Na.Issa Mzee - Maelezo 13/09/2021
Katibu Mkuu Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk, Joseph Edward Sokoine,
amesema ushiriki wa Tanzania katika Jumuiya ya nchi zilizopo kwenye mwambao wa
Bahari ya Hindi, unasaidia kikamilifu katika kuzitangaza fursa za kiuchumi
nchini.
Alitoa kauli hiyo wakati
akifungua kikao cha wadau wa nchi zilizopo kwenye mwambao wa bahari ya hindi,
kilichofanyika katika ofisi za ZURA Mjini Unguja.
Balozi Sokoine, amesema
lengo la kuweka kikao hicho ni kukuza uelewa kuhusu majukumu na ushiriki wa
Tanzania katika jumuiya hiyo, ili kuweza kuzitambua na kuzitumia fursa
mbalimbali za kiuchumi kwa maendeleo ya taifa.
Alisema malengo na
majukumu makuu ya jumuiya hiyo ni pamoja na kulinda na kuimarisha ulinzi na
usalama wa bahari, kuimarisha uwekezaji ili kukuza uchumi, kukuza na kuendeleza
sekta ya utalii na utamaduni.
Pia, kukabiliana na
majanga hususan kwenye ukanda wa bahari ya hindi, kuendeleza na kuimarisha ushirikiano
katika uchumi wa buluu pamoja na kuimarisha sekta ya uvuvi hasa kwenye eneo la
bahari kuu.
Katika kutekeleza
majukumu hayo, Dk. Sokoine alisema jumuiya imeunda vikundi kazi ili kufanikisha
na kutekeleza majukumu mbalimbali katika jumuiya hiyo.
Alifafanuwa kuwa,
vikundi kazi hivyo ni vyema vizingatie ushiriki wa pande zote mbili za Tanzania
Bara na Zanzibar ili kuhakikisha ufanisi unapatikana katika kutekeleza
majukumu.
Aidha, aliwataka wadau kutoa msukumo na kuzipa kipaumbele shughuli
zinazoratibiwa na jumuiya hiyo, ili kujua yanayojiri kwa lengo la kulinda kwa
vitendo maslahi ya Tanzania.
Alieleza kuwa uanachama
wa Tanzania katika jumuiya hiyo ni muhimu katika kuimarisha uhusiano na mataifa
mbalimbali duniani ambao unatoa fursa ya
kubadilishana uzoefu na kuibua changamoto za maendeleo.
Alisema mada
zilizoandaliwa katika kikao hicho zina umuhimu mkubwa na kuleta dira na muongozo katika kutangaza
fursa na rasilimali zilizopo kwenye
ukanda wa bahari ya Hindi.
Vilevile aliwataka
wajumbe hao kutoa mapendekezo yatakayowezesha utekelezaji wa masuala mbalimbali
ya uchumi wa buluu na uhifadhi wa mazingira.
Aidha, Dk, Sokoine aliwataka
wajumbe hao kuomba ufadhili wa miradi ya maendeleo ambayo italenga zaidi katika
uhifadhi wa mazingira pamoja na uvunaji
endelevu wa rasilimali za bahari kwa maslahi ya Tanzania.
Mapema Mkurugenzi Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki Zanzibar, Balozi Masoud Abdalla, alisema utekelezaji wa sera ya mambo
ya nje kwa njia ya amani ni jambo muhimu hasa katika kujadili faida na fursa za
bahari ya Hindi.
Alifahamisha kuwa, njia
ya amani husaidia katika kuimarisha uhusiano wa kimataifa ambao huleta faida
kubwa za kiuchumi ikiwemo muingiliano wa biashara.
Akizungumza kuhusu
uchumi wa buluu, Mkurugenzi huyo alisema sera ya uchumi wa buluu ina nyenzo kuu
tano ikiwemo utalii wa bahari, kilimo cha mwani, bandari, gesi na mafuta pamoja
na uvuvi.
Hata hivyo alisema
umefika wakati wa kutekeleza kwa vitendo sera ya Rais wa Zanzibar, katika
uchumi wa buluu ili kuleta maendeleo nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Idara ya Ushirikiano wa kikanda, Balozi Agnes Richard Kayola, amesema umefika
wakati kwa Tanzania wa kuzitazama vyema fursa zilizopo katika mwambao wa Bahari
ya Hindi, ili zitumike kwa maendeleo ya taifa.
Amefahamisha kuwa, Jumuiya
ya nchi zilizopo kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi inaundwa na Nchi 23 ikiwemo Tanzania.
Alisema tangu kuanzishwa
kwa jumuiya hiyo, Tanzania haijawahi kugombea nafasi ya Katibu Mkuu, hivyo umefika wakati kwa
Tanzania kugombea nafasi hiyo.
Alisema kuwa, uimarishwaji
wa ushiriki wa Tanzania katika jumuiya hiyo ni muhimu kwa maslahi mapana ya
nchi ambao pia utasaidia katika kukuza uchumi wa bahari nchini.
Aliongeza kuwa, uimarishwaji
wa vikundi kazi katika jumuiya hiyo
visivyopungua nane, ikiwemo kikundi cha uvuvi, ni jambo muhimu katika
kuimarisha utendaji na kuviunda upya vikundi visivyofanya kazi vizuri ni jambo
la msingi.
Alisema kikao hicho cha
siku tatu kinalengo la kuimarisha ushiriki wa Tanzania kwenye jumuiya ya nchi
zilizopo kwenye mwambao wa bahari ya Hindi.
Katika kufanikisha hilo,
Balozi Kayola amesema ushirikiano wa kisekta baina ya pande mbili kati ya
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni muhimu pia ni wa kuendelezwa.
Katika kikao hicho mada
mbalimbali zilijadiliwa, ikiwemo uchumi wa buluu na tija zake katika maendeleo
ya taifa, uhifadhi wa mazingira na mchango wake katika uchumi wa buluu, Uvuvi
katika bahari kuu, pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo kwenye ukanda wa
bahari kuu na Mazao ya Baharini.
No comments:
Post a Comment