Habari za Punde

Serikali imefanikisha zoezi la upimaji wa ardhi

 Rahma Khamis - Maelezo                 3/1/2022

Waziri wa Ardhi na  Maendeleo ya Makaazi Zanzibar amesema serikali imefanikisha zoezi la upimaji wa ardhi katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, ili kupunguza uhaba wa maeneo ya makaazi  kwa wananchi

Alisema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji  katika Ukumbi wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Kikwajuni Mjini Unguja, Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi Mh Riziki Pembe Juma ikiwa ni shamrashamra za kutimiza miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema tatizo la uhaba wa maeneo lipo hivyo wameamua kuanzisha miji mipya katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kilimani ambayo utajumuisha majengo ya makaazi, biashara ofisi na huduma za kijamii.

Amesema kuwa Wizara imefanikisha upimaji wa maeneo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi ikiwemo viwanda ambapo jumla ya hekta 61 katika kijiji cha Dunga na hekta 135 katika eneo la pangatupu yamepimwa kwa ajili ya uwekezaji wa  viwanda hivyo.

Aidha amefahamisha kuwa Wizara imekamilisha mapitio ya sheria zote za ardhi kwa ngazi ya wataalamu, ili kuhakikisha sheria  zinaendana na mazingira ya sasa na kuepusha migogoro ya ardhi kwa wananchi.

“Tumefanikisha hatua ya kuweka ardhi ya akiba katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ili kuiweka ardhi ya akiba kwa matumizi ya badae”,alisema Wazir Pembe.

Katika hatua nyengine Waziri ameeleza kuwa Wizara kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa imetenga maeneo kwa ajili ya wajasiriamali wadogo Unguja na Pemba ili kuwawezesha wananchi  kujiendeleza kiuchumi.

Pia ameongeza kusema kuwa katika kutekeleza majukumu Wizara imefanya utatuzi wa migogoro 498 ya ardhi na bado inaendelea kufatilia migogoro ambayo haijatatuliwa ili kuipatia utatuzi.

Hata hiyo Waziri Pembe ametoa wito kwa wananchi ambao wanadaiwa na hawajalipa  madeni ya kodi zao walipe madeni  ili kwa kuleta maendeleo nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.