Habari za Punde

Mijadala juu maboresho ya lugha ya Kiswahili inatakiwa kufanyiwa kazi kwa maslahi ya pande zote za Muungano - Wito

Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ya Muungano(JMT), Ndugu Khamis Siasa Hamisi  (kushoto)na Ndugu Haji Janabi ( kulia)
Washiriki waliohudhuria  kikao cha pamoja cha wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ya Muungano(JMT),kilichfanyika Zanzibar leo
Kaimu Katibu Mtendaji  Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Bi Consolata Mushi akitoa mchango wake katika kikao cha pamoja cha wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ya Muungano(JMT),
 
Na Adeladius Makwega, Zanzibar.

Mwenyekiti na makamu mwenyekiti wa vikao vya pamoja ambao pia ni Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na ya Muungano(JMT), Ndugu Khamis Siasa Hamisi na Ndugu Haji Janabi  kwa pamoja wamesema kuwa mijadala juu maboresho ya lugha ya Kiswahili inatakiwa kufanyiwa kazi kwa maslahi ya pande zote za muungano hata kama jambo linalojadiliwa si la muungano.

Hayo yamesemwa Januari 13, 2022 Mjini Zanzibar katika kikao cha pamoja kikiwa kukutanisha wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara hizo na wataalamu kama utangulizi ili kufanyika kikao cha Makatibu Wakuu wa wizara hizo wa JMT na SMZ.

“Kiswahili kimepitia hatua mbalimbali tangu watunzi wa lugha ya Kiswahili wakiwamo Shabani Robert, hata viongozi kadhaa wa kitaifa kama vile Julius Nyerere, Abeid Karume na wengine walikuwa wakitoa maagizo kadhaa ambayo yalikuwa na shabaha ya kukikuza Kiswahili ambayo kwa hakika yalitekelezwa” Alisema Mwenyekiti Siasa Khamisi.

Akifafanua zaidi makamu mwenyekiti wa kikao hicho Ndugu Janabi amesema kuwa ni wajibu wataalamu kuyaweka malengo yetu vizuri ili pale panapofanyika utekelezaji mambo yanakuwa mepesi na si vinginevyo.

Wakichangia katika mjadala huo baadhi ya washiriki wamesema kuwa pale panapotokea maneno yanayotumiwa kama yana ukakasi ni wajibu wa taasisi zinazosimamia lugha ya Kiswahli na utamaduni wetu kutafuta visawe kuondoa utata huo.

Akitololea mfano Kamishina wa Utamaduni wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Omari Salum Mohammed amesema kuwa katika lugha ya Kiswahili yapo maneno yanayotumika bara lakini visiwani yanakuwa mazito

“Neno ZAMISHA ambalo linatokana na neno la msingi ZAMA neno hilo linaweza kumaanisha tumbukia katika maji na wakati huo linaweza kuwa ni kipindi fulani cha wakati. Zama ya kutumbuki inatoa maneno mengine kadhaa kama zamivu na kadhalika lakini kwa Zanzibar neno hilo lina ukakasi, mtu anapomzamisha mtoto baharini linakuwa zito kwa yule anayesikiliza.” Alisema Dkt Mohammed.

Kwa upande wao Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) Kaimu Katibu Mtendaji Bi Consolata Mushi alisema kuwa sasa wameandaa mkakati wa kutoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa Wasanii na Washereheshaji ili kusaidia matumizi ya Kiswahili fasaha na sanifu nchini.

“Tumejipanga vizuri katika hilo kwani tumekusudia mno kushirikisha wadau mbalimbali, ikiwamo serikali kuu, Serikali za Mitaa, balozi,vyuo vikuu na wafadhili ili kuweza kufikia malengo hayo.” Aliongeza Kiongozi huyo wa BAKITA.

Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wajumbe Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili  Zanzibar (BAKIZA) Dkt Mwanahija Ali Juma amesema kuwa kwa hakika michango ya wataalamu wote wanaoshiriki kikao hicho imepokelewa na yanafanyia kazi kwa pamoja, yaani BAKIZA na BAKITA.

“Kwa sasa tunajitahidi angalau kuwa na kamusi za mifukoni na karatasi ndogo ndogo ambazo zinaweza kuwasaidia watalii na wageni wengine wanaofika hapa nchini kwa kufanya hivyo wageni hao wataweza kuwasiliana na wenyeji kwa urahisi mkubwa.”

Aliongeza Dkt Mwanahija.

Kikao hicho kinatarajiwa kuendelea kwa hatua za Makatibu Wakuu wa serikali ya JMT na SMZ.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.