Wazazi na walezi wametakiwa kutokuwa na muhali kwa watu wanaowafanya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto na wanawake ili kufikia lengo la Serekali la kuondosha udhalilishaji nchini.
Hayo yameelezwa na afisa wa dawati jinsia wanawake na watoto Mkoa wa Kusini Unguja Najat Saleh Abdulkadir wakati akiwasilisha mada ya udhalilishaji katika kikao cha Baraza la UWT Jimbo la Tunguu huko Tunguu.
Amesema kesi nyingi za udhalilishaji zinashindwa kufikia hukumu kutokana na wazazi au walezi na wahanga wa udhalilishaji kukataa kwenda mahakamani kutoa ushahidi Mahakamani kwa kuhofia muhali utakao jitokeza baada ya hukumu.
Akielezea Wilaya ya Kati amesema kwa sasa vitendo vya udhalilishaji vinavyoripotiwa kwa wingi ni kwa watoto wa kike wa miaka 14 hadi 17 kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile au kupewa ujauzito.
Akizitaja sababu zinazopelekea kuongezeka kwa vitendo vya udhalilishaji ni pamoja na talaka ,watoto kushirikishwa katika mambo ya kikubwa , ubinafsi na watu kuenda kinyume na mafundisho ya dini zao.
Nae mwenyekiti wa UWT Mkoa wa kusini Unguja Shemsa Abdallah Ali amewhimiza wazazi na walezi kurejesha malezi ya zamani kwa kuwalea watoto kwa mashirikiano kitu kitakachosaidia kuondosha vitendo hivi.
Wakati huo huo mgeni rasmi wa baraza hilo Semeni Khamis Vuai akifungua mkutano wa Baraza hilo amewataka wanachama wa UWT wa jimbo la Tunguu kulipa ada ili waweze kuwa wanachama hai na kufanikisha malengo ya Chama Cha Mapinduzi ya kupata ushindi katika chaguzi zijazo.
Aidha katibu wa Chama cha Mapinduzi wa Jmbo hilo Sharifa Maabadi amewataka wanachama hao kujitokeza kwa wingi katika kuomba nafasi mbali mbali za uongozi kwa chaguzi za ndani zinazo tarajiwa kuanza ifikapo mwaka 2022.
Nao wajumbe wa Baraza hilo wameushukuru uongozi wa Jimbo hilo kwa kuwapatia elimu inayohusu vitendo vya udhalilishaji na kusema kuwa wapo tayari kumunga mkono Rais wa Zanzibar Dkt Husein Ali Mwinyi katika harakati za kuondosha vitendo vya udhalilishaji hapa nchini.
No comments:
Post a Comment