Habari za Punde

CCM Yatoa Maelekezo Mahususi Kwa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndugu Shaka Hamdu Shaka akizungumza na wananchi katika shina 4 kata ya Inyala halmashauri ya wilaya ya Mbeya baada wananchi kuwasilisha  malalamiko yao kwake kuhusu kupigwa, kukamatwa hovyo na kuwekwa ndani pamoja na kuondoshwa katika mashamba yao.


Chama Cha Mapinduzi kimesema  kinathamini, kinaheshimu na kuuunga mkono uhifadhi wa maliasili na uoto wa asili katika hifadhi  za taifa, mapori ya akiba na misitu nchini.

Pamoja na hayo kimesema  uhifadhi endelevu unahitaji ushirikishwaji mkubwa wa jamii na uzingatie mahitaji ya msingi ya wananchi wanaozunguka maeno hayo.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndugu Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika shina 4 kata ya Inyala halmashauri ya wilaya ya Mbeya baada wananchi kuwasilisha  malalamiko yao kwake kuhusu kupigwa, kukamatwa hovyo na kuwekwa ndani pamoja na kuondoshwa katika mashamba yao waliyokuwa wakiyalima tangu mwaka 1977.

Shaka amesema kwa muda mrefu sasa wananchi wamekuwa wakipaza sauti za vitendo vya uonevu, ukatili, unyanyasaji, migogoro ya mipaka na hata uporoji wa mali kutoka kwa baadhi ya askari wa uhifadhi wa TANAPA au wakala wa misitu pamoja na uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyama pori.

"Ajabu wanaohusika wametia pamba masikio sasa Chama tunaielekeza wizara ya maliasili na utalii wachukue hatua za haraka kumaliza kero hizi. Hatuwezi kila wakati wananchi wanaoishi apembezoni na maeneo yanayohifadhiwa wakawa wahanga wa uhifadhi badala ya kuona neema." amefahamisha Shaka.

Shaka amezitaka mamlaka  za uhifadhi zije na programu za kuwawezesha pia wananchi hawa kiuchumi ili waone thamani ya uwepo wa shughuli hizo za uhifadhi katika maeneo yao na wahamasike kuona wanao wajibu wa kuunga mkono uhifadhi. Pia, waongeze juhudi ya kutoa elimu ya uhifadhi na kushiriki katika shughuli za maendeleo ya wananchi ili kuimarisha ujirani mwema.

Hata hivyo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya Ndugu Stephen Katemba amemueleza Ndugu Shaka kuwa atawasiliana na mamlaka hizo kwa kushirikiana na mkuu wa wilaya ili kuwapa wananchi utulivu na amani katika shughuli zao za kila siku za kiuchumi.

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo pamoja na Sekretarieti yake ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mbeya.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.