RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi amesema Serikali
inatumia nguvu zote kuongeza fedha
kwenye sekta za kiuchumi, hivyo amewataka atendaji wote watakaokabidhiwa
dhamana ya kusimamia fedha hizo kuwa wakweli na waaminifu ili ziweze kuwafikia
wananchi wote waliolengwa
Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika salamu zake kwa waumini wa Dini ya Kiislamu waliojumuika pamoja katika Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Arafaa, Mombasa jijini hapa.
Amesema kudorora kwa uchumi wa Zanzibar kulikotokana na ugonjwa wa Uviko 19, kumeifanya Serikali kuchukua kila hatua ikiwemo kutafuta mikopo ili kupata fedha kwa lengo la kupunguza makali ya ugumu wa maisha yanayowakabili wananchi, baada ya kuathirika kwa sekta mbali mbali, hususan sekta ya Utalii.
Alisema Zanzibar imejaaliwa kuwa na neema ya kuwa na amani , umoja na mshikamano, hivyo kuna haja ya kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa msingi kuwa mambo hayo ndio msingi wa maendeleo.
Alisema kila mmoja sehemu alipo,hususan kwa watendaji wa taasisi zinazotoa huduma kufahamu jukumu alilonalola kuhakikisha anakuwa mkweli na muaminifu
“Kila mmoja sehemu alipo awajibike na kumuomba Mwenyezi Mungu li tuweze kufanikiwa”, alisema.
Mapema, Katibu wa Mufiti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume, aliwaomba waumini hao kumuombea dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Mwinyi ili aweze kutekeleza malengo yake na kubainisha neema kubwa iliobarikiwa Zanzibar kwa kuwa na kiongozi mkweli, muaminifu na mwenye kusononeshwa na shida za wananchi wake.
Nae, Khatibu katika Sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Ali Yunus, aliwataka waumini wanaopewa dhamana katika taasisi zinazototoa huduma kuwa wakweli na waaminifu, kama kigezo cha kumfuata Mtume Muhammad (SAW).
Aliwakumbusha waumini hao wajibu wa kupendana, kuoneana huruma pamoja na kufanyiana wepesi katika maisha.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ya Zanzibar Alhaj Dk. Mwinyi ,alipata nafasi ya kufika nyumbani kwa Rais Mstaafu wa Zanzibar Awamu saba Alhaj Dk. Ali Mohammed Shein, na kutoa mkono wa pole kutokana na kifo cha kaka yake Shein Mohamed Shein, aliefariki dunia mapema wiki hii.
Aidha, Alhaj Mwinyi alifika nyumbani kwa Mwanasiasa mkongwe hapa nchini, Thereza Alban Ali na kumpa mkono wa pole kutokana na kifo cha mtoto wake kilichotokea hivi karibuni.
Kitengo cha habari,
Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment