Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Ambae Pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar Mhe Dk.Hussein Ali Mwinyi Amewatunukia Shahada za Uzamili na Uzamivu Wahitimu wa Mahafali ya 17 ya SUZA leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa  cha Zanzibar (SUZA)  Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimtunukia Shahada ya Uzamivu ya Kiswahili “Doctor of Philosophy in Kiswahili” ya Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Muhitimu Saade Said Mbarouk, katika hafla ya Mahafali ya 17 ya (SUZA) yaliofanyika katika ukumbi wa Dk.Ali Mohamed Shein Tunguu (SUZA) Wilaya ya Kati Unguja

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la  Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakubaliana na hatua zilizoanza kuchukuliwa na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) katika kuufanyia masahihisho muundo wa Utumishi ili kuhakikisha Wahadhiri na Wafanyakazi wa Chuo hicho wanalipwa kwa mujibu wa nafasi zao, muda na kiwango  cha elimu.

Dk. Mwinyi ambae pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), amesema hayo katika Mahafali ya 17 ya Chuo hicho, yaliofanyika katika Ukumbi wa Dk. Ali Mohamed Shein, uliopo Tunguu Mkoa Kusini Unguja.

Alisema kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Wahadhiri na Wafanyakazi wa Chuo hicho, Serikali inakubaliana  na hatua zilizoanza kuchukuliwa na Uongozi wa Chuo hicho katika kuangalia upya na kuufanyia masahihisho muundo wa Utumishi, ili kuhakikisha kila mmoja anapata stahiki zake kwa mujibu wa nafasi, muda wa utumishi na kiwango cha elimu.

Alieleza kuwa Serikali inatambua kuwepo kwa taratibu za upandaji wa madaraja kwa taasisi za elimu nchini, hivyo akabainisha suala hilo kuzingatiwa kikamilifu.

Aidha alisema Serikali ina azma ya kushirikiana na Uongozi wa Chuo hicho pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika kuitafutia ufumbuzi changamoto ya uhaba wa Wahadhiri  na watumishi wengine wa chuo hicho, ili kuziba nafasi zilizo wazi kufuatia hatua ya Serikali ya kuwateua wahitimu wengi kushika nafasi mbali mbali za uongozi Serikalini.

Dk. Mwinyi aliutaka Uongozi wa SUZA kuandaa utaratibu mzuri wa kupata Wahadhiri miongoni mwa waihitimu wake bora, sambamba na kuwaendeleza wahitimu waliopo na watumishi wa kada nyingine, kwa kuandaa program maalum za mafunzo ili kupanua wigo na kuwawezesha wale wenye sifa na ambao bado hawajapata mafunzo; kupata nafasi hizo.

Alisema Uongozi wa Chuo hicho una wajibu wa kutafuta njia mbadala za kupata fedha , ikiwemo mikopo na kuanzisha miradi ya maendeleo iyakayokiletea faida chuo hicho, na akibainisha kuwa mfumo wa aina hiyo umekuwa ukitumiwa na vyuo mbali mbali Duniani kama njia ya kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya aina mbali mbali ya Chuo,.

“Nikupeni moyo kuwa Serikali ipo tayari  kutoa dhamana , kwa taasisi za fedha  kwa mikopo  ambayo tutajiridhisha itakisaidia chuo kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo”, alisema.

Alieleleza kuwa Chuo Kikuu ni taasisi na kiungo cha mshirkiano kati yake   na watu, hivyo akatoa wito  wa kuwa na mashirikianpo na vyuo vikuu vyengine ili kujifunza mambo mapya, kubadilishana uzoefu, kushirkiana katika masuala mbali mbali ya kitaaluma pamoja na kufanya tafiti.

Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi aliwapongeza wahitimu wote, hususan wa kike kwa kuwa na idadi kubwa ya wahitimu, ikilinganishwa na wanaume pamoja na kushika nafasi nyingi za juu katika masomo mbali mbali.

Aliwataka wahitimu wote  kutotosheka na ngazi ya elimu waliyofikia na badala yake kuanza juhudi za kujiendeleza zaidi kimasomo pamoja na kuwataka kuitumia vyema taaluma waliyopata katika kujiletea mabadiliko na kujiajiri au kuajiriwa kwa kuzingatia sifa na uwezo walionao.

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Simai Mohammed Said

alisema Wizara hiyo ina azma ya kujenga ukaribu na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili kuwawezesha vijana wanaohitimu kuweza kuingia katika soko la Ajira katika maeneo tofauti Duniani.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Ali Khamis  akiwa pia ni Mjumbe wa Baraza la Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, alisema katika mwaka wa masomo 2020/2021  Baraza limeweza kusimamia uendeshaji, wajibu na haki za wahadhiri na wafanyakazi  wa chuo hicho, ikiwemo suala la upatikanaji wa stahiki zao pamoja na upandishaji wa madaraja.

Alieleza kuwa Baraza hilo lilipata fursa ya  kujadili na kuchambua changamoto mbali mbali zinazowahusu  wahadhiri na wafanyakazi  wa chuo ili kuhakikisha ufanisi  wa kitaaluma unapatikana, ikiwemo suala la kupishana sana kwa mishahara.

Aidha, Makamo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Pro. Mohamed Makame Haji alisema mafanikio ya chuo hicho ya kuendelea kutoa idadi kubwa ya wahitimu kuwa sio jambo la kubahatisha, bali linatokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Alisema mafanikio hayo yanatokana na umoja na mashirikiano ya wadau wote wa elimu, ikihusisha Uongozi wa SUZA  pamoja na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Alieleza kuwa katika mwaka huo wa masomo (2020/2021) chuo hicho kilikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo ya kutokuwa na  Dakhalia za kutosha katika baadhi ya Skuli zake pamoja na kutokuwa na  miundombinu bora katika baadhi ya Dakhalia.

Vile vile alisema kumekuwepo mlundikano mkubwa wa wahadhiri  katika baadhi ya Skuli na taasisi  za Chuo hicho, ikiwemo Chuo cha uongozi wa  Fedha Chwaka.     

Katika Mahafali hayo, jumla ya Wahitimu 1894 wa fani na ngazi mbali walitunukiwa Vyeti, Stashahada, Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu kutoka taasisi na   Skuli mbali mbali za Chuo hich.o, ikiwemo Skuli ya Kilimo, Skuli ya Komputa,Mawasiliano na Taaluma ya Habari,Skluli ya Biashara na Taasisi ya Utalii.                        

Nyengine ni Skuli ya Afya na Sayansi za Tiba, Skuli ya Elimu, Skuli ya Sayansi Asili na Sayansi Jamii na Skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni.

Aidha, katika hafla hiyo Rais Dk. Mwinyi alitunuku zawadi kwa wanafunzi bora waliofanya vizuri zaidi katika masomo mbali mbali.

Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.