Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amejumuika na Wananchi wa Mkwajuni Kidombo Katika Dua Maalum.

 
Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi leo amewaongoza Waumini wa dini ya Kiislamu katika dua maalum ya Hitma iliyosomwa huko katika Msikiti wa Ijumaa, Mkwajuni Kidombo, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Dua hiyo inayokwenda sambamba na Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) ni utamaduni wa muda mrefu uliowekwa na wakaazi wa Kijiji hicho ambapo kila ifikapo mwezi kama huu wa Mfunguo Sita hufanyika hafla hiyo ambayo huwakusanya wanakijiji wa eneo hilo pamoja na wale wa maeneo jirani wakiwemo wenye asili ya Kijiji hicho wanaoishi Mjini kwa ajili ya dua na Maulid hayo.

Katika dua hiyo iliyosomwa katika Msikiti wa Ijumaa Mkwajuni Kidombo, viongozi mbali mbali wa dini, vyama vya siasa na Serikali pamoja na wananchi walihudhuria akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaj Ali Hassan Mwinyi pamoja na viongozi wengine wakiwemo wastaafu.

Mapema akisoma hotuba ya Ijumaa Sheikh Mussa Haji Makame alieleza dhamira ya Mwenyezi Mungu kumleta duniani Mtume Muhammad (S.A.W) ikiwa ni  kuja kubainisha haki na kukataza maovu sambamba na kuufunza umma namna ya kuzitekeleza haki hizo pamoja na malipo yake.  

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na viongozi wengine kwenda kumsalimia na kumjuulia hali Rais wa Zanzibar Mstaafu wa Awamu ya Tano Alhaj Dk. Salmin Amour Juma hapo nyumbani kwake kijijini kwao Mkwajuni Kidombo.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.