Habari za Punde

CCM Mkoa wa Magharibi kichama watakiwa kufanya kazi kwa mashirikiano

Mjumbe wa Kamati ya halimashauri kuu ya CCM taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akitoa hotuba yake wakati akiyafungua mafunzo elekezi kwa viongozi wa Jumuiya ya wazazi wilaya Mjini yaliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa SUZA Kampasi ya Maruhubi
Viongozi na Wanachama wa Jumuiya ya wazazi ya Mjini wakifuatilia hotuba ya mjumbe wa Kamati Kuu Mhe. Hemed wakati akiyafungua mafunzo elekezi kwa viongozi  yaliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa  SUZA Kampasi ya Maruhubi.
Viongozi na Wanachama wa Jumuiya ya wazazi ya Mjini wakifuatilia hotuba ya mjumbe wa Kamati Kuu Mhe. Hemed wakati akiyafungua mafunzo elekezi kwa viongozi  yaliofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Taifa  SUZA Kampasi ya Maruhubi.

Na Kassim Abdi, OMPR

Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi Kichama wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili, miiko pamoja na misingi ya chama hicho sambamba na kufanya kazi kwa mashirikiano ili kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halimashauri kuu ya CCM taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo katika Mkutano maalum uliwashirikisha wajumbe wa halimashauri ya Mkoa, wilaya, mabaraza ya Jumuiya za chama cha Mapinduzi uliofanyika katika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Dimani uliopo Kiembesamaki.

Alieleza kuwa, Viongozi wa Chama cha Mapinduzi wana jukumu la kuisimamia serikali katika kuhakikisha ilani ya CCM 2020/2025 inatekelezwa vyema na viongozi wanatekeleza miradi mbali mbali iliopo serikalini.

Aliewaleza viongozi hao wa chama kwamba, wasisite kuitembelea na kuikaguwa miradi inayotekelezwa na serikali katika ngazi za wilaya na Mkoa pamoja na kutoa maelekezo pale inapohitajika lengo likiwa ni kuhakikisha ahadi zilizotolewa na viongozi wakadi wakiinadi ilani hiyo zinatakelezwa kwa vitendo.

Mjumbe huyo wa Kamati kuu alisema bajeti ya serikali iliopitishwa karibuni na wajumbe wa baraza la wawakilisha inalenga kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili wananchi wake pamoja na kuwaletea maendeleo.

Katika Kikao hicho Mhe. Hemed aliwataka viongozi wanaofanya kazi ya kuwasimamia wananchi katika majimbo kuepuka kupikiana majungu na kufitiniana na badala yake wafanye kazi kwa kushirikiana pamoja kwa kuwashirikisha vingozi wa serikali na Chama katika ngazi za Mikoa na Wilaya wakati wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumzia uchaguzi wa ndani ya chama unaotarajiwa kufanyika mwakani (2022) Mjumbe huyo wa Kamati Kuu aliwaagiza viongozi hao na wanachama wa Chama cha Mapinduzi kufuata miongozo na taratibu za chama kwa kuacha tabia ya kupanga Safu kabla ya uchaguzi kwani kufanya hivyo kunasababisha kuibuka kwa makundi yasiokuwa na tija katika kukijenga chama.

Alionya kuwa, kwa mwanachama yoyote yule atakaebainika kukiuka misingi ya chama kwa kuanza kupanga safu mapema kabla ya uchaguzi basi uongozi wa Chama taifa hautasita kumchukulia hatua ikiwemo kulikata jina lake kwa nafasi alioiomba.

Akigusia tatizo la madawa ya kulevya, Mhe. Hemed aliwaomba viongozi hao kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali kuu katika kupambana na kadhia hiyo ili kujenga taifa yenye Afya njema na kupata viongozi bora  wa baadae.

Alifafanua kuwa, Serikali itachukua hatua kali ikiwemo kufanya marekebisho ya baadhi ya sheria kwa lengo la kuwadhibiti wale wote wanaojihisisha na vitendo haramu vya kuharibu jamii ya wazanzibar.

Aliwatanabahisha kwamba serikali haitokuwa na woga wala muhali dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo viovu vya madawa ya kulevya vinavyoharibu vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed aliikumbusha jamii wakiwemo Jumuiya ya wazazi kurudi katika jukumu lao la msingi la kusimamia malezi bora kwa watoto wao ili kuwaepusha dhidi ya vitendo vya udhalilishaji vilivyokisiri katika jamii.

“Kila mtu anze kuchunga maadili katika familia yake” Alisema Mhe. Hemed

Nae, Katibu wa CCM Mkoa wa Magharibi kichama Ndugu Mgeni Mussa alimuleza Mjumbe huyo wa Kamati kuwa, hali ya Usalama katika Mkoa huo imeimarika vizuri kutokana na mashirikiano mazuri yaliokuwepo baina ya viongozi wa Chama na serikali.

Alisema Chama kupitia Mkoa wa Magharibi kimefanikiwa kuwasajili wanachama wake wapatao Shirini na Saba Elfu mia sita Themanini na Saba (27,687) kwa njia ya Kieletronic.

Mapema, Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halimashauri kuu ya CCM taifa alifungua mafunzo elekezi ya vionjgozi wa Ngazi ya matawi, wilaya kwa Jumuiya ya wazazi wilaya ya Mjini yaliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha SUZA kamapasi ya Maruhubi.

Akiyafungua mafunzo hayo, Mhe. Hemed alitoa wito kwa Jumuiya za Chama kubuni miradi itakayosaidia Jumuiya hizo kujijenga Kiuchumi ili ziweze kujitegemea kwa ajili ya kuimarisha uhai wa chama cha Mapinduzi.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.