Na Hamida Kamchalla, TANGA.
Kuelekea kwenye utekelezaji wa mradi mkubwa wa bomba la mafuta linalotokea Hoima nchini Uganda kuja Tanzania, wananchi wametakiwa kuwa makini na matapeli wanaotangaza nafasi za ajira na kuwalaghai kwa kuchukua pesa ili kutoa ajira.
Ofisa Mahusiano wa TPDC Francis Lupokela aliyasema hayo jana akiwa katika banda la maonyesho ya nane ya biashara mkoni Tanga na kusema muda wa kuanza utekelezaji huo umewadia hivyo wananchi wawe watulivu kwa kuwa nafasi za ajira zitatangazwa moja kwa moja kupitia vyombo vya habari na Taasisi zingine zenye mamlaka.
"Mradi wa bomba tayari umeshakidhi vigezo vilivyohitajika katika kupata kandarasi mbalimbali katika sekta yetu lakini pia hata nafasi za ajira zipo na zitatolewa kwa utaratibu maalumi, hazitangazwi vichochoroni, zitatangazwa kupitia vyombo vya habari na taasisi nyingine za serikali ambazo zina mamlaka ya kutoa matangazo ili watu wafahamu", alisema.
"Lakini pia zipo ajira ambazo tutaingia makubaliano na vijiji kwa maana vibarua, kwa mfano tumeingia kijiji fulani pale tunahitaji vibarua na hatujui watu wa eneo hilo inabidi tuonane na uongozi wa kijiji, kwahiyo niwaombe wananchi wasipotoshwe na hao wanaoingilia kazi hiyo" aliongeza Lupokela.
Aidha alibainisha kwamba mradi huo una faida kubwa kwa Watanzania katika fursa za biashara kutokana na ukubwa wa eneo lililopo ambalo ni takribani kilomita 1447 tofauti na nchi ulikotokea mradi huo jambo ambalo wananchi wataweza kufanya biashara mbalimbali kuliko wote kukimbilia kwenye ajira.
Lupokela alifafanua kwamba mradi huo utakuwa na miundombinu mbalimbali ambayo itajengwa katika utekelezaji huo na kutoa fursa nyingi kwa wananchi kutoka nje na ndani ya mkoa wa Tanga ambapo pia wazawa wa maeneo yanayopitiwa watapewa kipaumbele kwa wale watakaokuwa na uwezo wa kufanya kazi.
"Mradi wetu utakuwa na miundombinu mbalimbali, utakuwa na bomba, utakuwa na vituo vya mashine za kusukuma, lakini pia utakia na vituo vya kupoza mshkumo wa mafuta yatakapokiwa yanakaribia kufika bandarini, pamoja na kujengwa mapipa manne katika bandari ya Tanga ambayo kila moja litaingia lita laki tano" alifafanua.
"Hapo hapo pia kutakuwa na miundombinu mingine wezeshi itakayoweza kupakia matenji kwenye meli ya usafirishaji lakini pia kujenga nyumba na ofisi za wafanyakazi, kwahiyo hapo tunaona fursa zilizopo kupitia mradi katika mkoa huu wa Tanga" alisisitiza.
Hata hivyo Lupokela alisema mradi huo una maeneo mawili mbayo yana kipaumbele na yatakapokamilika muda siyo mrefu utekelezaji utaanza na katika maeneo hayo mokawapo ni ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya mradi huo.
"Kuna maeneo mawili katika mradi wetu, maeneo ya kipaumbele ambayo yatakuwa ndio kambi na karakana na sehemu ya kuhifadhi vifaa na hii ni muhimu kwakuwa ili kazi iendelee na vifaa vifike basi maeneo haya ni lazima yawepo na kwa watu waliopitiwa katika maeneo yao zoezi la fidia litaenda kufanyika muda siyo mrefu sana" alisema.
"Ni kwamba mara tu, tutakapomaliza katika eneo hili tunakuja eneo la njia ya bomba ambapo baada ya kukamilisha hapo kwenye zoezi la utoaji wa ardhi tunaenda kwenye shuhuli zenyewe sasa za utekelezaji" aliongeza.
No comments:
Post a Comment