Na Kassim Issa, OMPR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk Hussein Ali Mwinyi amesema SMZ itaendelea kushirikiana na Chama cha Walimu Zanzibar katika kutunga sera, sheria na utekelezaji wa mipango na mikakati kwa lengo la kuimarisha sekta ya Elimu Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo kupitia hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Rais Dk. Mwinyi katika Maadhimisho ya Siku ya walimu Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya kufurahishia watoto Tibirinzi Wilaya ya Chakechake Kisiwani Pemba.
Alisema Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) ni kiungo muhimu kinachofanya kazi ya kutetea maslahi ya walimu pamoja na kuwahimiza kutekeleza vyema majukumu yao kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais alisema katika kuunga mkono jitihada hizo serikali itaendelea kuthamini jitihada na kazi kubwa inayofanywa na walimu kwa kuendelea kuwaanda vijana kitaaluma kwa kuwapa maarifa na malezi bora licha ya kukabiliwa na changamoto mbali mbali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha,Mhe. Hemed aliendelea kutoa wito kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na chama cha walimu Zanzibar (ZATU) kwa kuwa na vikao vya majadiliano na uhusiano mwema ili kuondokana na malalamiko ya Chama hicho kwa kuzitatua changamoto zinazowakabili.
Akizungumzia maslahi ya walimu Mhe. Hemed alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga katika kuwapataia stahiki zao walimu pamoja na walimu wakuu na kuwataka kuendelea kuwa wavumilivu wakati Serikali ikilishughulikia suala hilo.
Katika maadhimisho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitumia fursa hiyo kuwaasa wazazi na walezi kuenelea kutoa mashirikiano katika suala la malezi ili kupunguza matendo ya udhalilishaji na unyanyasaji wa watoto ili kurudisha heshima na malezi bora kwa wanafunzi.
Akigusia suala la kukuza ufaulu Zanzibar Mhe. Hemed aliiagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na uongozi wa Mikoa na Wilaya zote katika kuandaa mipango madhubuti ya kuhakikisha Skuli zilizomo katika maeneo yao zinakuwa na mikakati maalum ya kuongeza kiwango kizuri cha ufaulu.
Kuhusu suala la ajira kwa walimu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema Serikali inajiandaa kutoa ajira za ualimu hasa kwa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu lililomo katika Skuli mbali mbali nchini.
Katika kufanikisha hilo aliuagiza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuharakisha kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya walimu wa ngazi mbali mbali za elimu huku kutoa kipaumbele maalum kwa walimu wanaofundisha kwa njia ya kujitolea ili kuwapa moyo na kuonesha nia njema ya Serikali katika kuthamini uamuzi wao huo wa kizalendo.
Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Simai Muhamed Said alisema wizara anayoisimamia inatambua thamani ya walimu katika kuhakikisha inawaanda wanafunzi kuwa na tabia njema kwa ajili ya kulitumikia taifa hivyo aliwathibitishia walimu hao kuwa uongozi Wizara utaendelea kuthamini jitihada za walimu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Waziri Simai alieleza kwamba, walimu wanapaswa kuzingatia muungozo wa kuwarekebisha tabia wanafunzi ili kuwakuza wanafunzi hao kinidhamu kwa lengo la kuongeza ufaulu na kuandaa watendaji bora kwa Taifa la sasa na baadae.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Walimu Zanzibar (ZATU) Mwalimu Seif Muhamed Seif alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa, ZATU inaipongeza serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais Dk. Mwinyi kwa kuendeleza utawala wa sheria katika uwajibikaji.
Aidha, Alisema Chama cha walimu Zanzibar kinaiunga mkono serikali katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na kueleza kuwa wanafunzi ndio wahanga wakubwa wa vitendo hivyo jambo linapolekea kuwaathiri kisaikolojia.
Maadhimisho ya Walimu duniani huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 05, ya kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu "MWALIMU ONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA UDHALILISHAJI WA WATOTO".
No comments:
Post a Comment