Habari za Punde

Michuano ya Ligi Kuu ya Zanzibar Pbz Premier League.

Na Mwajuma Juma

TIMU ya soka ya Black Sailor juzi iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande wa Polisi katika mchezo uliochezwa uwanja wa Amaan.

Mchezo huo ambao ulipigwa majira ya saa 10:00 za jioni ulikuwa na ushindani mkali huku Black Sailor ikiandika bao lao hilo la pekee dakika ya 10 tu kuanza kwa mchezo huo.

Bao hilo ambalo liliwafikisha pointi 12 na kuwa nafasi ya nne ya msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na KMKM wenye pointi 16 lilifungwa na Bonifas Kaheke.

Aidha katika uwanja huo majira ya saa 1:00 usiku Malindi ilishuka kuumana na wapinzani wao wa jadi timu ya Mlandege ambao waliwafunga mabao 2-0.

Katika uwanja wa Mao Zedong Kipanga iliwafunga Mafunzo mabao 3-0, wakati huko kisiwani Pemba wakati wa saa 8:00 KMKM waliocheza uwanja wa Gombani iliwafunga Kisiwani mabao 4-1 na saa 10:00 za jioni uwanjani hapo Machomane na Selem View walitoka sare tasa.

Kwa mujibu wa msimamo wa ligi hiyo nafasi ya pili inashikiliwa na Malindi wenye Pointi 14 wakati Zimamoto inashika nafasi ya tatu pointi 12 sawa na Black Sailor ambao wapo wanne wakiwazidi kwa idadi ya magoli ya kufunga na kushinda.

Nafasi ya tano inashikiliwa na Taifa ya Jang’ombe wenye pointi 11 sawa na KVZ ambao waliwazidi kwa idadi ya magoli ya kushinda, wakati Mlandege  inashika nafasi ya saba pointi 10, Mafunzo wapo nafasi ya nane pointi tisa na Kipanga inashika nafasi ya tisa point inane.

Nafasi ya 10 kwa mujibu wa msimamo huo inashikiliwa na JKU wenye pointi saba sawa na Uhamiaji wakishindana kwa magoli ya kushinda na kufungwa na Polisi wapo wa 12 wenye pointi tano.

Timu ambazo zipo katika mstari mwekundu kwenye msimamo wa ligi hiyo ni Selem Vioew wenye pointi tano nafasi ya 13, Yoso Boys nafasi ya 14 pointi nne, Machomanne ya 15 pointi moja na Kisiwani inashika mkia ikiwa haina pointi hata moja.

Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena Jumatatu ya Novemba 22, mwaka

huu, ambapo katika uwanja wa Gombani Pemba Taifa ya Jang’ombe itacheza

na Selem View saa 8:00 mchana na saa 10:00 Yoso Boys itacheza na KMKM,

wakati saa 10:00 katika uwanja wa Mao Zedong Black Sailor itacheza na

Malindi na katika uwanja wa Amaan Kipanga itacheza na JKU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.