Habari za Punde

Walimu Wapatiwa Stadi ya Maisha ya VVU na Ukimwi

Na Maulid Yussuf WEMA. ZANZIBAR.

Shirika la Kimataifa la Elimu na  Sayansi UNESCO kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wametoa Elimu ya Stadi za Maisha, VVU na UKIMWI pamoja na elimu ya Afya ya Uzazi kwa Walimu.

Amesema lengo ni kuwafundisha Wanafunzi wao ili waweze kupata elimu hiyo na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maisha yao ya kila siku na kupata taaluma ya kina  juu ya masuala ya stadi za maisha, VVU na UKIMWI pamoja na Elimu ya Afya.

Hayo yameelezwa na Afisa Ukimwi Afya ya Uzazi, dawa za kulevya kutoka Kitengo cha Elimu Mjumuisho na Stadi za Maisha bi Riziki Mohammed Juma, wakati wa warsha  ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Takwimu juu ya muitiko na upimaji wa viashiria vya kimataifa vya Elimu ya UKIMWI Afya ya Uzazi, stadi za maisha,  na Jinsia katika nyanja ya Elimu, katika Ukumbi wa Kituo cha Walimu TC Kiembesamaki Mjini Unguja.

Amesema kupitia mafunzo hayo, Serikali imetumia gharama kubwa, hivyo ni wajibu wao Watakwimu kuhakikisha wanafanya uhakiki wa kukusanya taarifa ili kuona kwa namna gani mafunzo hayo yameweza kuwasilishwa kwa Wanafunzi kama ilivyo kusudiwa.

Amesema tayari pamoja na masomo hayo kusomeshwa baadhi ya walimu wa Skuli, pia Walimu wa Ushuri pamoja na na Walimu wa Klabu za Afya nao wameshapatiwa kwa lengo pia la kusaidia katika jamii kutoa elimu hiyo kwa watoto.

Amefahamisha kuwa hivi sasa  Wizara ya Elimu inakamilisha utaratibu wa kuyaingiza masomo hayo katika mtaala wa Elimu ili kuweza kufundishwa kwa uhakika masomo hayo katika Skuli kuanzia ngazi ya maandalizi ili kuwasaidia watoto kuweza kujitambua na kuweza kukabiliana na masuala hayo wakati yatakapowakuta.

Nao watakwimu hao wamesema, moja kati ya kazi zao ni kuhakiki taarifa ili kuisidia Serikali kuweza kupanga mipango yake mbali mbali, hivyo wameahidi kuifanya kazi hiyo ili malengo yaliyowekwa yaweze kufikiwa.

Warsha hiyo ya siku tatu imewashirikisha Maafisa wa Takwimu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Maafisa Elimu wa Wilaya na Maafisa Takwimu Elimu wa Wilaya, imendaliwa na UNESCO kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu  kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Sweeden SIDA.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.