Habari za Punde

UWT waandaa mkutano wa kumpongeza Mhe Rais Samia

NAIBU Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Tunu Juma Kondo(Kushoto) akiwa na Katibu wa NEC,Idara ya Organazesheni Taifa Moudline Cyrus Castico(Kulia) wakizungumzia maandalizi ya Mkutano wa UWT wa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe.Samia Suluhu Hassan utakaofanyika Novemba 20,mwaka huu katika Viwanja vya Maisara Zanzibar, 


 NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

UMOJA wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (U.W.T) Zanzibar,  umesema unajivunia kuwa na Rais wa kwanza mwanamke wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan  ambaye ametimiza ndoto za Umoja huo katika nyanja za Kiuchumi,Kijamii,Kisiasa na Kidiplomasia.

Kauli hiyo ameitoa Naibu Katibu Mkuu wa U.W.T Zanzibar  Tunu Juma Kondo katika mahojiano Maalum juu maandalizi ya mkutano wa kumpongeza Rais Mhe.Samia ulioandaliwa na Umoja huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 20, mwaka huu katika Viwanja vya Maisara Mjini Zanzibar.

Alisema tangu kuanzishwa kwa UWT waasisi wake walikuwa wakipigania nafasi na haki mbalimbali za kumwezesha Mwanamke kushika nafasi za juu katika masuala ya uongozi na utawala ndoto ambazo zimetimia hivi karibuni baada ya kupatikana Rais wa kwanza mwanamke ambaye ni zao la umoja huo.

Tunu,alieleza kuwa si tu wanajivunia kuwa na Rais mwanamke bali wanaona fahari ya kuwa na kiongozi   mchapakazi, mwadilifu, mbunifu, mzalendo na mwadilifu.

Alisema miaka mingi iliyopita wanawake hawakuwa na nafasi hata ya kupiga kura lakini hivi sasa wanawake wamepiga hatua kubwa ya kimaendeleo kwa kuwa viongozi na watendaji katika sekta zote.

“ Zamani wanawake tulipata ugumu hata wa kupata nafasi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi lakini hivi sasa tunamshukru Mungu tumepata Rais mwanamke na tunampongeza kwa utendaji wake hasa kutetea na kusimamia haki za wananchi wa makundi yote.”, alisema Tunu.

Naibu Katibu Mkuu huyo Tunu, alisema lengo la mkutano huo ni kumpongeza Rais Samia kwa utendaji wake uliotukuka kwa kipindi cha miezi sita tangu ashike madaraka.

Katika maelezo yake Tunu alimtaja  kiongozi huyo kuwa amekuwa na kasi kubwa kiutendaji katika masuala ya kiuchumi,kijamii,kisiasa na kuendeleza mahusiano ya Kimataifa yanayotoa fursa mbalimbali za kuinua uchumi wa Tanzania.

Akizungumzia ratiba ya mkutano huo alisema mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe.Samia Suluhu Hassan ataungana na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali.  

Tunu amefafanua kwamba viwanja vya Maisara vitafunguliwa kuanzia saa 12:00 asubuhi na wananchi wataanza kuwasili uwanjani kuanzia saa 1:00 asubuhi ambapo mkutano huo unatarajiwa kumaliza saa 8:00 mchana.

Aliwasihi Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na Wananchi kwa ujumla kufika mapema ili kusikiliza sera na maelekezo ya Rais Samia ambaye ni mara ya kwanza kuja Zanzibar kuzungumza na Wana CCM toka ashike madaraka.

Naibu Katibu Mkuu huyo alisema katika maandalizi ya mkutano huo wamechukua tahadhari ya kuwakinga wananchi  na maradhi ya UVIKO-19 kwa kuweka vitakasa mikono na kuwasihi kuvaa barakoa.

Alisema pia itakuwepo huduma ya kuchanja chanjo ya UVIKO-19 kwa hiari kwa wananchi mbalimbali watakaohitaji huduma hiyo.

Kwa upande wake Katibu wa NEC, Idara ya Organazesheni Moudline Cyrus Castico, alisema Rais Samia ameonyesha uwezo wa asili wa mwanamke ambaye anapokuwa katika ngazi ya familia anakuwa ni kiungo muhimu sana hivyo wana matumaini makubwa ataendelea kufanya mageuzi makubwa ya kimaendeleo.

Alieleza kuwa Rais huyo ameiheshimisha Tanzania kimataifa kutokana na juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo.

Castico alisema amani imeendelea kutawala huku Serikali zote mbili zikiendelea kushirikiana kwa karibu katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Alieleza kuwa utendaji wa Rais Samia, ulianza kuonekana toka serikali iliyopita alivyokuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alivyokuwa akifanya kazi na kushauriana vizuri na hayati Rais Magufuli.

“Ndio maana miradi yote iliyoachwa na awamu ya Serikali iliyopita hivi sasa Rais Samia ameiendeleza kwa kasi kubwa hali inayoonyesha kwamba wanawake wakipewa nafasi wanaweza kuonyesha miujiza mikubwa ya kiutendaji.”, alisema Castico.

Castico ambaye pia idara yake ndio Mlezi wa Jumuiya zote za CCM, alisema wamejiandaa vizuri kumpokea Rais Mhe.Samia visiwani Zanzibar.

Akitoa ushuhuda wake juu ya chanjo ya UVIKO-19 Katibu huyo wa NEC Castico, alieleza kuwa chanjo hiyo haina madhara kama baadhi wanavyopotosha kwani yeye pia amechanja na mpaka sasa anaendelea kufanya kazi zake kwa ufanisi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.