Habari za Punde

Dk Shein aridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya CCM Wilaya ya Amani

MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wa Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Magharibi Kichama ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk.Ali Mohamed SheIn, akizungumza na Wana CCM mara baadae ya kupandisha Bendera katika Shina namba mbili Tawi la CCM Mpendae Juu.
MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Mjini Kichama akiweka Jiwe la Msingi katika Maskani ya Wazee ya 'Umaskini haukuletwa na CCM' iliyopo Jimbo la Amani Zanzibar.

MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Magharibi  Kichama Dk.Ali Mohamed Shein aliangalia bidhaa ya Chili zinazotengenezwa na Kikundi cha Hamasa Cha UVCCM Tawi la CCM Kwa Wazee Zanzibar.


MLEZI wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Magharibi  Kichama Dk. Ali Mohamed Shein akipandisha Bendera ya CCM katika Shina namba 2 Tawi la CCM Mpendae Juu Zanzibar. (PICHA NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR)

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR

MLEZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mjini na Mkoa wa Magharibi Kichama Dk.Ali Mohamed Shein, ameelezea kuridhishwa kwake na utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Wilaya ya Amani.

Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha na kukagua utekelezaji wa Ilani ndani ya Chama, huko katika Tawi la CCM Kwa Wazee Unguja, alisema viongozi na wanachama ndani ya Wilaya ya Amani wamefanya kazi kubwa ya kuimarisha Chama Kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Dk.Shein, ameeleza kwamba maeneo mbalimbali aliyoyatembelea na kukagua ameona miradi mbalimbali ya maendeleo inayotatua changamoto za Wananchi wa maeneo husika.

Alisema miradi inayotekelezwa ikiwemo ya upatikanaji wa Maji safi na salama, Vikundi vya Ujasiriamali, ujenzi wa Maskani za Kisasa za CCM na uendelezaji wa Madara ya Itikadi, Mafunzo na Elimu yote ni miongoni mwa mikakati endelevu ya kuimarisha Chama na wanachama kujitegemea wenyewe kiuchumi.

Alipongeza Wabunge, Wawakilishi na Madiwani wanaoshiriki kutekeleza miradi hiyo kwani ni sehemu yao utekelezaji wa Ahadi walizotoa kwa Wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita.

"Nimepewa jukumu na CCM niwe Mlezi wenu na nimekuja hapa kujitambulisha nimeanza Kwa ngazi za chini kabisa za matawi na mashina, walipo Wanachama wetu ambao ndio chimbuko na uimara wa Chama.

Toka nimeanza ziara hii nimeshiriki shughuli mbalimbali za maendeleo katika Matawi na Mashina, hali inayoonyesha utekelezaji wa Ilani yetu kwa vitendo,hakika Chama kinaendelea kuwa imara zaidi.", alisema Dk.Shein.

Alisema Serikali ya Zanzibar kwa awamu mbalimbali zimekuwa zikitekeleza miradi ya upatikanaji wa huduma za Maji safi na salama ili kuhakikisha changamoto hiyo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Katika maelezo yake Dk.Shein, aliwasihi wanachama kununua bidhaa zinazotengenezwa na vikundi vya Ujasiriamali vinavyoanzishwa na wanachama ili mitaji yao ikue na wajitegemee wenyewe.

Akizungumza katika Maskani ya shukrani iliyopo Jimbo la Chumbuni alisema Maskani zilizozinduliwa zitumike kufanyakazi za Chama Kwa kuongeza zaidi wanachama wapya.

Alisema viongozi wa CCM waendelee kufanya kazi za kisiasa Kwa kuwa mfano bora wa kusema na kuonyesha maendeleo Kwa vitendo ili Wananchi walio nje ya Chama wavutiwe na Sera za CCM na kujiunga na Chama kwa wingi.

Dk.Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema katika juhudi za kuimarisha Chama ni lazima wanachama walipe Ada Kwa wakati.

Alisisitiza wanachama kuendelea kupendana na kuheshimiana kwani Chama hakiwezi kujengwa Kwa kuchukiana.

"Waasisi wetu katika harakati za ukombozi walipenda,kushirikiana na kuchangishana michango mbalimbali Kwa hiari ndio maana walifanikiwa kufanya Mapinduzi ya Januari 12, mwaka 1964". Alisisitiza Dk.Shein.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Juma Abdulla Mabodi, alisema ziara hiyo ni miongoni mwa maelekezo ya Kamati Kuu ya CCM ya kuhakikisha Viongozi wanashuka kutembelea  ngazi za matawi na mashina kwa lengo la kuimarisha Chama.

"Tunaamini Wana CCM mnafanya kazi kubwa na iliyotukuka katika maeneo yenu na ndio maana viongozi wenu wamekuja katika maeneo yenu kukaa nanyi Kwa lengo la kubadilishana mawazo na kujionea wenyewe changamoto na mafanikio yaliyofikiwa", alisema Dk.Mabodi.

Kwa upande wake Balozi wa Shina namba 2 katika Tawi la CCM Mpendae Juu Khadija Hassan Salmin, alikishukuru Chama kwa kuisimamia vizuri Serikali iliyotekeleza vizuri mradi wa ujenzi wa mtaro mkubwa wa kupitisha Maji ya mvua na kutatua kero ya mafuriko kwa Wananchi wa Jimbo la Mpendae na maeneo jirani.

Aidha alikiomba Chama kuanzisha utaratibu wa kuwalipa posho Mabalozi wa mashina kwani nao wanafanya kazi kubwa ya kukijenga Chama, hivyo fedha hizo zitawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika ziara hiyo Katibu wa Ushirika wa 'Uvivu hauna Maendeleo' Kilichopo Kilimahewa Bondeni, Mtende  Jirani Mtende alisema kikundi kinachotengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo ususi wa mikeka, mikoba na ushoni wa nguo niwanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Soko, ukosefu wa Ofisi ya kudumu, mikopo nafuu na ukosefu wa Elimu ya Ujasiriamali.

Katika ziara hiyo Dk.Shein alitembelea maeneo mbalimbali yakiwemo kupandisha bendera Shina namba mbili Mpendae Juu, kumtembelea mwasisi wa Chama Ali Omar Ali (Chengo), kuweka jiwe la msingi Maskani ya Wazee ya 'Umaskini haukuletwa na CCM', kuangalia Mradi wa Pilipili 'Hamasa Chill', ametembelea kikundi Cha 'Uvuvi hauna Tija, ametoa kadi za uanachama kwa wanachama na Jumuiya.

Nyengine ni uzinduzi wa mradi wa Maji safi na salama uliopo Shehia ya Kwa Wazee, kuweka jiwe la msingi katika uwanja wa mpira wa Kivumbi na kuzindua Darasa la Itikadi na kutoa kadi za CCM Kwa wanachama wapya Jimbo la Shauri Moyo 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.