wote wa maisha ya Mwanaadamu na haitapendeza kuachiwa Kikundi au Mtu akapewa fursa ya kumuelekeza shetani katika kuvuruga Tunu hiyo ya Taifa inayokosekana kwa baadhi ya Mataifa Ulimwenguni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alishauri kuandaliwa kwa utaratibu wa kuwaomea Viongozi wa Kitaifa na Nchi kupitia Shehia, mitaa hata Mikoa na Wilaya wavuke salama katika kuiona Nchi inaendelea vyema Kimaendeleo na Ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliwakumbusha Waumini kwamba unyenyekevu na wema waliyouonyesha ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani uedelezwe katika miezi mengine inayofuata.

Alibainisha kwamba yale makosa na mapungufu madogo madogo yaliyojichomoza ndani ya harakati zao katika kipindi hichi ni vyema yakapatia ufumbuzi katioka njia muwafaka isiyoleta hitilafu kwa upande wowote wa Jamii.

Mapema akitoa shukrani kwa niaba ya Washiriki wa Futari hiyo ya pamoja Mkuu wa Mkoa Majini Magharibi Mheshimiwa Idrissa Kitwana Mussa alisema Muumini anapomfutarisha mwenzake moyo wa upendo kati yao huongezeka mara dufu.

Mheshimiwa Idrissa alimpongeza na kumshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimwa Hemed Suleiman Abdulla kwa kitendo chake cha kuwakusanya wenzake katika Futari ya pamoja jambo linalopaswa kukumbukwa kila mara.

Futari hiyo ya pamoja iliyoandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni miongoni mwa mfululizo mwa matendo hayo yanayofanywa na Viongozi Wakuu katika kujumuika pamoja na Viongozi na Wananchi mbali mbali katika maeneo tofauti Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.