Habari za Punde

WanaCCM watakiwa kuitangaza ilani ya chama


 MJUMBE wa Sekretariet ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Gilbert Kalima,akizungumza na wanachama wa shina namba 10 Tawi la Mkokotoni Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’ Kichama Unguja.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini wametakiwa kusema na kutangaza Utekelezaji wa Ilani ya Chama unaotekelezwa na Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar ili wananchi wapate taarifa sahihi juu ya maendeleo endelevu yaliyofikiwa.

Rai hiyo imetolewa na Mjumbe wa Sekretariet ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Gilbert Kalima, alipokuwa akizungumza na Wana CCM wa shina namba 10, Tawi la Mkokotoni Jimbo la Tumbatu Wilaya ya Kaskazini ‘’A’’ Kichama Unguja.

Alisema Serikali zinatekeleza kwa kasi kubwa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 katika maeneo mbalimbali nchini lakini bado baadhi ya wananchi hawajui na hawapati taarifa sahihi ya  miradi mikubwa inayotekelezwa katika maeneo yao.

Alisema ni wajibu wa kila Mwana CCM kuzisemea mazuri Serikali hasa kwa mambo mengi yanayotekelezwa kwa maslahi ya wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa,kidini na kikabila.

Kalima, alifafanua kwamba ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja kunatekelezwa miradi mikubwa ya kimkakati itakayoinua uchumi wa nchi na kipato cha mtu mmoja mmoja hivyo ni lazima Wana CCM wajipange vizuri kuwa wa mwanzo kunufaika na fursa hizo.

Alisema katika Mkoa huo kunajengwa Bandari kubwa za mizigo,abiria,mafuta,gesi na kuwekwa miundombinu bora ya uvuvi wa kisasa sambamba na kujengwa Hospitali kubwa ya Wilaya itakayopunguza upungufu wa huduma bora za Afya ambayo itagharimu zaidi ya Bilioni 4 zinazotokana na mfuko wa UVIKO-19.

“Katika ziara hii nimejionea miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ile ya Uchumi wa Bluu itakayojumuisha vikundi vya Akina Mama na Vijana vya ujasiriamali.

Wito wangu tuhakikishe CCM Mkoa huu tumejipanga vizuri watu wetu wawe wanufaika wa mwanzo kwa kila sekta kwani ajira 300,000 zilizoadiwa katika Ilani ya CCM zitatokana na fursa hizo”,,alisema Kalima.

Katika maelezo yake Kalima, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa aliwasisitiza Wana CCM hao kuchagua viongozi bora katika uchaguzi Mkuu wa Chama mwaka 2022 watakaowavusha na kusimamia maslahi ya chama  bila hofu.

Aidha aliwataka wananchi na wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la sense ya watu na makaazi inayotarajiwa kufanyika mwaka huu wa 2022 ili kutoa fursa kwa Serikali kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo.

Aliwasisitiza wanachama hao kufanya vikao vya ngazi ya shina kwa wakati ili kujadili kwa kina changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo ili zipatiwe ufumbuzi na Serikali.

Naye Mbunge wa Jimbo la Tumbatu Mhe. Juma Othman Hija, alimwambia kwamba hali ya Kisiasa ndani ya Jimbo hilo ipo vizuri na wanaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujikimu kimaisha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shina namba 10 Mwanakombo Mtumwa Ali, aliipongeza Sekretariet ya H/KT kwa uamuzi wake wa kuwapelekea Kiongozi wa ngazi za juu ndani CCM ili azungumze na wanachama hao hatua hiyo imeongeza ari na faraja kubwa kwa Wana CCM hao.

Alisema katika shina hilo wamekuwa Mabalozi wazuri wa kuimarisha suala la amani na utulivu nchini ajenda ambayo wamekuwa wakiijadili katika vikao vyao mbalimbali.

Kupitia risala ya Shina hilo walikiomba Chama kuwawezesha kiuchumi kwa kuwapatia mabalozi posho la kujikimu ili waweze kutekeleza kazi zao kwa ufanisi zaidi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.