Habari za Punde

Wananchi Watakiwa Kuwajibika Ipasavyo Katika Shughuli Wanazofanya -Alhaj Dk.Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kuwasalimia Waumini wa Kiislam baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika  Msikiti wa Maisara Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo 14-1-2022.
WAUMINI wa Dini ya Kiislam wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi.(hayupo pichani) akizungumza na kuwasalimia baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Maisara Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Sheikh Alhadi Mussa Salum na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi, baada ya kumalizika kwac Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Maisara Wilaya ya Mjini Unguja


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi kuwajibika ipasavyo katika shughuli wanazofanya ili Taifa liweze kufanikisha dhamira ya  kupata maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo katika salamu alizotoa kwa waumini wa dini ya Kiislamu; baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliofanyika Masjid Meman, Maisara Jijini Zanzibar.

Amesema ili nchi iweze kupata maendeleo makubwa, ni lazima kwa kila mwananchi mahala alipo kuwajibika ipasavyo katika shughuli anazofanya  na kufanya kazi kwa bidii.

Alieleza kuwa Dunia inakabiliwa na mdororo wa kiuchumi unaotokana na kuibuka kwa Ugonjwa wa Uviko -19, na hivyo  kusababisha kushuka kwa uzalishaji katika sekta mbali mbali, hatua iliofanya bei ya bidhaa kupanda.

Akitolea mfano, Alhaj Dk. Mwinyi alisema hivi sasa gharama za usafirishaji wa Kontena moja kutoka nchini China hadi Zanzibar ni Dola za Kimarekani 13,000, wakati ambapo kabla ya kuzuka kwa ugonjwa huo lilikuwa likisafirishwa kwa Dola za Kimarekani 3,000.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alisema hali imeanza kutoa matumaini na kubainisha baadhi ya mambo, ikiwemo shughuli za biashara kuanza  kukwamuka.

Katika hatua nyengine, Rais Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa wananchi kudumisha amani, utulivu na umoja ndani ya jamii kwa kigezo kuwa hakuna mbadala wake, sambamba na kuwa ndio msingi wa kupata maendeleo, huku akibainisha mambo hayo ndio njia ya kulitoa Taifa katika mkwamo wa kiuchumi unaotokana na Ugonjwa wa Uviko -19.

Nae, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alimuomba Mwenyezi Mungu kumjaalia kheri nyingi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi na kumpongeza kwa juhudi zake za kuutumikia Uislamu, kama ilivyo kwa mzazi wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.

Mapema, Khatibu wa Sala hiyo ya Ijumaa Sheikh Mussa Mohamed Mussa alieleza Dini ya Kiislamu kuwa ni Dini bora iliokuja kubainisha mfumo mzima wa maisha ya binadamu na  umuhimu wake katika kutenda mambo mema.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alifika Mpendae nyumbani kwa Mjane wa aliekuwa Mbunge wa Jimbo la Mpendae, Marehemu Salim Turky, na kuonana na Bi Tamima Swaleh kwa ajili ya kumsalimia.

Aidha, Alhaj Dk.Mwinyi alifika nyumbani mwa Mwanasiasa mkongwe Sukwa Said Sukwa eneo la Maungani  kwa ajili ya kumjuilia hali.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.