Habari za Punde

Awamu ya Sita Yazidi Kuvutia Wawekezaji

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutoa kipaumbele katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ili kuzalisha ajira.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, wakati akitoa taarifa ya wiki ya Msemaji Mkuu wa Serikali kuhusu utekelezaji wa Serikali.

"Nafurahi kuwaambia kuwa juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hususani sekta binafsi zimeendelea kuzaa matunda, uwekezaji unaendelea kufanyika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii licha ya dunia ikiwemo Tanzania kukabiliwa na changamoto zinazosababishwa na janga la ugonjwa wa Korona (Uviko- 19)” Amesema Msigwa.

Msigwa amefafanua kuwa, katika mwaka 2020/2021 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi mipya ya uwekezaji 235 ikilinganishwa na miradi 219 iliyosajiliwa mwaka 2019/2020.

Aidha, amebainisha kuwa, taarifa ya uwekezaji ya dunia ya mwaka 2020 inayotolewa na Shirika la Maendeleo na Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) imeonesha kuwa Tanzania ilipokea uwekezaji wa Dola za Marekani Bilioni 1 (sawa na shilingi Trilioni 1.235) katika mwaka huo, na hivyo kuifanya Tanzania kuongoza kwa kupata uwekezaji wenye thamani kubwa Afrika Mashariki.

Vilevile, amebainisha kuwa, katika kipindi ambacho nchi imekumbwa na wimbi la nne la Uviko- 19, kati ya Machi na Agosti, 2021 TIC imesajili miradi mipya 133 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 29,709 ikilinganishwa na miradi 105 iliyosajiliwa mwaka jana 2020 katika kipindi kama hicho ambayo imezalisha ajira 8,252.

“Thamani ya uwekezaji ulifanyika kulingana na kituo chetu cha TIC kwa kipindi cha Machi hadi Agosti mwaka huu 2021 ni Dola za Marekani Bilioni 2.98 (sawa na takribani shilingi Trilioni 7) ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana ambapo thamani ya uwekezaji ilikuwa Dola za Marekani Milioni 510 (sawa na shilingi Trilioni 1.198). Kwa hiyo uwekezaji wa mwaka huu umeongezeka kwa mara nne zaidi ya mwaka jana” amefafanua Msigwa.

Mbali na hayo, TIC imeandikisha maeneo ya ardhi yenye viwanja 273 vyenye ukubwa wa hekta 159,721 kwa ajili ya uwekezaji kutoka kwa wadau mbalimbali ambapo maeneo hayo yameandaliwa kwa ajili ya uwekezaji unaojumuisha sekta za kilimo, viwanda, mifugo, dawa za binadamu, hoteli, hospitali, makazi ya kuishi watu na huduma za kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.