Habari za Punde

Wananchi Mkoani Tanga Watakiwa Kuepuka Kuvamia Maeneo Yanayomilikiwa na Serikali.

Mkuu w Mkoa wa Tanga Adamu Malima katikati akizungumza na Wawakilishi kutoka Benki ya Dunia na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kujadili uboreshaji wa kiwanja cha ndege cha Tanga ikiwa ni pamoja na kuwahamisha wananchi waliovamia eneo hilo.


Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WANANCHI Mkoani Tanga wameaswa kuepuka kuvamia na kujimilikisha maeneo yanayomilikiwa na serikali kisheria ili kuepusha migogoro isiyo na tija na badala yake kufanya uzalishaji mali kwa njia ya halali ambao utaleta maendeleo mapana ndani ya Mkoa na wananchi wake.

Hayo yalibainishwa na mkuu wa Mkoa wa Tanga Adamu Malima wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya kutembelewa na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia (WB) pamoja na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kujadili namna watakavyoshiriki katika ujenzi wa kiwanja cha ndege mkoani humo.

Malima alibainisha kwamba wapo watu wenye tabia za kuvamia maeneo ya serikali na kufanya makazi yao ya kudumu jambo ambalo huleta migogoro kati yao pindi serikali itakapoamua kufanya matuminzi katika maeneo hayo ambayo inayamiliki kisheria.

"Na tabia hii nimeiona kuna watu wanavamia maeneo ya shule, niwaombe kama eneo limetengwa kwa ajili ya shule usiingie, nitakutoa tu na baadaye tutatengeneza mgogoro usio na sababu, mimi ninafikiria kwamba wakati umefika sasa tujipange na tuwe wachangiaji wa maendeleo kwa jitihada za kazi tunazofanya" alisema.

"Na tujichunge sana na hawa watu ambao wanapiga ardhi halafu mnaenda mahakamani, hapana ebu amka kwanza uwe mzalishaji mali au mashamba au biashara na hata uwekezaji kitu ambacho kinachangia kwenye maendeleo mapana ya Mkoa wa Tanga ili tuondokane na hapa tupipokuwa na twende kwenye ngazi za juu ambazo Tanga ndipo tulipokuwa" alisisitiza.

Aidha Malima alisema serikali imeamua kuboresha kiwanja cha ndege cha Tanga hivyo wale wote waliovamia na kujenga eneo hilo wanapaswa kujua kwamba walivamia pamoja na kwamba wamejenga na kuishi hapo lakini hawako kisheria hivyo kuwasihi wawe wapole pindi serikali itakapochukua hatua ya kuanza ujenzi ili wapatiwe maeneo mbadala.

"Nataka niwasihi Wanatanga wenzangu kwamba, Tanga tuna migogoro ya ardhi ambayo inakuwa mingi mno na haina tija, kwahiyo tunakaa maeneo ambayo siyo yet, lakini nawaomba pia wajue kwamba mtu alivamia akakaa akajenga, siyo kwamba ana haki napo, hapana hana haki napo bado kama ni eneo la serikali basi litabaki kuwa eneo la serikali" alisema.

"Kwahiyo tutakapokuja kwa lengo la kuchukua katua katika eneo ulilovamia, ushauri wangu ni kwamba uje kwa upole na sisi tuje kwa upole ili tufike sehemu tukusaidie namna ya kuondoka pale na kutafuta sehemu nyingine, lakini uwe mwangalifu na watu hasa wanasheria vishoka ambao wanakuja na kumiambia tutaipeleka serikali mahakamani, utaipelekaje serikali mahakamani kwa kitu ambacho ni mali ya serikali, vitu vya ajabu kabisa" aliongeza.

"Tumeongea na watu wa Benki ya Dunia na Wizara kuona jinsi ya kufanya pale, tumeangalia na tumeona eneo lile lisiwe kikwazo kwa wananchi wa Mkoa wa Tanga, watu walioko pale wasiwe kikwazo kwa maendeleo ya Mkoa wa Tanga" alieleza Malima.

"Kwahiyo tumewaomba waende wakaangalie kama lile eneo watu walilovamia kama linaweza kuzuia ujenzi wa kiwanja kile ambacho ni mahitaji kwa ajili ya Wanatanga wote, ni uwekezaji kwa Wanatanga wote sasa kwanini uzuiliwe na watu 60,70 ambao wamevamia na sasa wanafanya makusudi" alifafanua

Hata hivyo mkuu huyo alibainisha kwamba mambo ya uvamizi wa ardhi yanahitaji kukemewa  kwani wananchi wengi wamefanya mazoea kwakuwa wanaona serikali haichukui hatua pindi wanapoamua utaratibu wao wa kuvamia maeneo na kugawana ili kuishi.

"Kwahiyo haya ni mambo ambayo yanahitaji kuyakemea, lakini Tanga nimeikuta hiyo kwamba watu wanavamia maeneo ya serikali tena kwasababu serikali haikuchukua hatua wakati watu wanavamia miaka 15, 20 iliyopita sasa tunajikuta kuna tatizo kwamba utamkuta mtu amekaa mahali miaka 15 iliyopita kuanzia anazaliwa mpaka anamaliza shule, yeye anajua pale ni kwao kumbe wazazi wake walivamia" alifafanua.

"Na sasa Rais wetu na Amiri Jeshi mkuu ametupa mwongozo wakuu wa Mikoa, sheria ipo, vyombo vya dola vipo, amri ipo na mabavu yapo lakini pia na busara ipo na upole upo, na Mwenyezi Mungu ni Rahim na anapenda wanadamu wake wake wawe Rahim, sasa kama watu wamefanya kosa hilo ni vizuri wakakiri kwamba walifanya kosa ili serikali sasa itafute huruma na  namna ya kufanya ili kumaliza matatizo haya" alisisitiza.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.