Habari za Punde

Mhe. Bashungwa Kufunga Tamasha la Muziki wa Cigogo


Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha kubwa la Ngoma za asili linalofahamika kama Tamasha la Cigogo litakalo fanyika Julai 24 na 25, 2021 katika viwanja vya Kituo cha Sanaa Chamwino Ikulu Jijini Dodoma

Na.Adeladius Makwega, (WHUSM)-Dodoma.

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha kubwa la Ngoma za asili linalofahamika kama Tamasha la Cigogo litakalo fanyika Julai 24 na 25, 2021 katika viwanja vya Kituo cha Sanaa Chamwino Ikulu Jijini Dodoma

Akizungumza  na Vyombo  vya  Habari  Julai 22, 2021 Jijini Dodoma  Kaimu Mkurugenzi wa  Maendeleo ya Sanaa  Mfaume  Said amesema kuwa  tamasha hilo linaandaliwa na Wizara  ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na Kituo cha Sanaa Chamwino  Mkoani Dodoma na litakuwa la kukata  na shoka –nguo kuchanika, ambapo  amewasihi  wakaazi wa Dodoma na  viunga vyake  kujitokeza   kwa wingi.

“Hili ni tamasha linalowakutanisha wasanii wa  ngoma  za asili  zaidi ya 600 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania tuna imani  litakuwa ni fursa  kubwa  kwa wapenzi wa  ngoma  za asili kupata burudani ambayo  haijawahi kutokea” amesema Mkurugenzi huyo.

Tunatambua na halina  ubishi kuwa kwa  muda  mrefu Watanzania tumekuwa  tukitilia  mkazo  Sanaa ya muziki wa dansi, muziki wa nje na bongo  fleva tu  lakini muziki wa kitamaduni umekuwa kando mathalani,   muziki huu umekuwa  haurudiwi kwa wingi  na kuchezwa  katika  vyombo vya  habari kama vile  luninga na redio.

Bw. Mfaume amesema kufanyika kwa tamasha hilo la muziki wa wagogo litaibua ari ya kuikuza zaidi Sanaa ya ngoma za asili.

Kwa upande wake  Mwenyekiti wa  Kituo cha Sanaa  Chamwino ,Dkt Kedomn Mapana amesema kuwa wao kama kituo  wamekuwa wakiandaa  matamasha  ya namna hiyo kwa  kipindi cha mika  16 sasa na tamasha la mwaka huu litakuwa  la 12 likiwa na kauli mbiu  “Utamaduni wetu Maendeleo  yetu”.

“Tumemualika  Naibu Waziri wa Ofisi  ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Deograthias  Ndejembi  katika ufunguzi akiambatana na Katibu Mkuu  wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Hassan Abbas na litahitimishwa  na  Waziri wa  Habari ,Utamaduni, Sanaa na Michezo  mheshimiwa Innocent Bashungwa  amesema Dkt  Mapana.

Akizungumzia Tamasha hilo Mkuu wa  Mtaa wa  Talama Chamwino Ikulu,  ndugu Andason Makolokolo amesema kuwa sasa  Dodoma imekuwa jiji  na kumekuwa na muingiliano wa makabila mengi lakini jumamosi na jumapili itakuwa wasaa wa  Wagogo kuonyesha utamaduni wao kwa  vitendo.

“Digule ndina mwenda, ulambi nani kadigulila ulambi. Digule dina shati, ulambi nani kadigulila ulambi” aliimba Mkuu huyo wa mtaa wa Talama.

Ndugu Makolokoli alifafanua kuwa hiyo ni sehemu tu ya wimbo wa Kigogo akisema panya ana nguo nani amemnunulia huo ni uwongo, panya ana shati, huo uwongo nani kamnunulia. Akisema wimbo huo unaimbwa na wagogo mara baada ya mavuno kusherekea furaha ya mavuno.

Kituo cha Sanaa Chamwino kwa  muda mrefu kimekuwa ni miongoni mwa mashirika  yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kwa  karibu na serikali kwa kukuza sanaa na utamadauni wa Mtanzania ambapo kilisajiliwa kwa mujibu wa Sheria Nambari 23 ya mwaka 1984 ya  Baraza  la Sanaa la Taifa  BASATA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.