Habari za Punde

WANAHARAKATI: ‘Changamoto hazitukatishi tamaa kupambana na udhalilishaji’

Na.ZUHURA JUMA, PEMBA

DUNIA ikiwa katika siku 16 za kuhamasisha mapambano ya ukatili na udhalilishaji, wanaharakati Pemba wanapaza sauti zao wakionesha kutofurahishwa na yanayotendeka ndani ya jamii.

Wanaharakati wa masuala ya udhalilishaji wametaja kwamba, muhali, kuitwa majina mabaya, rushwa na kukataa kutoa ushahidi ni miongoni mwa sababu za kuongeza matukio hayo.

Jamii imegubikwa na mambo ambayo inakaribia kuwakatisha tamaa wanaharakatia katika mapambano dhidi ukatili na udhalilishaji kwa wanawake na watoto.

Zipo changamoto mbali mbali zinazowakabili wanaharakati wa masuala ya udhalilishaji, ingawa imekuwa ni fursa kwao kwani inawapa nafasi ya kutafuta mbinu mbadala ya kudhibiti.

Ikiwa dunia inaadhimiasha siku 16 za kupinga udhalilishaji, mwandishi wa makala haya aliwasaka wanaharakati mbali mbali ili kujua kinachowakamisha wakati wa mapambano dhidi ya udhalilishaji na jinsi gani wanatatua.

WARATIBU WA WANAWAKE NA WATOTO WA SHEHIA

Waratibu wa wanawake na watoto wa shehia wanaeleza kwamba, changamoto zinazowakumba zimekuwa zikirudisha nyuma juhudi zao za kupambana na udhalilishaji.

Wanadhalilika na kuvunjiwa heshima kwa kuitwa majina mabaya na kutishiwa amani, jambo ambalo linawatia hofu kila siku zinapoendelea.

Mbeu Makame Bakar ambae ni Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mchangamdogo Wete anasema, kwa vile wanaibua matukio ya udhalilishaji, wanaonekana ni watu mafisadi na wanaofitinisha familia na majirani.

“Tunaibua kesi za udhalilishaji ili makusudi kuwasaidia wao, lakini wanatuona wabaya”, anasema.

Wanafanya kazi ngumu huku wakiwa na hali duni ya kimaisha, hali ambayo inasababisha kushindwa kufuatilia matukio ya udhalilishaji kwa wakati.

Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Piki Bikombo Shazil Makame anasema, wanaposikia tukio na kuanza kulifuatilia wanafikwa na mitihani mikubwa, kwani wanaonekana wanafuatilia mambo yasiyowahusu.

“Nishawahi kupelekwa kituo cha Polisi kwa kufuatilia tukio la mtoto anaedaiwa kupewa ujauzito, kwa kweli tuna hali ngumu, tunahitaji mashirikiano ya kila upande, ili tusivunjike moyo”, alieleza.

Watoto wenye umri mkubwa wanawakatisha tamaa ya kuendelea kuyaibua matendo hayo, kwa sababu wanakataa kutoa ushahidi na hatimae mtuhumiwa anaachiwa huru.

“Hawa wenye umri kuanzia miaka 13 wanatupa shida sana, kwa sababu hawataki kusema ukweli na pia wanakuwa kigeugeu, tunaomba ushahidi wao uchukuliwe wa awali tu”, alieleza.

Mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Mjiniole Khadija Henoick Maziku anasisitiza usiri katika mapambano hayo, kwani wanayokumbana nayo ni makubwa na yanahatarisha maisha yao.

Ukatili umekuja na sura mpya kutokana na wadhalilishaji ni ndugu, watu wa karibu, jirani, baba na kaka, hivyo tatizo wanapoligundua tayari limeshaleta athari.

“Wazazi wanaficha kwa sababu kuna matukio mengi ambayo yamesababishwa na baba, kaka lakini tunapowafuata ni vigumu kusema”, anasema.

Akitoa ushahidi wa kesi katika shehia yake kuna kijana wa miaka zaidi ya 20 alimbaka ndugu yake wa miaka 14, ingawa wazazi hawataki kutoa ushirikiano.

“Sijachoka kufuatilia lakini kwa inavyokwenda, kufanikiwa kwangu ni kudogo mno, kijana wa kiume ameshakimbia tangu alipofanya tukio hilo na mama mzazi anasema hataki mwanawe afungwe”, anahadithia mratibu.

Kesi nyengine ni ya mtoto wa miaka 16 kubakwa na baba yake mzazi, ingawa alifanikiwa kutoroka na kumfuata mama yake nje ya Tanzania baada ya kuchoshwa na udhalilishaji aliokuwa akifanyiwa.

Anasema, ili wafanikiwe kudhibuti vitendo hivyo inabidi wale walengwa watoe ushirikiano, ingawa sio rahisi kutokana na familia ndio inayowatendea watoto udhalilishaji.

Hakukaa kimya mratibu wa wanawake na watoto shehia ya Shengejuu Salma Abdalla Hamad na kueleza, kila baada ya nyumba nne tano katika shehia unakuta mtoto wa kike anamnyonyesha mtoto mwenzake aliemzaa.

“Hali inatisha ndani ya jamii zetu, watoto wanaangamia huku wazazi wakibaki kimya, sijui tulaumu wapi na nani katika jambo hili, juhudi zinafanyika ila bado hali ni tete”, anasema mratibu huyo.

Wanafanya kazi ya kujitolea ingawa wanakaribia kushindwa kutokana na jamii kutokuwaunga mkono, huku wakikosa hata pesa ya sabuni.

WANAHARAKATI WA ASASI ZA KIRAIA

Mratibu Tatu Abdalla Mselem wa Jumuiya ya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE) anasema, kufuatia siku 16 wanatakiwa wajitathimini katika kazi wanazofanya na changamoto zao, jamii ikoje na kuweka mbinu itasaidia kupiga hatua mbele.

“Tunatakiwa tuondoke na azma ya kuondoa matatizo kupitia siku hizi, wanaharakati tunapambana na changamoto nyingi kwa sababu hatupewi ushirikiano kwa jamii, akinababa wanapokea pesa, mama anataka kesi iende mahakamani, hivyo tunavutana”, anaelezea.

Anahadithia kesi ya mtoto ambae ameathiriwa vibaya baada ya kudhalilishwa ingawa baba yuko upande wa mtuhumiwa kwa vile anapewa rushwa ya pesa.

“Alimwambia mke wake kesi imalizwe, lakini dada wa mtoto alisimamia ili mdogo wake apate yake, lakini kila anaporudi kufuatilia anatukanwa na baba yake, mwisho aliona aiache”, anaelezea.

Wale wanaotegemewa kuwa ndio wasimamizi, walezi, watakaosimamia haki za watu ndio ambao wanazivunja na ndio maana tatizo hilo linakuwa kubwa.

Changamoto zilizopo ni kubwa ingawa hawakati tamaa kwani ndio sifa ya mwanaharakati, kadiri wanavyopiga hatua wanajikuta wanakuwa na jambo moja ambalo tayari umeshalifanyia kazi.

Mratibu Fat-hiya Mussa Said kutoka Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Tanzani (TAMWA) kwa upande wa Pemba, wana changamoto nyingi kwa sababu bado jamii imegubikwa na rushwa muhali.

Wanajitahidi kuibua kesi na kuzifikisha Polisi ingawa wazee wanaporudi nyumbani wanasuluhisha na ndio maana hawaendi kutoa ushahidi mahakamani au wanapokwenda wanaharibu ushahidi.

“Tunapeleka juhudi hizi mbele, lakini familia zinaturudisha nyuma, tunaumia sana kwa sababu hata ufanye nini hufaniki ikiwa wenye kesi hawajawa tayari, lakini tunaendelea kupambana”, anasema.

Hali hiyo imesababisha watendaji wa makosa kuachiwa huru, jambo ambalo linawarudisha juhudi zao pamoja na vyombo vya sheria ambavyo vina kazi kubwa ya kusimamia haki ili ipatikane.

WANAHARAKATI WA TAASISI ZA KISERIKALI

Mkuu wa Idara ya Jinsia na Watoto Pemba Mwanaisha Ali Massoud anasema, wanakabiliwa na chanamoto nyingi wakati wa kufuatilia matukio ya udhalilishaji ikiwa ni pamoja na watu kukataa kutoa taarifa sahihi.

Wanakosa mashirikiano kutoka kwa wahusika ambayo yangeweza kuwasaidia kujua ukweli wa tatizo lililotokea, ingawa linaturudisha nyuma katika upatikanaji wa haki kwa wateja wao.

“Tunajitolea zaidi lakini ukosefu wa nyenzo za kufikia maeneo husika ni tatizo, elimu inahitajika zaidi kwa wanajamii ili wafahamu viashiria vya udhalilishaji na namna ya kuvidhibiti mapema”, anasema.

Bizume Haji Zume ambae ni Afisa Jinsia na Watoto Wilaya ya Micheweni anasema, bado wanajamii hawajazielewa harakati zinazofanywa kwa ajili ya kudhibiti udhalilishaji.

“Kuna changamoto zinatukwaza sana kwani licha kulivalia njuga jambo hili lakini bado jamii inaendelea kuwakosesha wanawake haki zao ikiwemo umiliki wa ardhi, kuwapokonya mahari yao, kutelekezwa pamoja na watoto wakifanyiwa ubakaji na ulawiti”, anafahamisha.

VYOMBO VYA SHERIA

Ali Amour Makame Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Pemba, anaamini kwamba ushahidi unaotolewa na hukumu zinazotolewa sio sahihi kwani haziendi kwa mujibu wa sheria, na ndio maana zinapomaliza kesi wanaomba kukatiwa rufaa.

“Kesi zinapata hukumu lakini nyingi watuhumiwa wanaachwa huru, nakumbuka kuanzia Aprili hadi Oktoba mwaka huu kuna kesi zisizopungua 20 zimepata hukumu lakini 14 kati ya hizo zimeachiwa huru na katika hizo, 12 tumeenda rufaa”, anaeleza.

Anafafanua kuwa, wakati mwengine mashahidi wanafika na kutoa ushahidi vizuri, ingawa inapokuja hukumu maamuzi yanayotolewa yanawastaajabisha sana.

Changamoto nyengine inayowakwaza ni mashahidi kutokutoa ushahidi vizuri ama kukataa kabisa hasa wale wenye umri wa miaka 16 na 17.

“Unapomsimamisha mtoto anatoa ushahidi vizuri lakini unapomwambia tuoneshe huyo mtuhumiwa, anakwambia hayupo mahakamani, mara yupo Unguja, mara Tanga, na ndio kesi nyingi hizo”, anasema Wakili huyo.

“Kuchelewa kuripoti tukio na kusameheana wao kwa wao ni tatizo kubwa, kwa sababu unawapigia simu mpaka unachoka hawaji mahakamani, nishawapigia zaidi ya watu 20 lakini majibu yao ni kwamba wameshasuluhishana”, anafahamisha.

Hakimu wa Mahakama ya Mkoa Wete Abdalla Yahya Shamhun anasema, changamoto zinazowakabili katika kupambana na makosa hayo ni jamii kukataa kutoa ushahidi, hali inayosababisha watuhumiwa kuachiwa huru.

“Kwa mfano ile kesi ya Mtambwe ya baba anaedaiwa kumbaka mwanawe wa kambo, mtoto alisema mama yake alimuona lakini tulipomwita mama hakuja, kwa hiyo ushahidi ulikuwa na shaka”, anasema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Juma Sadi Khamis anasema, wanapokea kesi nyingi lakini wazazi wanaporudi nyumbani wanasuluhishana, hivyo wanapohitaji ushahidi hawatoi tena ushirikiano.

“Mzazi anakuja hapa kulipoti akiwa yupo moto, lakini kinachotushangaza, mara ya pili ukiwaita hawataki kusema kwa sababu tayari wameshakaa pamoja na kusuluhishana, hivyo siku 16 tuwe na mikakati kuhakikisha tunadhibiti hali hii”, anafahamisha.

MAFANIKIO

Miongoni mwa matukio ambayo yamempatia mafanikio Afisa Jinsia na Watoto wa Micheweni Bizume Haji ni shehia ya Maziwa Ng’ombe, baba mmoja alimtelekeza mke na watoto baada ya kwenda dago kuvua, lakini walifanya jitihada na hatimae alirudi kuishi na familia yake.

“Alipofika huko nje ya Tanzania alioa mke mwengine na yule wa huku alimtelekeza lakini baada ya kumpelekea barua alirudi na sasa anaishi hapa na wake zake wawili”, anasema.

Mwanaisha Ali Massoud ambae ni Mkuu wa Idara ya Jinsia na Watoto anaelezea, wamefanikiwa sana kutokana na wananchi kupata mwamko wa kuripoti matukio hayo kila siku.

“Siku 16 za kupinga udhalilisha tujiulize ni namna gani kesi zikiripotiwa zinapata hatia, kwa sababu zinaripotiwa nyingi lakini watuhumiwa wanaachiwa huru kwa sababu jamii haitaki kutoa ushahidi”, anaeleza.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anasema mafanikio yapo kwa kiasi, kwani wapo walioonesha utayari katika kusimamia vizuri kesi zao na zinapata hatia.

Juhudi mbali mbali zinafanyika ikiwa ni pamoja na kubadilisha sheria ili kuhakikisha wanapambana na vitendo hivyo na ndio maana dk, Hussein Mwinyi akaunda mahakama maalumu kwa lengo la kumaliza udhalilishaji.

NINI KIFANYIKE

“Tusiyafiche wala tusiyafumbie macho matukio haya kwani ni janga hatari linaloendelea kuwatesa na kuwadumaza watoto, athari yake ni kubwa katika maisha ya mbele”, anasema kwa uchungu mratibu wa Shengejuu Salma Abdalla.

Mratibu wa TUJIPE Tatu Abdalla Mselem anasema, katika mahakama maalumu za udhalilishaji ambazo ziliundwa hivi karibuni, kunahitajika mahakimu wapya ili waone mabadiliko.

“Mahakimu waliopo tumewalalamikia tangu mwaka 2019 kwamba hawatufai kwa kesi za udhalilishaji, lakini imeundwa mahakama maalumu ila wameachwa wale wale, tutegemee nini?”, anasehoji.

Anasema, rushwa ya pesa bado ni tatizo kubwa linalohitaji kuondoshwa kwa nguvu zote, kwani dk, Hussein Mwinyi kila siku anaumiza kichwa kutafuta njia mbadala ya kuona matukio ya udhalilishaji yanadhibitiwa.

Mwanaisha Ali Massoud anafahamisha, elimu inahitajika katika madrasa, skuli, misikitini na kwenye jamii ili wanaharakati kupata mashirikianao pale wanapokwenda kufuatilia.

Bizume Haji Zume anawataka akina baba wasiwatelekeze akina mama na watoto na wawape huduma stahiki ili kuepuka kuwadhalilisha na kudhalilishwa na wengine.

Mratibu wa TAMWA Pemba Fat-hiya Mussa Said anaishauri jamii itoe ushirikiano kupambana kwa pamoja, sio wanaharakati wapambane wao wakae kwenye mikeka na kusuluhishana.

Tatu Abdalla Mselem yeye ni mratibu wa TUJIPE asisitiza kutolewa elimu kwa wanafunzi wa chuo cha mafunzo, kwani wanaporudi kwenye jamii wanaendelea kuwadhalilisha watoto.

Tangu kuanzishwa mahakama maalumu ni kesi 29 ambazo zimetolewa hukumu kati ya kesi 88 zilizofikishwa katika mahakama za Mkoa Wete na Chake Chake.

Ingawa kesi 19 zimeachiwa huru kutokana na jamii kukataa kwenda mahakamani kutoa ushahidi, hivyo kupitia siku 16 ya kupinga udhalilishaji ipo haja jamii ijitathmini ili kuhakikisha matukio hayo yanaondoka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.