Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
SERIKALI imeendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazowakabili Vijana nchini ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kufungua fursa zaidi kama vile fursa za ajira, mitaji na kutengeneza mazingira wezeshi na jumuishi yatakayowasaidia kushiriki kikamilifu kwenye nafasi mbalimbali za Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobas Katambi alipokutana na Waandishi wa Habari katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana (International Youth Day) Agosti 12, 2021 kwenye Ukumbi wa Mkutano uliopo PSSSF, Jijini Dodoma.
Alieleza kuwa, Serikali inaungana na Jumuiya ya kimataifa katika kuthamini mchango wa Vijana katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii kutokana na kushiriki kwao kikamilifu katika shughuli za Maendeleo ya Kiuchumi, kisiasa na kijamii.
“Dhumuni kuu la kuadhimisha siku hii ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa na jamii kwa ujumla kupata fursa ya pamoja ya kusherehekea na kutambua nafasi ya Vijana katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Nchi zao. Hii inatokana na ukweli kwamba vijana ndio kundi kubwa katika jamii yoyote na Vijana ndio wenye nguvu zaidi za kufanya kazi, Vijana ni wabunifu, Vijana ndio chachu ya mabadiliko chanya katika jamii na Vijana ndio warithi wa Mataifa yao,” alieleza Naibu Waziri Katambi
Katika kuthamini mchango wa vijana kuelekea siku hiyo Serikali imeendelea kuweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria inayowapa vijana fursa pana ya kushiriki katika kazi za maendeleo kwa ari na ubunifu mkubwa.
Alifafanua kuwa makadirio ya utafiti wa nguvu kazi (ILFS), idadi ya watu walio katika ajira imeongezeka kutoka watu milioni 20 mwaka 2014 na kufikia milioni 22.6 mwaka 2020. Ongezeko hilo limetokana na utayari na ushiriki mkubwa wa vijana kufanya kazi katika sekta binafsi.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhesimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwawezesha vijana kujiendeleza kupitia ubunifu ambapo pamoja na kutatua changamoto mbalimbali katika jamii lakini pia vijana wamekuwa wakihimizwa kutumia Ubunifu wao kujiajiri,” alisema
Aliongeza kuwa Ofisi ya Waziri ya Mkuu – Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Programu ya Taifa ya kukuza Ujuzi vijana zaidi ya 52,353 wamewezeshwa kumudu ushindani katika soko la ajira kupitia mafunzo mbalimbali ya kukuza ujuzi ambapo katika kipindi cha Miaka Mitano tayari vijana 28,941 wamepatiwa mafunzo ya Uanagenzi, Vijana 14,432 wamepata mafunzo ya Kurasimisha Ujuzi na vijana 8,980 wamepata mafunzo ya kilimo kupitia teknolojia ya Kitalu Nyumba.
Aidha, Naibu Waziri Katambi ilitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau mbalimbali wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi waliosaidia kufanikisha maadhimisho haya kwa kuwakutanisha vijana na kujadili masuala muhimu yanayogusa ustawi wao.
Pia aliwasihi Vijana kuwa wazalendo na kuwa pamoja na kuwa na moyo wakujitolea kufanya kazi ili kuonyesha ujuzi wao badala ya kusubiri ajira pamoja na kutoa mawazo chanya yatakayopelekea Taifa kusonga mbele.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa UNFPA, Dkt. Mariam Ngaeje alisema kuwa shirika hilo linatambua juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kwa kuwa mstari wa mbele kutetea haki na maslahi ya vijana.
“UNFPA pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa ikiwemo UNICEF, UNESCO, UNAIDS, WHO na ILO tutaendeelea kushirikiana na serikali pamoja na vijana na wadau wengine katika kuleta maendeleo na kufanikisha malengo mbalimbali ya vijana Tanzania,” alisema Ngaeje
Naye, akiwasilisha maazimio kwa niaba ya vijana Bi. Rabia Mussa amesema vijana wanaiomba serikali kutoa miongozo kwa halmashauri na mashirika ya umma kutangaza fursa kama vile zabuni ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo katika maeneo ya mbalimbali ili wanufaike na fursa kupitia ujuzi na ubunifu walionao katika kuanzisha shughuli za uzalishaji mali kama ilivyoainishwa kupitia mpango wa miaka mitano wa maendeleo wa taifa 2021/22 mpaka 2021/2025.
Maadhimisho ya Siku Kimataifa ya Vijana huadhimishwa kila Mwaka tarehe 12 Agosti na mwaka huu 2021 yamebeba kauli mbiu isemayo “Ubunifu na Ushiriki wa Vijana katika Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”.
AWALI: Wazo la kuwa na siku ya Kimataifa ya Vijana lilitolewa katika Mkutano wa Vijana wa Kimataifa mwaka 1991 Mjini Vienna nchini Australia. Madhumuni ya mkutano huu yalikuwa kutafuta njia ya kuchangia fedha za kusaidia Mifuko ya Taifa ya Vijana.
Mwaka 1998 wazo la kuwa na siku ya Kimataifa ya Vijana lilikubaliwa na Mkutano wa Duniani wa Mawaziri wenye dhamana na masuala ya Maendeleo ya Vijana.
Mwaka 1999 Umoja wa Mataifa (UN) ulipitisha Azimio No. 54/120 kwa kuifanya tarehe 12 Agosti ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Vijana (International Youth Day – IYD).
Mwaka 2000 nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania zilianza kuadhimisha siku hiyo kulingana na mazingira yake kwa kuzingatia kauli mbiu ambayo huandaliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU
(SERA, URATIBU, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU)
No comments:
Post a Comment