Na.Kassim Abdi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyataka mabaraza na Jumuiya za uhifadhi na uwendelezaji Mji Mkongwe kuendelea kutoa Hamasa kwa wakaazi na wageni wanaotembelea Mji huo ili kujega utamaduni wa kutumia usafiri wa Baiskeli badala ya vyombo vya moto kwa lengo la kuendelea kuhifadhi mji huo.
Mhe. Hemed alieleza hayo katika mapokezi maalum ya matembezi ya usafiri wa baiskeli yaliyofanyika katika bustani ya Forodhani ambapo yeye binafsi alishiriki kwa kuendesha baiskeli kuanzia ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil na kumalizia katika eneo la bustani ya Forodhani.
Alieleza kuwa, kampeni ya kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya matumizi ya baiskeli katika eneo la Mji Mkongwe itasaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi na kuendeleza mji huo na kupunguza athari mbali mbali za kimazingira.
Alisema kitendo cha utumiaji wa usafiri wa baiskeli mbali na kupunguza athari katika mitaa ya mji huo wa kale lakini pia kutasaidia kuimarisha afya za watu ikiwa utumiaji wa usafiri wa baiskeli kuwa sehemu moja wapo ya kufanya mazoezi.
Makamu wa Pili wa Rais alisema katika kukabiliana na changamoto hio Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbali mbali za kupunguza uingiaji holela wa vyombo vya moto wa kutunga sheria na kanuni za usafiri zinazodhibiti uingiaji wa vyombo vya moto pamoja na kuhamasisha matumizi ya usafiri mbadala.
“Tumekuwa tukihamasisha wananhchi kutumia usafiri mbadala ikiwemo matumizi ya usafiri baiskeli ili kukabliana na changamoto ‘’ Alisema Makamu wa Pili wa Rais.
Mhe. Hemed aliendelea kufafanua kwamba, katika kukabiliana na changamoto serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbali mbali kwa kuweka miundombinu rafiki ya kuwawezesha wananchi kutembea kwa miguu na kutumia baiskeli katika mitaa ya Mji Mkongwe.
‘”Sambamba na yote Serikali imekuwa ikishirikiana na Jumuiya za kiraia za ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha kuwa tunapunguza matumizi ya vyombo vya moto ili kuunusuru mji wetu usiendelee kuharibika’’ Alifafanua Mhe. Hemed.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Kaimu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Suleiman Masoud Makame ambae pia ni Waziri wa Maji Nishati na Madini alisema kuna umuhimu mkubwa kwa viongozi kuweka utaratibu maalumu wa kutembea kwa baiskeli ili kutoa hamasa kwa wananchi kutumia usafiri huo.
Aidha, Mhe suleiman alisema kutembea kwa baiskeli katika jiji la Zanzibar ni ishara tosha ya kuwepo kwa amani na utulivu ndani ya Zanzibar, ambapo jambo hilo linawapa fursa wageni kuja kwa wingi kuitembelea Zanzibar.
Nae Mkurugenzi wa tamasha la Nyama choma ambe pia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Mjini Ndugu Abdulrahim Hamid alisema kufanyika kwa matembezi hayo kuna lenga kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais za kuwinua Mji Mkongwe na kuimarisha utalii kupitia uchumi wa buluu.
Alieleza kuwa, vyombo vya moto vimekuwa vikisababisha athari kubwa kutokana na vishindo vinavyopelekea kuharibika kwa majengo.
Alisema kupitia kundi hilo la vijana wamekusudia kufanya tamasha hilo kuwa endelevu ili kuongeza idadi ya matamasha kwani kufanya hivyo kutapelekea kuongezeka kwa fursa za ajira kwa vijana .
Mji Mkongwe wa Zanzibar una jumla ya hekta Tisini na sita (96 ) ambapo umekuwa maarufu kwa shughuli za kitalii na ni moja ya miji uliokuwemo katika uhifadhi na urithi wa kimataifa.
Kassim Abdi
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
04/09/2021.
No comments:
Post a Comment